AFRIKA MASHARIKI INA AKIBA YA FUTI TRILIONI 156 ZA GESI ASILIA ZILIZOTHIBITISHWA

Picha inayoonyesha mahali mafuta yanakochimbwa katika Ziwa Albert nchini Uganda.
Kisima cha Mafuta kinachomilikiwa na kampuni ya Tullow nchini Uganda.

AFRIKA Mashariki inakadiriwa kuwa na kiasi cha mapipa bilioni 7.2 ya akiba ya mafuta iliyothibitishwa na futi za ujazo trilioni 156 (trillion cubic feet – Tcf) za akiba iliyothibitishwa ya gesi asilia, MaendeleoVijijini inaripoti.

Kiwango cha mafuta kilichopo ni kile ambacho tayari kimekwishagunduliwa nchini Uganda, ambako serikali ya nchi hiyo imekwishaanza ujenzi wa bomba la mafuta hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, ambapo uzinduzi wake ulifanyika hivi karibuni.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, katika upande wa gesi asilia, kiwango cha futi za ujazo trilioni 156 kinachotajwa kinahusisha nchi za Tanzania yenye akiba ya futi za ujazo trilioni 56 na Msumbiji ambayo ina akiba iliyothibitishwa ya futi za ujazo trilioni 100, ambazo tayari zimekwishaanza uzalishaji huku utafiti zaidi ukiendelea.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, mwaka 2015 Tanzania ilishika nafasi ya 10 barani Afrika na ya 66 duniani kwa uzalishaji wa gesi, wakati Msumbiji ilishika nafasi ya sita Afrika na ya 54 duniani.
Msumbiji imehusishwa ndani ya Afrika Mashariki kutokana na ukweli kwamba hata gesi iliyopatikana ipo katika Bonde la Ruvuma, eneo ambalo ni la mpaka baina yake na Tanzania, ambayo pia imefanya ugunduzi mkubwa kwenye bonde hilo.
Takwimu hizo zinaonyesha kwamba, akiba ya mafuta iliyopo Afrika Mashariki ni sawa na asilimia sita ya mafuta yaliyothibitishwa Afrika na wakati gesi asilia ni asilimia 2.19 ya gesi iliyothibitishwa barani humo.
Taarifa ambazo MaendeleoVijijini inazo zinaonyesha kwamba, ugunduzi wa mafuta nchini Uganda na gesi asilia katika Tanzania na Msumbiji umeendelea kuvutia wawekezaji katika eneo hili tangu mwaka 2006 huku Msumbiji ikitajwa kwamba inaweza kuwa nchi ya kwanza katika Afrika ya Mashariki kuanza kusafirisha nje ya nchi gesi asilia iliyosindikwa katika mfumo wa kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG).
Taasisi ya Habari za Nishati duniani (EIA) inaripoti kwamba, historia ya uwekezaji katika gesi asili nchini Kenya inalingana na ile ya Uganda, Tanzania, Madagascar na Msumbiji ambako shughuli za utafiti katika eneo hilo zilianza zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Ingawa utafiti wa kwanza ulifanyika katika nchi za Uganda na Madagascar mwanzoni mwa karne ya 20, lakini umesubiri kwa miaka mingi hadi hivi karibuni ambapo yameonekana mafanikio madogo huku baadhi ya wawekezaji wakikatishwa tamaa na uwepo wa mizozo ya ndani na kukosekana kwa uimara wa kiutawala kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, hali hiyo imebadilika kwa sasa, hasa baada ya kugundulika kwa kiasi kikubwa cha mafuta nchini Uganda mwaka 2006 pamoja na ugunduzi na uchimbaji wa gesi asilia unaoendelea Msumbiji na Tanzania.
Kwa mujibu wa maelezo ya mkuu wa kampuni moja ya mafuta yaliyochapishwa katika Mwongozo wa Mafuta na Gesi Afrika Mashariki wa Deloitte, haidrokaboni zaidi zimegunduliwa ndani ya Afrika ya Mashariki katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, hadi Januari 2013, kampuni za kigeni zinazoongoza kwa uwekezaji Afrika Mashariki ni pamoja na Anadarko na Eni zilizoko nchini Msumbiji upande wa kaskazini katika Bonde la Ruvuma, Oil Madagascar iko nchini Madascar, Tullow inafanya tafiti mbalimbali nchini Kenya lakini pia kampuni hiyo iko Uganda pamoja na kampuni za Total na CNOOC.
Maeneo yaliyogundulika kuwa na akiba ya mafuta.

Nchini Tanzania, japokuwa kuna kampuni nyingi, lakini ambazo tayari zimekwishaanza na uchimbaji katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo upande wa Pwani na kwenye Bahari ya Kina Kirefu ni BG Group, Statoil, Ophir Energy, ExxonMobil na Aminex.
Kutokana na kugundulika kwa rasilimali za mafuta na gesi asilia Afrika Mashariki, kampuni zinazomilikiwa na serikali za nchi za Asia nazo zimejipenyeza katika ushindani kwenye akiba za nishati katika eneo hilo huku zikipata nguvu katika miradi ya kusafirisha nje, shughuli ambazo zamani zilikuwa zikishikiliwa zaidi na kampuni za Ulaya Magharibi kama Shell na nyinginezo.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesha kwamba, hivi sasa wawekezaji kutoka Asia wanaokuja juu katika sekta ya mafuta na gesi ndani ya Afrika Mashariki ni CNOOC ya China, ambayo inaendesha utafiti na maendeleo ya mafuta nchini Uganda, wakati kampuni nyingine kutoka China, CNPC, iliyonunua hisa za dola za Marekani bilioni 4.2 kutoka kampuni ya Eni kuendesha shughuli za uchimbaji katika pwani ya Ruvuma nchini Msumbiji, sasa iko katika hatua za mwisho za kujenga mtambo wa kusindika gesia ya asilia katika hali ya kimiminika (LNG plant), shughuli ambazo zilianza Machi 2013.
Wawekezaji wengine wakuu wa Asia ni pamoja na Shirika la Mafuta Ghafi la Bharat la India, na kitengo cha Viwanda vya Videocon vya India, ambao kwa pamoja wanamiliki asilimia 10 ya eneo la Msumbiji (1 Block).
Aidha, Kampuni ya Gesi ya Osaka na Kampuni ya Nguvu za Umeme ya Tokyo (TEPCO) zimekuwa na mazungumzo na Anadarko na washirika wake tangu mwaka 2012 kuhusu mauzo ya baadaye ya gesi ya asilia iliyoweka katika hali ya kiminika nchini Msumbiji.
Lakini pia nchi za Afrika Mashariki zenyewe zinatafuta wawekezaji kutoka Asia. Mnamo Agosi 2013, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipanga safari ya siku nane Urusi na China kuvutia uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi nchini Kenya.
Wataalamu wa masuala ya uchimbaji wanasema ukaribu wa masoko ya Asia, usalama wake kisiasa ikilinganishwa na wasafirishaji nje wakubwa kutoka Mashariki ya Kati, pamoja na kukua kwa mahitaji ya nishati, ndizo sababu za kukua kwa mvuto huo wa uwekezaji Afrika Mashariki.
Ripoti ya Dunia kuhusu Gesi Asilia ya Kimiminika (World LNG Report) ya mwaka 2011 inasema kwamba, Japani na Korea ya Kusini zinaingiza kutoka nje karibu asilimia 50 ya gesi asilia ya kimiminika katika mahitaji ya gesi hiyo tu duniani, na kwamba India ni muagizaji mkuu wa sita duniani wa gesi hiyo, nyuma kidogo ya China.
Inaelezwa pia kwamba, tangu mwaka 2012, nchi za Indonesia na Malaysia zinaagiza kutoka nje gesi ya asilia ya kimiminika na Singapore na Israeli zinasemekana kujenga vifaa vya kurudisha upya gesi na hivyo zinajiandaa kuagiza gesi asilia ya kimiminika.
Kutokana na ukaribu wa masoko hayo, blog ya The Next Oil Rush inakadiria kwamba inachukua siku 19 kusafirisha mafuta kutoka Lamu nchini Kenya hadi Shanghai, China ikilinganishwa na siku 27 kutoka Soyo, Angola hadi Shanghai na karibu siku 17 kutoka Saudi Arabia au Iran hadi Shanghai.

Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, kugundulika kwa kiwango kikubwa cha gesi asilia nchini Tanzania kulichochea kuanzishwa kwa Kongamano na Maonyesho ya Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (TOGaCE) ambalo linawakusanya wadau wa sekta ya mafuta na gesi nchini humo.
Lengo kubwa la kongamano hilo lililofanyika mwaka 2012 lilikuwa kukuza ufahamu na uelewa wa umuhimu wa maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania, kutoa nafasi kwa taasisi za ndani kujitangaza, kujadili sera, sheria na mwongozo mzima wa sekta hiyo na kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kuwekeza nchini.  Kongamano pia linatoa nafasi kwa kampuni na watu binafsi kutangaza bidhaa na huduma zao.
Kongamano la kwanza kabisa lilifanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 18 mpaka 19, 2012 ambalo liliandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET).
Lengo kuu la kongamano hilo la kwanza lilikuwa kujenga uelewa wa dhana nzima ya mafuta na gesi miongoni mwa washiriki wa Tanzania lakini pia kuangalia mchango wa sekta ya mafuta na gesi katika kuchochea viwanda na maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku washiriki walijadili njia mbalimbali za kukuza sekta husika.
Mambo matano yaliwasilishwa kwenye kongamano hilo, ambayo ni: Sera na Sheria zinazohusika na gesi asilia; Masuala ya teknolojia yanayohusiana na utafutaji, tathmini ya visima, uchimbaji, usafirishaji, uchakataji na matumizi ya gesi asilia; Kujenga uwezo kwa wazawa kushiriki katika sekta hii ikiwemo masuala ya maendeleo ya miundombinu, mafunzo na tafiti; Masuala ya usalama, uharibifu wa mazingira na namna ya kusimamia na kulinda mazingira; na Kukuza uelewa kuhusu sekta ya gesi, umuhimu wake na fursa zilizopo.
Kumbukumbu ambazo MaendeleoVijijini inazo zinaonyesha kwamba, changamoto za sekta hiyo zilibainishwa na washiriki wa kongamano zikijumuisha, pamoja na masuala mengine, kuongeza idadi ya wataalamu kwenye sekta ya mafuta na gesi, kuendeleza miundombinu na kuwekeza kwenye nishati endelevu. Washiriki walikubaliana kuanzishwa kwa mfuko wa mafuta na gesi kama ilivyo nchini Norway na kutafuta suluhisho za ndani katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hii. Maazimio ya kongamano yalitengenezewa mpango mkakati wake.
Kongamano la pili lilifanyika pia Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Oktoba 23 – 24, 2013 na liliandaliwa kwa pamoja na Idara ya Uhandisi Kemikali na Madini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Wizara ya Nishati na Madini, TPDC na EWURA. 
Kongamano lilikutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, sekta binafsi ikijumuisha kampuni za mafuta na gesi na wanataaluma ambao walijadili masuala mbalimbali yanayohusu sera, hali halisi ya sekta hususan masuala yanayohusu mkondo wa juu (upper stream), mkondo wa kati (midstream) na mkondo wa chini (downstream).
Mkondo wa juu ndio unaohusika na utafiti na uchimbaji, mkondo wa kati unahusika na uchakataji na miundombinu ya usafirishaji, wakati mkondo wa chini unahusika na usambazaji tayari kwa matumizi.
Masuala kadhaa yalijadiliwa ambayo ni pamoja na Ufanyaji wa biashara, kodi na masuala ya fedha; Uendelezaji na ufaidikaji wa rasilimali za mafuta na gesi; Utafutaji endelevu na matumizi ya mafuta na gesi; Kujenga uwezo kwa wazawa; na Changamoto na mustakbali wa sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, sehemu kubwa ya majadiliano ilitazama namna gani Watanzania wanaweza kushiriki katika ngazi zote za mlolongo wa thamani wa sekta hiyo na kupendekeza kuwepo kwa mwongozo wa kuhakikisha sekta binafsi inasaidiwa kushiriki katika sekta hiyo, ukilenga hasa uhamishaji wa maarifa na teknolojia kutoka nje ya nchi kwa manufaa ya wazawa.
Oktoba 21-22, 2014 kongamano la tatu lilifanyika Dar es Salaam ambalo liliandaliwa na taasisi zile zile zilizoandaa kongamano la pili, ambapo kwa mara ya kwanza kongamano hilo liliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili, lengo likiwa kuwapatia nafasi Watanzania wasioweza kutumia lugha ya Kiingereza kushiriki kwenye mijadala mbalimbali.
Katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo, Stephen Masele, aliahidi kutungwa kwa Sera ya Ushirikishaji na Uwezeshaji Wazawa Tanzania ambayo itahakikisha Watanzania wanashiriki katika mlolongo mzima wa thamani na kufaidika na sekta ya gesi na mafuta.
Lakini mwaka huo pia, mnamo Novemba 14-15, lilifanyika kongamano jingine mjini Mtwara, maarufu kama Kongamano la Mafuta na Gesi Mtwara (MOGBE), ambalo lilikuwa la kwanza na la aina yake kuhusiana na sekta ya mafuta na gesi. Lengo kubwa lilikuwa kulifanya liwe kiunganishi miongoni mwa wadau kwenye mlolongo wa thamani nchini humo kwa kuwawezesha, kuwapatia fursa za ajira na kujenga uwezo miongoni mwa wanajamii wa maeneo ya Kusini mwa Tanzania.
Kongamano la Nne linalohusu sekta ndogo ya mafuta na gesi lilifanyika kuanzia tarehe 20 – 21 Oktoba, 2016 jijini Dar es Salaam na kukutanisha wadau mbalimbali zikiwemo kampuni zinazojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, Vyuo Vikuu, Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Kutokana na uwekezaji katika shughuli za gesi na mafuta, kumekuwepo na mabadiliko ya kiuchumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara kama vile kuongezeka kwa fursa za ajira, malazi na utoaji wa huduma kwa wawekezaji.

Hali hiyo inawapa fursa wananchi kujiona kama nao ni sehemu ya maamuzi lakini ni wanufaika wa rasilimali hizo asilia ambazo zinachimbwa katika maeneo yao badala ya kujiona kana kwamba wametengwa.