Featured Post

WATAALAMU WA KILIMO BUKOMBE WATAKIWA KUWA NA KUMBUKUMBU ZA KILIMO ZA KATA ZAO.




Na: Calvin Edward Gwabara

Bukombe - Geita


Wataalamu wa kilimo kwenye kata na vijiji vyote vya wilaya ya Bukombe wametakiwa kuwa na kumbukumbu sahihi za wakulima,mazao,mifugo na uzalishaji wa mazao kwenye maeneo yao ili kuwezesha kutumia takwimu hiyo kwenye shughul mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo kwenye maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ya Bukombe Mhe. Joseph Maganga wakati akizungumza na wataalamu hao wa kilimo kwenye mafunzo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Bukombe Mhe. Joseph Maganga wakati akizungumza na wataalamu hao wa kilimo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo kwenye kilimo cha mazao ya Mihogo,Pambana Viazi lishe yaliyoandaliwa na Tume ya taifa ya sayansi na teknolojia COSTECH kupitia Jukwaa la Bioteknolojia OFAB.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bukombe amesema kuwa wataalamu hao wengi hawana kumbukumbu zinazohusu kilimo na ufugaji kwenye maeneo yao hivyo inapotokea taarifa hizo zikahitajika kwenye kuandaa mipango mbalimbali ya kuwezesha sekta hiyo kwenye maeneo yao ndipo huanza kuhangaika kuzitafuta na wengine hubuni hali ambayo inachelewesha na kuharibu mipango ya wilaya na wadau wa kilimo.
Wataalamu hao wa kilimo wilaya ya Bukombe  wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.

Amewataka kila mtaalamu wa kilimo kuwa na taarifa zote za kilimo na idadi ya wakulima na wafugaji na aina ya ghughuli ya kilimo wanayoifanya kila wanapokwenda kuwatembelea na kuwasaidia shughuli mbalimbali za ugani.
Mhe. Maganga ameishukuru COSTECH kwa kupeleka mafunzo hayo kwenye wilaya yake kwani anaamini yatasaidia sana kuwarudisha maafisa ugani hao kwenye mstari kama ambavyo walivyokuwa wakati wanatoka vyuoni maana wanapofika kwenye maeneo ya kazi huanza kufanya kazi kwa mazoea kutokana na kubadirishwa na mazingira wanayoyakuta.
Wataalamu hao wa kilimo wakipokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo

Amewataka wataalamu hao wa kilimo kutatua changamoto zingine za kilimo kwenye kata zao ikiwemo zile za kimasoko hususani madalali ambao wanawanyonya wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo na wao kuyauza kwa bei kubwa hali ambayo inashusha ari ya wakulima kuendelea kuzalisha.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Baraka Hussen Maganga amewataka wataalamu hao wa kilimo kwenda kuitumia elimu waliyoipa kuleta mabadiriko kwenye kilimo kwa wakulima wa wilaya hiyo kwa kuwapa mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija.
Muwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukombe Mhe.  Baraka Hussen Maganga

Amesema halamshauri yake itaendelea kushirikiana na kuwafuatilia kwa makini utekelezaji wa kazi zao hususani mbinu hizo wanazopewa ili zisiishie kwenye mabrasha na ukumbi wa mafunzo hayo badala yake zifike kwenye maeneo yao ya utawala kama walivyopewa.

Kwa upande wake muwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa tume ya taifa ya sayansi na teknolojia COSTECH Bi. Bestina Daniel amesema mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa kazi za COSTECH za kuwawezesha wakulima na wadgani katika kutumia mbinu na teknolojia bora za kilimo kwenye uzalishaji ili kuongeza tija na kupunguza umasikini kwenye kaya.
Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia( COSTECH) Bi. Bestina Daniel akitoa Salamu za Tume na malengo ya mafunzo hayo kwa mgeni rasmi na washiriki wa mafunzo.

Amesema COSTECH ndio wenye dhamani ya kuishauri Serikali kwenye masuala yote yanayohusu Sayansi na Teknolojia hivyo pale kunapotokea teknolojia na mbinu nzuri ambazo zinaweza kuleta mageuzi kwenye uzalishaji kwa wakulima hutafuta mbinu mbalimbali za kuzifikisha kwa wahusiaka.


Bestina amesema ili kufikia kwenye uchumi wa viwanda lazima malighafi za kutosha ziwepo ili kulisha viwanda hivyo na kuzalisha bidhaa hivyo mazao hayo ambayo COSTECH inayahamasisha yatasaidia sana katika kulisha viwanda vya nguo,usindikaji wa mihogo na viazi lishe ambavyo vina umuhimu mkubwa kwenye kuongeza lishe na usalama wa chakula.


Mafunzo hayo ya siku moja kwa maafisa ugani hao yanalenga kuwapatia mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya Mihogo,Viazi lishe pamoja na Pamba na nafasi ya matumizi bioteknolojia kwenye kuongeza uzalishaji na kutatua changamoto za kilimo kama magonjwa,wadudu na matatizo ya mabadirliko ya tabia nchi.
Picha ya Pamoja ya Baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo.

Comments