BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB) KUFADHILI MRADI WA RELI YA KATI KIWANGO CHA KIMATAIFA

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (aliyenyoosha mikono) akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Benki yake.
(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kushirikiana na Tanzania kujenga mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kuipatia mkopo wenye masharti nafuu.

Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.

Dkt. Weggoro amesema kuwa Benki yake imeridhika na utendajikazi wa Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na hivyo kuifanya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo kukubali kufanikisha ujenzi wa Reli hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Amesema kuwa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa ni muhimu kwa uchumi wa Taifa lakini pia kwa uchumi wa nchi za Maziwa Makuu kwa kuunganisha nchi kama vile Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na baadae itaunganishwa na Reli ya Kaskazini upande wa Kenya.

“Benki iko tayari na inasubiri Tanzania ilete mapendekezo ama maombi ili yafanyiwekazi, tutakaa pamoja ili tuone Benki itasaidia kiasi gani na Benki pia inaweza kuwatafuta wadau wengine tunaosaidiana nao katika miradi mikubwa kama hii” Aliongeza Dkt. Weggoro

Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (Standard gauge), yenye urefu wa kilometa 2,561 umepangwa kugharimu kiasi cha Dola bilioni 7.6 za Marekani, sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16,awamu ya kwanza imeanza kujengwa kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na baadae awamu nyingine zitafuata.

Aidha, Dkt. Weggoro amesema Benki yake itashirikiana na Serikali kuboresha utendajikazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hasa upande wa muundo wake na madeni makubwa yanayolikabili shirika hilo ili liweze kuchangia ipasavyo ukuaji wa uchumi wa viwanda.

“Benki itatoa fedha ili kulifanya shirika hilo lifanyekazi kwa ufanisi zaidi, tunajadiliana na tutawashirikisha pia wadau wengine zaidi ili uamuzi wa Serikali wa kuifanya nchi iwe ya viwanda uweze kufanikiwa” Alifafanua Dkt. Weggoro

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kujaji, ameishukuru AfDB kwakuwa mshirika mkubwa wa kimkakati wa maendeleo kwa kusaidia miradi mbalimbali ikiwemo barabara, nishati ya umeme, kilimo na huduma za jamii.

Dkt. Kijaji amesema kuwa uwekezaji wa AfDB hapa nchini umefikia Dola bilioni 1.8 huku asilimia 74.5 za uwekezaji huo iko kwenye sekta ya miundombinu, ambapo barabara imechukua asilimia 51.4, Nishati (10.1%), Maji na Usafi wa Mazingira (13%) na Sekta nyingine za huduma za jamii, kilimo na masuala ya fedha (25.5%).

Amesema kuwa uamuzi wa Benki hiyo kuamua kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) pamoja na kuihuisha TANESCO ni hatua muhimu itakayochochea ukuaji haraka wa uchumi wa nchi.

Ameitaja miradi mingine ya kimkakati iliyotekelezwa kupitia msaada na mkopo nafuu kutoka Benki hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami inayoanzia Afrika Kusini-Cairo-Misri-Tanzania, kuanzia mkoani Iringa, Dodoma hadi Babati mkoani Manyara, inayotarajiwa kukamilika katika kipindi cha takriban miezi miwili ijayo.