Featured Post

RAIS AMFUKUZA KAZI WAZIRI MKUU BAADA YA KUKAA MIEZI MITATU OFISINI

Picha ya faili ya Abdelmadjid Tebboune. Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amemtimua Tebboune Agosti 15, 2017, chini ya miezi mitatu tangu alipomteua. PICHA YA AFP| RYAD KRAMDI 

Na AFP
ALGIERS
RAIS wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, amemtimua Waziri Mkuu Abdelmadjid Tebboune juzi Jumanne, ikiwa ni chini ya miezi mitatu tangu alipomteua, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.
"Rais Abdelaziz Bouteflika siku ya Jumanne amemvvua madaraka Waziri Mkuu Abdelmadjid Tebboune na kumteua Ahmed Ouyahia", Mnikulu wa Algeria alisema.
Chama anachotoka Bouteflika cha National Liberation Front (FLN) na Rally for National Democracy (RND) kinachongozwa na Ouyahia kwa pamoja vina wabunge wengi baada ya kushinda katika uchaguzi wa marudio Mei 4.
Katika hali ya kushangaza, wiki tatu baada ya uchaguzi, rais alimteua Tebboune, ambaye alikuwa Waziri wa Nyumba na Makazi, kuwa Waziri Mkuu kuchukua nafasi ya mshirika wa Bouteflika, Abdelmalek Sellal.
MATATIZO
Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya serikali ambacho kiliongea na AFP kwa masharti ya kutotajwa jina, Tebboune mwenye umri wa miaka 71 amefukuzwa kazi kwa sababu "mtazamo wake haukuendana na wa rais".
Chanzo hicho kimeeleza pia kwamba kulikuwa na matatizo ya mawasiliano baina yao. Kutimuliwa huko kumekuja siku chache baada ya ripoti kwamba Bouteflika alikuwa ametuma barua kali kwa waziri mkuu, akimtaka arekebishe sera zake na kupinga kuzuia uingizaji wa bidhaa nchini humo.
Lakini mchambuzi wa masuala ya siasa Rachid Tlemcani alisema Tebboune alikuwa akitafuta namna ya kuwabana "baadhi ya watu walio katika kambi ya rais" na amekuwa muhanga wa vita ya madaraka.
Mchambuzi mwingine Rachid Grim alisema "Tebboune alifanya kosa kwa kudhani kwamba alikuwa analindwa" na Bouteflika,  hali inayoashiria kwamba baadhi ya wenye maamuzi wanaweza kuwa wameingilia kati nyuma ya pazia.
Wakosoaji wamekuwa wakihoji uwezo wa Bouteflika kuongoza tangu alipopata kiharusi mwaka 2013, lakini duru za rais zinasema kiongozi huyo amesema anao uwezo mkubwa wa kuongoza.
KUKOSA SHUKRANI
Mrithi wa Tebboune, Ouyahia mwenye umri wa miaka 65, amekuwa mtu maarufu katika siasa za Algeria katika miongo miwili na amekuwa akimtumikia rais kwa bidii licha ya kuyumba kwa uhusiano wakati fulani.
Waalgeria wamembatiza jina la utani "Mr Dirty Work", baada ya kusema amepewa kazi isiyo na shukrani ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyoagizwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) wakati wa muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Nchi hiyo kutoka Afrika ya Kaskazini wakati wa machafuko ya mwaka 2011 (2011 Arab Spring uprisings) ilitumia fedha nyingi na ruzuku ambazo zilikwangua akiba ya serikali.
Lakini kushuka kwa bei ya mafuta ghafi mwaka 2014 kuliilazimu serikali kuongeza kodi na kusitisha miradi mingi.
Leo hii, kati nchi yenye wakazi milioni 40 na nusu yao wakiwa chini ya miaka 30, kijana mmoja kati ya watatu hana ajira.
Uchaguzi wa Mei 4 ulitawaliwa na uhaba wa wapiga kura pamoja na kwamba wengi wanasema ahadi za serikali zimevunjika na mfumo wa siasa umetawaliwa na rushwa na ufisadi.

Comments