RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (31)
Akazungumza na mhudumu kwa Kichina kibovu, halafu akachukua ufunguo wa chumba cha Leila.
Wakati tukipita ukumbini, akasema, “Huyu kizee ni mpumbavu. Tutalifunga hili danguro lake. Hataki kukiri kwamba alikuwa kahaba — siwezi kumlaumu.”
Nikamchukia kwa sababu za kihisia. Leila, nilihisi, alistahili jambo zuri kuliko kuitwa kahaba na polisi huyu wa Kiskochi.

MacPherson alifungua mlango wa chumba cha Leila na kuingia kwenye chumba hicho kidogo. Nikabaki nje, nikichungulia ndani. Kwa ustadi mkubwa wa kipelelezi, akaanza kupekua chumba. Kulikuwa na magauni matatu tu yaliyotundikwa kwenye kabati na seti moja ya chupi kwenye saraka. Vitu vya Leila vilikuwa vichache sana.
MacPherson alitoa mguno wa ghafla wakati alipochungulia chini ya kabati.
“Nilifikiria zaidi . . .” akasema, akainama na kutoka na kutoa kibunda kidogo. Akakitoa taratibu. Ilionekana kama kimetoka kwenye pakiti ya sigara kumi.
“Unajua hii ni nini?” akauliza, akinionyesha. Katikati yake kulikuwa na alama nyeusi ya moshi.
“Wewe uniambie,” nikasema.
Aliinama tena na kuchungulia kwenye kabati na safari hii akatoka na mshumaa mdogo ulioungua nusu: ni aina ya mishumaa unayoiweka kwenye keki za siku ya kuzaliwa.
Akaketi kwenye upande mmoja wa kitanda, akiwa amemshikilia kitambaa na mshumaa na kukitanua.
“Alikuwa mtumiaji wa heroin,” akasema. “Watu zaidi ya kumi wanaotumia dawa za kulevya hujiua kila wiki.”
“Nini kinachokufanya uwe na uhakika huo?” nikamuuliza.
“yeyote ambaye ana vitu hivi viwili ni mraibu wa dawa za kulevya,” akasema MacPherson. “Unajua inafanyaje kazi? Wanaweka heroin kwenye kitambaa. Wanaweka mshumaa mdogo chini ya kitambaa na kunusa moshi wake. Inafanyika kwa sekunde chache. Unajua nini? Kitu cha kipumbavu ambacho Serikali ilifanya ni kutangaza vita kwa watumiaji wa dawa za kulevya. Walidhani ndicho kitu rahisi zaidi duniani kukifanya na kukizuia. Wavutaji wa dawa za kulevya lazima wawe na chumba, kitanda na vifaa kama hivi vya kuvutia ambavyo ni ghali. Huwa hatuppati shida kuvipata vyumba vyao na kuharibu vifaa vyao. Mtemba wa kuvutia dawa za kulevya unagharimu fedha nyingi sana, na baada ya muda wavutaji wakachoshwa na sisi kuvunja vitanda vyao na mitemba yao na kuwafukuza kwenye paa za nyumba. Tulijidanganya kwamba tulikuwa tunafanikiwa katika vita hiyo ya dawa za kulevya, lakini sasa kumbe tulikosea.” Akasogeza kofia yake nyumba ya kichwa chake wakati akinitazama. “Watumiaji waligundua kwamba wanaweza kupata heroin kutokana na opium na walichokuwa wanahitaji ni kipande cha kitambaa na mshumaa. Wanaweza kuvuta sumu hii mahali popote: kwenye sinema, kwenye maeneo ya umma, kwenye treni, mabasi, teksi – mahali popote. Kama utakkuwa unachunguza utashangaa kukuta alama za mishumaa katika maeneo yasiyotarajiwa. Hiyo itakueleza, kama tunavyoelewa sisi, kwamba kuna watu wamevuta heroin. Kuvuta opium ni uraibu, lakini haiui. Lakini usije ukakosea: heroin inaua. Kama tungewaacha Wachina wavute opium, tusingekuwa tunahangaika kupambana na wavutaji wa heroin.”
Nikakuna upande wa taya langu.
“Nashukuru wa darasa,” nikamwambia, “lakini sidhani kama amejiua na sidhani kama alikuwa mtumwa wa dawa za kulevya. Nadhani ameuawa na hivi vitu vimekuja kupandikizwa tu hapa ili uvione.”
Uso mkavu wa MacPherson haukuonyesha hali yoyote. Akachukua mtemba wake na kuujaza tumbaku.
“Ndivyo unavyodhani?” akauliza, akiwa amekerwa. “Mkuu amesema wewe ni kachero wa kujitegemea. Nimesoma kuhusu Chandler na Hammet — waliandika riwaya. Hii inaonekana kuwa ni maisha halisi.”
“Ndivyo ilivyo,” nikamwambia. “Sawa, usijali. Sidhani kama ina umuhimu sana.”
“Nini kinanchokufanya ufikirie kwamba ameuawa?” akauliza bila kuwa na hamu yoyote.
“hakuna ambacho kinaweza kukushawishi. Utavifanyaje vitu vyake?”
“Nitavipeleka polisi. Pengine atatokea mtu akavidai. Huyo mzee hapo mapokezi hajui kama alikuwa na ndugu yeyote. Nimewahi kuzungumza naye – hajui chochote kuhusu chochote.” Akasimama. “Nashauri usimfikirie sana.” Akaweka vitu vya Leila kwenye mkoba mdogo alioukuta juu ya kabati. “Kama ungekuwa unashughulika na kesi nyingi kama sisi tunavyofanya, wala usingemfikiria kabisa.”
“Nina uhakika. Hilo ndilo wazo lenyewe.”
Akanitazama kwa makini.
“Wazo gani?” akauliza.
“Watu waliomuua wasingependa wewe ufikirie mara mbili, au siyo?”
Akatabasamu.
“Oh, achana nalo. Tunakabiliana na mamia ya kesi hizi za kujiua. . . .”
Alikuwa amenichosha.
“Nimekusikia tangu mwanzo.” Nikaelekea chumbani kwangu. “Nitakuwepo hapa kwa siku chache kama utanihitaji.”
Akanichungulia, akiwa amepoteza kujiamini kwake.
“Nini kinachokufanya udhani kwamba nitakuhitaji?” akauliza.
“Sawa, tunaweza kusoma hadithi ya kachero pamoja,” nilisema na kufunga mlango.
Itaendelea kesho…