Featured Post

UCSAF YATAKIWA KUBORESHA MAWASILIANO VIJIJINI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga, wakati alipotembelea Mfuko huo, jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Ulanga, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, namna Mfuko huo unavyohakikisha mawasiliano ya simu na data unapatikana hususan vijijini, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani), wakati alipowatembelea na kuzungumza nao changamoto na namna ya kufanikisha malengo ya Mfuko huo, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), kuhusu uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini leo, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bw. Salim Msangi akitoa taarifa ya utendaji wa Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wakati alipokuwa akizungumza nao leo, jijini Dar es Salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Serikali imeutaka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), kuona namna ya kuboresha huduma za mawasiliano ya simu na data vijijini ili kuwawezesha wananchi kufikiwa na huduma hiyo kwa urahisi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mfuko huo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani,  amesisitiza kwa Mfuko huo kuhakikisha unafikisha mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo kabisa lengo likiwa ni kufanya usawa na kuwezesha vijiji vyote kufikiwa na huduma hiyo.
"Hakikisheni mnapeleka mawasiliano katika vijiji ambavyo hakuna mawasiliano kabisa kwani wananchi wamekuwa wakilalamika kutofikiwa na huduma", amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Aidha, ameutaka Mfuko huo kuwasimamia watoa huduma nchini kuhakikisha wanafunga minara na mitambo sahihi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Ameutaka Mfuko huo kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha maeneo ambayo watoa huduma wamejenga minara yanakuwa ni ya uhakika.
Ameongeza kuwa Mfuko huo una wajibu wa kutafuta vifaa vingine vitakavyowawezesha kusaidia kufanya ukaguzi kwa haraka badala ya kukaa na kusubiri vifaa vya TCRA.
Ametoa rai kwa makampuni ya simu nchini hususan yanayochangamkia zabuni za Serikali kupitia mfuko huo kutoa taarifa sahihi za usimikaji wa minara na utendaji wake kwa mfuko huo ili kusaidia kuboresha mawasiliano vijijini kwa nia moja.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Eng. Peter Ulanga, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa wataendelea kuwasimamia watoa huduma nchini kuhakikisha wanajenga minara na kuhakikisha inafanya kazi masaa yote.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ngonyani ametembelea Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), na kuwasisitiza kuwajibika katika kuongeza mapato na kuendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini ili kukuza sekta ya usafiri wa anga.

Naibu Waziri ameendelea na ziara yake ya kikazi jijini Dar es Salaam ambapo ametembelea na kuzungumza na uongozi wa UCSAF na TAA.

Comments