Featured Post

ABETI MASIKINI


Elisabeth Finant
Kuzaliwa: Novemba 9, 1954
Mahali: Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kufariki: Septemba 9, 1994, Paris, Ufaransa

Elisabeth Jean Finant (alizaliwa Novemba 9, 1954 mjini Kisangani, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mwanamuziki wa Congo (zamani ikijulikana kama Zaire) ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Abeti Masikini.

Maisha yake ya awali
Elisabeth Finat au Abeti Masikini alitokea katia familia tajiri yenye watoto nane. Baba yake mzazi mzee Jean Finant, alikuwa chotara wa mchanganyioko wa Mkongo na Mbelgiji.
Mwaka 1961, Abeti Masikini alipatwa na pigo baada ya baba yake kuuawa kikatili mjini Mbuji Mayi kutokana na matatizo ya kisiasa. 
Mzee Finant alikuwa mwanachama wa cha MLC, kilichokuwa kikiongozwa na hayati Patrice Emery Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa Congo Leopoldville ambayo ndiyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya sasa. Ndiye shujaa wa uhuru wa nchi hiyo.
Hali hiyo ikamfanya mama yake Abeti Masikini kuchukua uamuzi wa kuhamia katika Jiji la Kinshasa ili apate kujihifadhi akiwa na wanawe. 
Wakiwa Kinshasa, mama yake alimchukua Abeti Masikini na kumrejesha darasani kwenye shule iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Lycee Ycee Sacre Ceur, ambayo kwa sasa inaitwa Bosongani.
Baada ya kumaliza shule ya sekondari, Abeti Masikini aliajiriwa kama Katibu kwenye Ofisi ya Waziri wa Utamaduni. 
Hata hivyo, kwa mshangao wa ndugu zake na familia nzima, Abeti Masikini aliamua kujiuzuru kazi hiyo na kuwaeleza nduguze kwamba mawazo yake yalikuwa kwenye fani ya muziki, na ndio wakati alipojipachika jina la ‘Betty’ likiwa kifupi cha Elisabeth, ingawa mashabiki wake wakaamua kumwita Abeti.
Mwaka 1971, chini ya usimamizi wa mwanamuziki Gerard Madiata, palitokea mashindano ya kumtafuta mwanamuziki chipukizi. Betty akaamua kushiriki kwenye mashindano hayo, ambayo kwa bahati mbaya hakufanikiwa kufaulu. 
Hilo halikumkatisha tamaa kwani ilionekana kama hamu yake ya muziki iliongezeka Zaidi licha ya umri wake kuwa mdogo wa miaka 17 wakati huo.
Ili aruhusiwe kutumbuiza akiwa mnenguaji wa kujitegemea, ilibidi ajiongezee miaka mitatu zaidi, ambapo alisema yeye alikuwa na miaka 20. 
Akiwa anasaidiwa na kaka yake Jean Aboumba Masikini aliyekuwa mpiga gitaa mahiri wa solo, Abeti akawa kila siku anafanya onyesho kwenye vilabu vidogo vidogo jijini Kinshasa.
Mwaka huo wa 1971, Abeti Masikini alikutana na Gerard Akueson jijini Kinshasa, raia wa Togo. Hapo ndipo fani yake ya muziki ilipoanza rasmi. Gerard Akueson ndiye akawa meneja wake mkuu tangu mwaka 1972. A
beti na Akueson wakaanzisha uhusiano wa mapenzi ingawa ndoa yao walifunga mwaka 1989 jijini Paris, Ufaransa ambaye walibahatika kupata watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume.
Mwaka 1973 mumewe huyo alimshauri wahamie katika nchi za Afrika Magharibi kwa matarajio ya kupata mafanikio zaidi. Wakiwa huko alipata mashabiki wengi sana kwenye nchi za Benin, Cote D’Ivoire, Togo, Niger, Nigeria, Guinea na Ghana.
Baada ya miaka kadhaa akiwa kwenye nchi hizo, Abeti Masikini aliamua kurudi Congo. Aliporejea mapokezi hayakuwa mazuri kwa kuwa watu wengi walikuwa hawamfahamu kabisa. Kilichomponza zaidi ni kwamba, katika kipindi chote hicho hakuwahi kurekodi hata albamu moja na kuiweka sokoni.
Changamoto nyingine ilikuwa ushindani uliokuwepo hasa wa bendi kubwa kama T.P. O.K. Jazz, Afrisa International, Zaiko Langa Langa, na nyinginezo na suala jingine ni kwamba, wanamuziki wanawake, hususan wa kujitegemea, walikuwa hawajapata nafasi ya kutosha wakati huo.
Lakini licha ya kutofahamika kwake, aliamua kufanya onyesho kubwa katikati ya Jiji la Kinshasa kwenye ukumbi wa CINE Palldium, lakini katika mshangao mkubwa aliambulia watu 12 pekee ambao ndio waliojitokeza kumuangalia. Tukio hilo halikumkatisha tamaa Abeti, aliendelea kufanya kazi kwa bidii ili malengo yake yakamilike.
Hatua ya kwanza aliyoifanya ni kufanya mazoezi kwa bidi ili kuboresha sauti yake. Baada ya kufanya mazoezi makubwa hatimaye mwaka 1973 alifyatua album yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina la Pierre Cardin ikiwa na nyimbo kadhaa zikiwemo Mutoto wangu, Bibile, Aziza, Miwela na Safariet Papy yaka. Album hiyo haikupokelewa vilivyo na wakazi wa jiji la Kinsahasa. Machoni mwao walimchukulia Abeti kama mgeni huku mashabiki wengine wakimlaumu kutokana na tabia yake ya kuimba nyimbo zake nyingi kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kilingala ama Kifaransa kama walivyofanya wanamuziki wengi.
Changamoto hizo zikamfanya aunde kundi lake alilolipa jina la Les Redoutables ambalo lilikuwa na wanenguaji wengi warembo na mahiri waliojulikana kama ‘Les Tigresses’. Ni wanenguaji hao waliofanya watu wengi waanze kuvutiwa naye.
Maonyesho yake katika Jiji la Kinshasa yakawa gumzo mitaani. Kazi alizokuwa akizifanya meneja wake ambaye ndiye mumewe, zikazaa matunda mema. Alifanikiwa kupata mkataba uliompeleka kwenda kufanya onyesho katika ukumbi maarufu wa Olympia katika Jiji la Paris, Ufaransa.
Mwaka1973 akiwa njiani kuelekea Paris kwenye onyesho hilo, alitua kwanza katika Jiji la Dakar nchini Senegal. Huko alifanya onyesho ambalo pia rais wa nchi hiyo wakati huo Leopold Seadar Senghor alihudhuria. Pesa zilizopatikana katika onyesho hilo alizitoa kama msaada wake kwa watu walioathiriwa kwa ukame nchini Senegal. Alipotua jijini Paris Februari 2, 1973 aliporomosha onyesho kabambe lililowavutia hasa mashabiki Wazungu kwenye ukumbi wa Olympia.
Abeti Masikini alifanikiwa kufanya onyesho jingine Juni 6, 1974 kwenye ukumbi wa Carnegie, jijini New York, Marekani.
Umaarufu wake ulizidi kuongezeka pale alipopewa fursa ya kutumbuiza kwa pamoja katika jukwaa moja na wanamuziki mahiri duniani kama James Brown, Miriam Makeba, Tabu Ley na Franco Luambo Makiadi, kabla ya pambano la masumbwi la kihistoria kati ya Mohammed Alli ‘Cassius Clay’ na George Foreman kwenye Uwanja wa Mei 26 jijini Kinshasa, Congo, pambano ambalo linafahamika zaidi kama ‘Rumble in the Jungle’.
Albam yake ya pili aliifyatua mwaka 1975 ikiwa na jina la La Voix Du Zaire. Nyimbo zilizokuwa zimesheheni katika albam hiyo ni Likayabo, Yamba yamba, Kiliki, Bamba, Nalikupenda na Ngoyaye.
Mwaka huo huo Abeti alipokea mwaliko kutoka kwa Bruno Coquatrix aliyekuwa mmiliki wa ukumbi wa Olympia wa jijini Paris. Akaenda kwa mara nyingine tena kufanya maonyesho kwa siku mbili mfululizo. Ni wakati huo alipopachikwa jina la utani la ‘Tigeress mwenye kucha za dhahabu’
Mwaka 1976 ulikuwa mbaya kimaslahi kwa Abeti Masikini. Alimpata mpinzani wa uhakika katika muziki aliyejulikana kwa majina ya M’pongo Love, aliyekuja juu kuliko yeye. M’pongo akaongoza Hit Parade kwenye radio ya taifa ya Zaire. Wimbo wake Pas Possible ulimfanya M’pongo kupendwa mno na mashabiki.
Pamoja na yote hayo, mwaka 1977 Abeti na M’pongo walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa na wengi. Walifanya onyesho kubwa kwa pamoja kwenye ukumbi wa ‘Cine Palldium’ katika Jiji la Kinshasa na kuacha simulizi kubwa. Kila mmoja aliimba kwa namna yake. Wakaweka misingi mizuri ya kupendana kwa wanamuziki wa kike wa kizazi kijacho.
Historia ya Abeti Masikini itaendelea kukumbukwa daima kwa kuwa yeye ni darasa tosha. Wanamuziki wengi maarufu wamepitia kwenye bendi yake wakiwemo akina M’bilia Bel, aliyekuwa mnenguaji toka 1976  hadi 1981, Lokua Kanza aliyekuwa mpiga gitaa mwaka 1980 hadi 1981, Abby Surya aliyekuwa mnenguaji mwaka 1984 hadi 1986 na Malage De Lugendo aliyekuwa mwimbaji. 
Wengine walikuwa wanenguaji JoĆ«lle Esso, Tshala Muana mwaka 1978 hadi 1979, Yondo Sister mwaka 1986 na Lambio Lambio ‘Komba Bellow’ mtaalamu wa kupiga kinanda.
Abeti Masikini ni mmoja kati ya wanamuziki wa kike barani Afrika waliofanikiwa kujiwekea jina kimataifa. 
Alidhihirisha uwezo wa kipaji chake na kufahamika nchini Congo ambako muziki umetawalia na wanaume.
Abeti pia alikuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanawake.
Alifariki dunia Septemba 9, 1994 jijini Paris, Ufaransa, takriban miezi miwili kabla ya kutimiza miaka 40.

Comments