Featured Post

NAIBU WAZIRI AWAASA UONGOZI WA SHIRIKA LA POSTA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akifafanua jambo wakati akizungumza na uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), alipotembelea makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Bw. Macrice Mbodo.

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Bw. Macrice Mbodo (kulia), akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo, jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (hayupo pichani), wakati alipozungumza nao kuhusu changamoto zinazowakabili, jijini Dar es Salaam .
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Mgwatu akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, namna huduma za vivuko zinavyotolewa kati ya Magogoni na kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Mtaalam wa mifumo ya TEHAMA, Peter Mungo, akimwonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani namna mfumo huo unavyofanya kazi, wakati alipofanya ukaguzi eneo la Magogoni kujionea utendaji kazi wa Vivuko vinavyotoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (mwenye suti), pamoja na abiria wengine wakishuka kutoka kwenye kivuko cha MV. Kazi kinachotoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni, wakati alipokagua kivuko hicho, jijini Dar es salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Seriklaini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Shirika la Posta Tanzania (TPC), limetakiwa kuangalia na kuona namna ya kuboresha mishahara ambayo itatoa motisha kwa watumishi wake ili kufanikisha kutekeleza majukumu yao na hatimae shirika kujiendesha kwa faida na kutoa gawio kwa Serikali.
Akizungumza na uongozi pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amesisitiza kuwa ipo haja kwa uongozi wa shirika hilo kurekebisha mishahara ya watumishi wake kulingana na mazingira ya sasa.
"Angalieni namna ya kuboresha viwango vya mshahara angalau vikidhi matakwa ya wafanyakazi hawa ambao wana hali mbaya ili nao waweze kujikimu kama watumishi wengine”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Eng. Ngonyani, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, ujuzi na ufanisi ili kuongeza uzalishaji wa shirika hilo na hatimae kukuza pato la Taifa.
Aidha, ameutaka uongozi wa shirika hilo kuongeza na kupanua wigo wa kufikisha huduma za posta kwa wateja wake hususan katika mikoa ya nyanda za juu kusini na mikoa ya Kanda ya Ziwa kwani huduma hizo katika mikoa hiyo zimekuwa zikisuasua.
Naye, Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo, amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa ujio wake katika shirika hilo na kumuahidi kutekeleza maagizo yote ili kuleta tija kwa shirika na kukuza pato la Taifa.
Ameongeza kuwa Shirika liko kwenye hatua za mwisho za kuwekeana mikataba ya kibiashara na taasisi za Serikali kama vile MSD, NIDA, TBS na nyinginezo ili kuhakikisha inafikia wateja wote mahali popote nchini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ametembelea Ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), pamoja na kukagua shughuli zinazoendelea katika karakana ya Magari ya Serikali (M.T. Depot) iliyopo eneo la Kurasini na kusisitiza kuongeza wataalam wa ufundi hususan mafundi mchundo na mafundi sanifu ili kutatua changamoto zinazokabili karakana za Wakala huo mikoani.
Ameitaka TEMESA kuboresha miundombinu ya vivuko katika visiwa vya Ukerewe na Ukara vilivyopo mkoani Mwanza, ambapo changamoto za uharibifu na uchakavu wa vivuko hivyo umekuwa ukiripotiwa mara kwa mara.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu, amebainisha baadhi ya miradi ambayo inatarajiwa kutekelezwa na wakala wake kwa mwaka wa fedha 2017-2018 ikiwemo ununuzi wa kivuko kipya cha Kigongo - Busisi na ukarabati mkubwa wa vivuko vya MV. Sengerema, MV. Misungwi, MV. Kigamboni na Boti ya MV. Kiu ambapo lengo likiwa ni kuongeza na kurahisisha huduma za usafiri kwa watumiaji.

Naibu Waziri Ngonyani anaendelea na ziara ya kikazi jijini Dar es salaam ambapo jana ametembelea na kukagua utoaji huduma katika Shirika la Posta nchini na Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA).

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Comments