RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (30)
Nikaelekea chumbani kwangu. Niliona chumba cha Leila kikiwa kimefungwa na nikasimama kugonga. Hakukuwa na jibu. Nikajaribu kufungua mlango, lakini ulikuwa umefungwa. Nikagonga tena, likasikiliza, baada ya kutosikia chochote, nikaamua kwenda chumbani kwangu.
Ilikuwa ni mapema mno kufanya chochote hivyo nikavua jaketi langu, tai na viatu na kujilaza kitandani. Nikajaribu kuwaza kidogo lakini sikufika popote, halafu likapitiwa na usingizi.

Ilikuwa ni saa nne wakati niliposhtuka kutokana na mtu aliyekuwa akigonga mlangoni kwangu. Nikainuka haraka na kufungua mlango.
Kijana wa Kichina akainama, akiwa anatabasamu, na kuelekeza niende ukumbini. Nilivaa viatu vyangu na kumfuata hadi mapokezi. Mhudumu mzee akanipa mkonga wa simu.
Alikuwa Inspekta Mkuu MacCarthy.
“msichana huyu uliyeniambia,” akasema, “Ulisema umemnunulia pete ya jade jana usiku?”
Nikaganda kwa muda.
“Ndiyo . . . ilikuwa ni ya kulingana na jade.”
“Unaweza kuchukua teksi hadi kituo cha polisi cha Chatham Road? Kiko upande wa Kowloon. Wana msichana pale – anaweza kuwa huyo unayemzungumzia. Amevaa pete ya jade.”
“Amekufa?” nikauliza, nikijua mishipa yangu ya tumbo ilikuwa imebana.
“Oh, kitambo.” Niliweza kuhisi harufu ya moshi wa tumbaku lake kupitia kwenye simu. “Itasaidia kama utakwenda kumtambua. Muulizie Sajini Hamish.”
“Mskochi mwingine?”
“Ni sahihi kabisa. Waskochi wengi wako kwenye jeshi la polisi.”
“Pengine ni jambo jema kwa Scotland,” nikakata simu.
Dakika arobaini baadaye, nikapandisha ngazi za kituo cha polisi cha Chatham Road. Ndani ya ukumbi tu kulikuwa na ubao mkubwa ukutani wenye picha za kutisha hamsini za maiti za wanaume na wanawake wa Kichina waliokutwa mto Straits au mitaani huku kukiwa na maelezo ya Kiingereza na Kichina ya kuomba watambuliwe.
Sajini wa mapokezi akanielekeza kwenye ofisi ndogo ambako kijana mdogo mwenye uso mng’avu na mtazamo wa kipolisi alikuwa akikagua faili. Aliitikia wakati nilipoingia na kujitambulisha. Alisema jina lake alikuwa Sajini Hamish.
“Kuna maiti ambayo ninapaswa kuitambua,” nikamweleza.
Akachukua mfukoni mwake mtemba. Polisi wa Hong Kong walionekana ni wavuta mitemba. Nikamtazama akiujaza tumbaku, huku macho yake ya kijani yakiniangalia bila hamu yoyote.
“Ni sahihi. Inspekta Mkuu anadhani unaweza kumtambua. Aliopolewa kwenye Mto Straits jana usiku majira ya saa nane. Hakuna chochote kilichosalia. Inawezekana aliingia kwenye mojawapo ya injini za boti kwa namna alivyo.”
Nilihisi jasho jembamba likivuja mgongoni kwangu.
Akainuka.
“Hawa wanaharamu kila siku wanauana,” alisema kimazungumzo. “Kila siku tunaokota maiti si chini ya sita. Wachina wanaonekana hawayathamini maisha yao.”
Tulipita kwenye uchochoro, katika eneo la wazi hadi tukafika mochwari. Kulingana na rundo la karatasi na fomu zilizojazwa, inaonekana biashara ya kupokea maiti ilikuwa imepamba moto asubuhi hii.
Aliniongoza hadi kwenye meza, ambayo ilifunikwa na shuka zito la plastiki. Akainua upande mmoja wa shuka, akachungulia na kutoa kono mdogo ulio na pete ya jade.
“Nimekula mayai na nyama wakati wa kifungua kinywa,” alisema. “Kama utamtambua kwa pete, inaniokoa nisitapike.”
Niliitazama pete na vidole vidogo vyembamba. Ilikuwa ni pete niliyomnunulia Leila.
“Hiyo ndiyo pete haswa,” nilisema, na nilijihisi vibaya mno.
Akaurudisha mkono ndani ya shuka.
“Sawa, nitamwambia Inspekta Mkuu.”
Nikasogea mbele na kulifunua shuka la plastiki. Nikatazama kwa muda mrefu kuhusu mabaki ya aliyekuwa Leila. Bora hata nisingetazama, lakini nilipaswa kumuaga. Nikalirudisha shuka mahali pake.
Nikakumbuka jinsi alivyopumua kwa furaha baada ya kula kile chakula cha kumbukumbu. Nikakumbuka umbile lake kwa nyuma wakati alipokuwa amenitangulia. Sikuwa nimemfahamu kitambo, lakini tabia zake zilikuwa zimenifurahisha. Nikahisi nimempoteza mtu muhimu sana kwangu.
Kulikuwa na kachero aliyekuwa akinisubiri upande wa pili wa Feri. Alikuwa bonge la mtu mwenye uso mpana ambaye aliitwa MacPherson: ilionyesha hakuna mwisho wa hawa Waskochi. Akanirejesha hotelini kwenye gari ya polisi.
Itaendelea kesho…