SONONA (DEPRESSION) HAIKUBALIKI, MAZUNGUMZO NI DAWA YA KUITOKOMEZA
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO
Miongoni mwa vitu vinavyomhangaisha mwanadamu ni dhoruba za kimaisha, ameumbwa akiwa amekamilika kwa afya ya mwili, inapotokea afya yake haipo sawasawa, hali hiyo hujulikana kama anaumwa au mgonjwa.
Ugonjwa humfanya mtu ashindwe kutimiza majukumu yake ya kila siku kiufasaha katika jamii na taifa bila kujali umri, jinsia, kabila au rangi, awe mtoto, kijana, mtu mzima au mzee.

Mfumo wa maisha ya watu umekuwa chanzo cha magojwa yanayomsumbua mwanadamu, sonona imekuwa tishio kwa maisha na humpata mtu kutokana na maisha yasio na mpangilio yakiambatana na kujihisi huzuni.
Hali hii inaweza kuchukuwa wiki mbili au zaidi kama haitadhibitiwa na kupelekea mtu kutotamani kuendelea kuishi, upweke, kukosa tumaini na kuathiri utendaji wake wa kazi wa kila siku.
Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo Tanzania ni mwanachama, limetenga Siku ya Afya Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Aprili 7, mwaka huu siku hii imetengwa kwa ajili ya kuwapa watu uelewa na kutambua juu ya hali ya sonona ili jamii zote duniani wahamasike na kujikinga na hali hiyo waweze kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.
Ni dhahiri Sonona siyo udhaifu wa kitabia, na wala haina maana kuwa mtu mwenye hali hiyo hana uwezo wa kufanya kitu chochote, bali ni hali ya kimedikali kama yalivyo magonjwa ya kisukari au vidonda vya tumbo, hivyo ni muhimu kwa mtu mwenye sonona kupata matibabu sahihi na stahili kwa wakati.
Katika kuadhimisha siku hii, WHO hutoa kaulimbiu inayobeba ujumbe maalum  ambao unalenga  kuhamasisha  na kuelimisha jamii juu ya suala mojawapo muhimu na lenye manufaa kiafya kwa nchi zote wanachama.
Ndiyo maana Tanzania imeungana na WHO kusimamia afya za wananchi kupitia Wizara yenye dhamana kwa kuunganisha nguvu pamoja katika maadhimisho ya mwaka huu kuelimisha jamii kujua na kumtambua hali ya sonona ili kuokoa maisha ya watu.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu “Sonona, Tuzungumze”, hii ni dira na mwongozo wa kuhamasisha wadau wote na jamii kwa ujumla kutambua ukubwa wa tatizo hilo kwa kila taifa na kimataifa.   
Hatua hii itasaidia jamii kujua visababishi vyake, umuhimu wa kubadili tabia na mienendo hatarishi ili kudhibiti na kujikinga na namna ya kupata huduma ya matibabu ya sonona mara baada ya kugundulika ana hali hiyo.
Watafiti wameonesha kuwa sonona huathiri watu wa rika zote na jinsia zote hasa vijana, wanandoa na kubainisha kuwa watu wenye umri mkubwa wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.
Hali hiyo inatokana na unyanyasaji wa kijinsia na kimwili unaosababishwa na mambo mbalimbali yaliyotokea mwanzoni wakati wa utoto ama karibuni, huzuni baada ya kufiwa na rafiki au mpenzi ama ndugu, kuvunjika kwa mahusiano kama uchumba au kuachwa (TALAKA), hatua hiyo hupelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo.
Hali chanya katika maisha kama kuoa, kupata kazi mpya, navyo vinaweza kusababisha mtu kupata ugonjwa wa sonona baada ya kuwa na furaha isiyo na kifani.
Katika Ulimwengu wa leo, pombe na matumizi ya madawa ya kulevya ni hatari zaidi kwa mtu mwenye sonona, akitumia vilevi hivyo vinaweza kuchagia hali yake kuwa mbaya zaidi.
Kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alilolitoa hivi karibuni amesema kuwa wizara yake inaendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na hali ya sonona kwa Watanzania.
Ni dhahiri jamii yenye afya bora inauwezo wa kuchangia kujenga taifa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025 kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
“Tunapozungumzia afya, tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na jinsi anavyohusiana na kushirikiana na wenzake katika familia na jamii kwa ujumla” amesisistiza Waziri Ummy.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni za Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu milioni 300 wanaishi na hali ya kuwa na sonona ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 18 kati ya mwaka 2005 hadi 2015.
Aidha, takwimu za WHO zinaonesha kuwa kati ya watu 5, mmoja kati yao ana matatizo au alishapata matatizo ya Sonona kutokana na ukweli kwamba watu wanaopata matatizo ya Sonona ni wachache tu wanaweza kufikia na kupata huduma ya afya, hata hao wanaohudhuria katika vituo vya Afya, wapo waliogundilika kuwa na tatizo la Sonona.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Afya ya magonjwa ya Akili ya mwaka 2015/2016 inaonesha Tanzania kuna takribani Wagonjwa 41,789 waliogundulika kuwa na tatizo la Sonona. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo linavyokisiwa kutokana na wagonjwa wachache kuudhuria vituo vya kutolea huduma kwa matatizo mbalimbali ya afya ya akili na matatizo ya kisaikolojia hapa nchini.
Naye Naibu Waziri Wizara hiyo Dkt. Hamis Kigwangalla amesema kuwa dalili za mtu mwenye Sonona ni pamoja na kuwa na msongo mkubwa wa mawazo, kukosa raha, usingizi na hamu ya kula, kujitenga na watu au jamii inayomzunguka na mara nyingine kutaka kujiua au kuwaua watu wengine.
Kinga ni bora kuliko tiba, iwapo mtu ameonesha kuwa na dalili zilizotajwa, familia na jamii wanashauriwa kuzungumza naye au mtu wake wa karibu anayemwamini kuhusu matatizo yake yanayokukabili ili upate ushauri na faraja itakayompunguzia msongo wa mawazo na kuondokana na tatizo hilo.
Dkt. Kigwangala amesisitiza kuwa mtu anapoona kuna dalili hizo ni vema apate muda wa kutosha, ale chakula, apumzika au kulala na aendelee kufanya shughuli alizokuwa anafanya kabla ya kupata Sonona na kuongeza iwapo dalili zinaendelea, mgonjwa apate ushauri wa kitaalam kutoka kwa mtoa huduma za afya katika kituo cha afya kilicho karibu nae.
Katika kukabiliana na Sonona, Waziri Ummy amesema ipo haja huduma za afya ya akili na saikolojia kutolewa katika maeneo ya kutolea huduma za afya kwa jamii, kuwa na kitengo maalumu kinachotoa huduma hizo katika hospitali zote nchini na kuboresha upatikanaji wa dawa.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali itapeleka wataalamu wa afya ya akili wakiwemo Madaktari Bingwa ili kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wale waliolazwa pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili waweze kutambua na kubaini mapema dalili za ugonjwa huu na kutoa matibabu stahiki au rufaa kwa wakati.
Ni vema Watanzania kutambua kuwa Sonona inazuilika kwa kujenga familia zenye mahusiano mazuri, kupendana, kupeana faraja na kusaidiana miongoni mwao.
Mwandishi wa makala haya anaunga mkono msisitizo wa Waziri mwenye dhamana kuwa upo muhimu watu wakachagua marafiki ambao wanaweza kuzungumza nao pindi wanapohitaji ushauri na faraja juu ya matatizo yanayowakabili, ni vizuri kuwasaidia watu wenye Sonona wapate ushauri wa kitaalam toka kwa watoa huduma za afya katika vituo vya huduma za Afya kwa wakati.