Featured Post

TPA WAPEWA MIEZI MITATU UJENZI FLOWMETER

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, alipofanya ziara ya kikazi bandarini hapo, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (katikati), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko. Kulia ni Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Freddy Liundi. 


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, ametoa miezi mitatu kuanzia sasa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha kuwa mkandarasi wa ujenzi wa mita za kupimia mafuta (flow meter), eneo la Kurasini Oil Jetty (KOJ), anapatikana na kuanza kazi mara moja.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri huyo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza mradi huo kumalizika ndani ya mwaka mmoja na ujenzi wa mita hizo kuhusisha bandari za Tanga na Mtwara. 

"Hakikisheni mnaongea lugha inayofanana kati yenu na mtengenezaji ili kuepuka ucheleweshaji wa mradi huu ambao una tija kwa Taifa, pia hakikisheni mnapeleka wataalam nje ya nchi ili kuwajengea uwezo na kuongozea ujuzi na maarifa katika kusaidia kutekeleza mradi huu", amesema Eng. Ngonyani.
Ameongeza kuwa suala la ‘Flow Meter’, ni la ushirikiano kati ya Mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wadau wengine wa mafuta, hivyo kukamilika kwake kutasaidia na kurahisisha ukusanyaji wa mapato yatakayosaidia kukuza uchumi wa nchi. 

Aidha, amefafanua kuwa TPA ikifaulu kuwajengea uwezo wataalamu wake wa ndani, itasaidia usimamizi mzuri wa uingizaji na uhakiki wa viwango vya mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salam, Tanga na Mtwara. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ngonyani ametembelea na kukagua mitambo ya ukaguzi wa mizigo inayoingia bandarini (Scanner) na kuwasisitiza wafanyakazi wa kitengo hicho kuangalia suala la uingizwaji wa mizigo inayopita bandarini hapo kwa mapana zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amemhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kutatua changamoto za Mamlaka hiyo na kutekeleza agizo la ujenzi wa flow meter mara moja. 

Ameongeza kuwa TPA imetoa taarifa kwa Taasisi na Idara zote za Umma ambazo zinaagiza mizigo nje ya nchi kufanya mawasiliano na Mamlaka hiyo mapema kwa mizigo ambayo ni tofauti na ile ya kawaida ili kuongeza udhibiti na usalama wa mizigo hiyo. 

Naibu Waziri Ngonyani amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Makao Makuu ya TPA na Bandari ya Dar es salaam na kujionea maendeleo na changamoto zinazoikabili Mamlaka hiyo. 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI – WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO 

Comments