Featured Post

MGEJA: VIONGOZI WANAOFANYA UBAGUZI WA KIITIKADI ZA KISIASA WAKEMEWE

Khamis Mgeja
Na Hastin Liumba,DodomaMWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation (Taasisi inayoshughulikia utawala bora na haki za binadamu) Khamis Mgeja amewataka viongozi mbalimbali waliokabidhiwa dhamana na wananchi wa Tanzania walinde haki na uhuru wa mtanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Mgeja aliyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Dodoma akilaani na kukemea kuhusiana na kauli za baadhi ya viongozi hivi karibuni.
Alisema hivi sasa imezuka kasumba mbaya sana nchini kwa baadhi ya viongozi hivi karibuni ya kutishia kutowapelekea miradi ya maendeleo wananchi waliochagua upinzani katika majimbo yao na kata zao na miradi inaenda kwa kusuasua ni kama funika kombe.
Mgeja aliwataka viongozi watambue wananchi walioamua kuchagua upinzani katika uchaguzi mkuu 2015 walitumia haki zao za kikatiba wala hawakufanya kosa lolote la kuvunja katiba na wala kosa la kisheria na jinai ila wananchi wanapaswa kuheshimiwa na watanzania wako huru ndani ya nchi yao.
Mgeja alisema amesikitishwa na kauli za hivi karibuni za viongozi wa kitaifa kuwa waliochagua upinzani watakoma ni kauli za kutowatendea haki wananchi wa maeneo waliochagua upinzani na ni sawa na kuwanyanyapaa.
Aidha kuhusu kauli za kibaguzi Mgeja amewaomba wananchi hao na wapenda demokrasia ni lazima kauli hizo za kibaguzi zikemewe,kupuuzwa na kulaaniwa bila kujali sura ya mtu wala nyadhifa zake.
Mgeja amewaomba watanzania waliochagua upinzani wasikatishwe tamaa na vikwazo vyovyote hivi sasa vinavyoendelea vya kusuasua kimaendeleo katika maeneo yao na ukandamizaji mkubwa wa demokrasia nchini.
Mwenyekiti huyo ameendelea na kuwaomba watanzania watambue safari yoyote ya mafanikio na hata dhamira yao kutaka mabadiliko ya kweli kuwa hayaji kirahisi na huambatana na kejeli,chuki,dhuluma,manyanyaso na misukosuko mbalimbali ikiwemo baba lao kamatakamta, nawaomba wasikate tamaa iko siku haki itasimama.
Mgeja amewataka na kuwaomba viongozi waliopewa dhamana watambue Watanzania wote wako sawa na wanalipa kodi mbalimbali za kuchangia maendeleo nchini na hata misaada ya maendeleo inayotoka nje inakuja kwa watanzania wote na haisemi kwa ajili ya chama fulani.
Alisema ni vyema sasa viongozi wa dini na wapenda haki, demokrasia na usawa kwa heshima na taadhima washikamane nao waungane  kukemea na kulaani tabia hiyo.
Aidha aliwaomba kumekea na kulaani tabia hii ya ubaguzi,vitisho na kuwafanya watanzania waishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao kutokana na upandikizwaji wa chuki.
Mgeja alisema nchi zote zilizoendelea duniani ziliheshimu watu wake na kuwapa hadhi kama raia wa nchi zao na kudumisha demokrasia bora siyo ya magumashi kama ilivyo baadhi ya nchi nyingi za kiafrika na Tanzania ni mojawapo .

Comments