Featured Post

AHMED MOHAMMED KIPANDE NA KILWA JAZZ

Ahmed Mohammed Kipande

Na Daniel Mbega
Ahmed Mohammed Kipande (alizaliwa mwaka 1937, Kilwa Kivinje mkoani Lindi) alikuwa mwanamuziki wa Tanzania na kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz. Ahmed Kipande alishiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigani Uhuru wa Tanganyika akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz, ambayo siku Tanganyika ilipopata Uhuru Desemba 9, 1961 ilitumbuiza wimbo wa kusifia nchi hiyo kupata Uhuru kutoka kwa wakoloni. “Ewe Mola tunakuomba uibariki Tanganyika yetu na jirani  zetu, Uhuru tumepata lakini, Nyoyo zinasikitika wenzetu wanateseka, Wakoloni wamewashika…” ni mashairi yaliyokuwemo kwenye wimbo wa Uhuru.
Chini ya uongozi wa Ahmedi Kipande, Kilwa Jazz ilishiriki pia kutoa burudani wakati mikakati ya kufanya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye meneo ya makao makuu ya bendi hiyo jijini Dar es Salaam mwaka 1964. Ahmed Kipande na bendi yake waliteuliwa na serikali ya Tanganyika kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa Malawi mwaka 1963 na Uganda mwaka 1962.

Maisha yake ya awali
Ahmed Mohammed Kipande alizaliwa mwaka 1937 huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi. Miaka michache baada ya kifo cha mama yake, Ahmed Kipande alifuatana na baba yake kwenda Dar es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Uhuru Wavulana ilikuwa maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam. 
Kikosi cha Kilwa Jazz. 
Ahmed Kipande na 'midomo ya bata'
Katikati ya miaka ya 1950 Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo Violin katika bendi ya Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidosi. Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao hivi sasa unaitwa mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Ahmed Kipande aliyekuwa ametoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi naye akishirikiana na mwanamuziki mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Shamte wakaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958. Kilwa Jazz ikaanza kujizolea umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo za siasa, mapenzi na za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.
Alitunga na kuimba nyimbo kama TANU Yajenga Nchi, Nchi Yetu, Enyi Vijana Tujenga Yetu, Doli, It can be done, play your party, Mapenzi Yananivunja Mgongo, Roza Waua, Nipate lau nafasi, Nacheka cheka Kilwa leo na ule wa Maneno Hayafai.
Wimbo wa Nipate Lau Nafasi ulitungwa na Ahmed Kipande baada ya kunakili wimbo wa  Tabu Ley na John Bokelo wa Mokolo Nakokufa, hali kadhalika nyimbo za Nacheka cheka Kilwa leo, Rose Waua na Maneno Hayafai ambazo walizinakiri kutoka wimbo wa Course au Povouir na Est ce Que za T.P.OK. Jazz.
Mwaka 1973, Kilwa Jazz ilialikwa na kutumbuiza katika utangulizi wa onyesho la gwiji la muziki wa dansi Afrika, Franco Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz lililofanya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Luambo Makiadi baada ya kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake mkubwa wa ‘kokopi na kupesti’ pasipo kukosea.
Kilwa Jazz na usafiri wao
Makao makuu ya Kilwa Jazz yalikuwa katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako siku moja katika mwaka 1964 ilipiga muziki nje ya ofisi yao na kuwashangaza watu kuona bendi ikipiga muziki mchana. Lakini wakati ikipiga dansi hilo nje mchana kweupe, mipango kamambe ilikuwa ikipangwa katika maeneo hayo kwa viongozi wanamapinduzi siku chache kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12. Viongozi walikuwa wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Kisultani mwaka 1964 huko Zanzibar. Bendi ya Kilwa Jazz baadaye haikueleweka na jamii. Wengine wakafika mbali wakizusha maneno kwamba ni bendi ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika sherehe nyingi za kitaifa.
Kilwa Jazz pia ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za ndoa ya Oscar Kambona, wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Tanganyika. Katika sherehe hiyo, Ahmed Kipande alionyesha kipaji chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo wa papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao Oscar Kambona na mkewe. Yaelezwa kwamba Kambona aliinuka kutoka kwenye kiti cha maharusi na kwenda kumkumbatika Kipande kisha akamtunza kwa pesa.
Bendi hiyo ya Kilwa Jazz ilikuwa chini ya udhamini mkubwa wa Mzee Nangwanda Lawi Sijaona, ambaye anaelezewa kuwa alitoa mchango mkubwa wa hali na mali. Kilwa Jazz ilikuwa na wanamuziki wenye vipaji tofauti. Walikuwepo ambao walikuwa wakipiga ala za muziki zaidi ya moja pamoja na kuimba.
Ahmed Kipande alikuwa kiongozi, mtunzi wa nyimbo, alikuwa akiimba pia alikuwa hodari wa kupuliza ‘mdomo wa bata’ Saxophone. Duncan Njilima, Zuberi Makata na Hassan Shabani ‘Kichwa’ (kaka mkubwa wa Ahmed Kipande) wote walikuwa na uwezo wa kupiga gita la solo. Kwa upande wa saxophone walikuwepo akina Kisi Rajabu, Juma Town na Abbas. Waimbaji alikuwa yeye Ahmed Kipande, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ na Kassimu Mapili. Gita la kati lilikuwa likiungurumishwa na Abdul Mngatwa wakati drums zilikuwa zikicharangwa na Said na Abdallah Kanjo.
Upigaji wao wa muziki ulikuwa ukiwakuna vilivyo viongozi wengi wa siasa na serikali, ilifikia kiongozi mkubwa wa nchi wakati huo, Mzee Rashid Mfaume Kawawa alitoa ofa ya suti kwa wanamuziki wote wa Kilwa Jazz.
Katika maisha yake, Ahmed Kipande alifanikiwa kupata watoto sita.
Ahmed Mohammed Kipande afariki dunia Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa kipindi kirefu. Alizikwa kwenye makaburi ya Tandika Maguruwe, mkoani Dar es Salaam, Aprili 28, 1987.


Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.

Comments