Featured Post

RAIS WA MISRI AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUPAMBANA NA RUSHWA NA UFISADI


Na Said Ameir – MAELEZO
Agosti 15, 2017 -  Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri amesifu ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na Misri zinazoshughulikia mapambano dhidi ya rushwa na kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano wa uongozi bora unaopambana na maovu katika nchi yake.

“Nampongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa na ufisadi na huo ni mfano wa sifa za uongozi bora” alieleza Rais Al Sisi wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam.

Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri (Administration Control Authority of Egypt) zimekuwa na ushirikiano wa karibu kwa kubalidilishana utaalamu, uzoefu na mbinu katika kutekeleza majukumu yao.

Katika mkutano, huo ambao uliofanyika mara baada ya kumalizika mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo, Rais Al Sisi alieleza dhamira ya nchi yake ni kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuunga mkono jitihada za kuleta amani barani Afrika na kuendelea kuwa na msimamo mmoja katika masuala ya kimataifa.

“Tunampongeza Rais Magufuli na Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kutafuta amani barani Afrika hasa katika eneo la Maziwa Makuu” Rais Al Sisi alisema na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za usuluhishi katika mgogoro wa Burundi.

Rais huyo ambaye alikuwa nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili, ameeleza kutambua mzigo mkubwa inaoubeba Tanzania katika kushughulikia migogoro ikiwa ni pamoja na kuhudumia maelfu ya wakimbizi kutoka katika nchi mbalimbali.

Katika mkutano ambao ulihutubiwa pia na mwenyeji wake Rais Magufuli, Rais huyo wa Misri alieleza utayari wa nchi yake kuendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwa kuhimiza kubuni na kutekeleza miradi ya pamoja, kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kubadilishana wataalamu.

”Misri na Tanzania hatma yao ni moja,  tutaendelea kushirikiana kwa hali na mali na kwa kuwa tuna dhamira, matumaini yetu makubwa ni kufanikiwa” Rais Sisi alisisitiza.

Kabla ya mkutano huo na wanahabari, Rais wa Misri alikuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais Magufuli na baadae kuhudhuria mazungumzo rasmi ya mashauriano kati ya Tanzania na Misri.

Comments