Featured Post

MAREKANI YAIMWAGIA TANZANIA BILIONI 550 KUSAIDIA MAENDELEO

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Inmi Patterson (kulia) akizungumza jambo wakati wa Mkutano kati yake na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (Hayupo pichani) kuhusu msaada wa Sh. bilioni 550, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) hapa nchini, Andy Karas (katikati) na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Dkt. Inmi Patterson wakisikiliza maelezo ya wajumbe (hawapo pichani) waliohudhuria hafla ya kusainiwa kwa msaada wa Dola milioni 225 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) nchini, Bw. Andy Karas (katikati) wakisaini mkataba wa msaada wa Dola milioni 225 kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Misaada la nchi hiyo (USAID), Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) hapa nchini, Bw. Andy Karas, wakibadilishana mkataba wa msaada wa Sh. bilioni 550, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) hapa nchini, Bw. Andy Karas (kushoto), akizungumzia ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani wakati wa hafla ya kusainiwa kwa makubaliano ya ruzuku ya Dola milioni 225 kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika la msaada la nchi hiyo (USAID), Jijini Dar es Salaam, kulia ni Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Inmi Patterson.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (wa pili kushoto), Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Inmi Patterson (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) Tanzania, Bw. Andy Karas (kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (kushoto) na wajumbe wengine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusainiwa kwa mkataba wa msaada wa Sh. bilioni 550 kutoka Serikali ya Marekani,  katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

0645
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto) akiagana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Inmi Patterson baada ya kusainiwa kwa mkataba wa ruzuku ya Sh. bilioni 550 kutoka Serikali ya Marekani,  katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Serikali ya Marekani imetiliana saini na Tanzania makubaliano ya kuipatia ruzuku ya Dola za Marekani milioni 225 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 550 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii katika sekta za afya, elimu ya msingi, kilimo, maji na usafi wa mazingira.

Tukio hilo limefanyika Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania imewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kwa upande wa Serikali ya Marekani, makubaliano hayo yametiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Bw. Andy Karas

Utiwaji saini wa makubaliano hayo umefanyika siku moja baada ya Marekani kupitia Kaimu Balozi wake hapa nchini, Dkt. Inmi Patterson kukutana na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa Serikali yake iko tayari kuongeza misaada kwa Tanzania.

Maeneo ambayo fedha hizo zitatumika na kiwango chake kwenye mabano ni mapambano dhidi ya Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (Dola milioni 98.2), Malaria (Dola milioni 46), Kifua Kikuu (Dola milioni 5), Uzazi wa Mpango (Dola milioni 26.4), Sekta ya Kilimo (Dola milioni 45), Maji na Usafi wa Mazingira (Dola milioni 9) na Elimu ya msingi (Dola milioni 13.9)

Akizungumza wakati wa tukio hilo lililohudhuriwa pia na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Inmi Patterson, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, ameishukuru Marekani kwa msaada huo unaolenga kusadia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi wake.

“Marekani ni rafiki yetu na mdau wetu mkubwa wa maendeleo wa siku nyingi na ninachowaahidi ni kwamba tutatupa jicho kali kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika kama ilivyokusudiwa na jinsi tulivyokubaliana” Alisisitiza Bw. James.

Nae Bw. Andy Karas amesema Serikali na watu wa Marekani kwa ujumla wanafurahishwa na hatua kubwa ya kimaendeleo iliyopigwa na Tanzania na kuahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano huo kwa faida ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Dkt. Inmi Patterson, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo.

Comments