RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (28) 
Mhudumu akaleta bakuli la wali uliochanganyika na maharage, shrimps na mayai ya kukaanga. Leila akajaza bakuli yake kwa kutumia vijiti na kuanza kutafuna haraka. Mimi nilikuwa nakula taratibu. Ili kukitendea haki chakula hicho, ulihitajika uzoefu wa kutosha kutumia vijiti.
“Aliishi naye kwenye hoteli unayoishi?” nikauliza wakati nilipodondosha wali kwenye kitambaa katika harakati za kuifuata kasi yake ya kula.
Akaitikia.
Zile shrimps zilikuwa zimepotea na nusu ya wali. Kwa hakika alikuwa na uwezo wa kula.

“Aliishi naye katika chumba pembeni ya chumba changu kwa miezi mitatu baada ya kuoana, halafu akaondoka.”
Bakuli kuba la supu ya  pezi la papa likawasili. Leila akaanza kujaza bakuli lake.
“Kwanini aliondoka?”
Akapandisha juu mabega yake.
“Hakumhitaji tena.”
Baada ya kuanza kunywa supu nikitumia kijiko, walau nikaweza kwenda na kasi yake.
“Kwanini hakumhitaji tena?”
Leila alitulia kwa muda na kunitazama kwa uchunguzi, halafu akaendelea kunywa supu.
“Alimuoa tu ili aweze kumsaidia kuishi,” akasema. “Baada ya kuanza kutengeneza fedha zake mwenyewe, hakumhitaji tena.”
“Aliwezaje kumhudumia Herman?” nikauliza, nikijua nini ambacho kingekuwa jibu lake.
“Alikuwa akiwastarehesha wanaume kama ninavyofanya,” Leila alisema, na kunitazama kwa huzuni. “Hatuna namna nyingine ya kutengeneza fedha.”
Mhudumu akaingia tena. Akaleta kipande cha zuria ambacho alikilaza mezani.
Leila akageuka kwenye kiti chake, akikunja mikono yake kwa furaha. “Huyu ndiye kuku wa ombaomba. Hupaswi kumkosa.”
Kijana wa Kichina akaingia akiwa amebeba kitu kilichoonekana kama yai la mbuni kwenye sahani ya mbao. Akaliweka yai kwenye kijizuria.
“kuku huyu kwanza anapakwa viungo vingi halafu anafungwa kwa majani ya lotus,” Leila akaelezea, akizunguka kwenye kiti chake kwa furaha. “Baadaye anafunikwa kwa udongo wa mfinyanzi na kupikwa kwa saa tano. Unaona udongo umekuwa mgumu kama jiwe.”
Kijana akatoa nyundo na kulivunja yai: ikatokea harufu nzuri ajabu. Mhudumu na kijana huyo wakachuchumaa kila upande. Yule kijana akamfungua kuku  na kumtoa kwenye majani ya lotus na kumweka kwenye beseni lililoshikiliwa na mhudumu. Ndege huyo alikuwa amepikwa vizuri na kuiva hasa kiasi kwamba ni nyama tu iliyodondoka kwenye beseni huku mifupa ikienda upande wake.
Kwa ujuzi mkubwa na mikono makini, mhudumu akatuwekea nyama ya kuku kwenye bakuli zetu.
Vijiti vya Leila vikaanza kazi yake tena. Name nikaanza kushambulia yangu. Kilikuwa chakula kkizuri mno ambacho nimewahi kula. Leila alitulia kwa muda, mnofu wa kuku ukiwa kwenye vijiti vyake na kuuliza, “Umeipenda?”
Nikatabasamu.
“Hakika. . .nimeipenda.”
Hakukuwa na haja ya kumuuliza maswali mengine mpaka chakula kilipokwisha. Niliona mawazo yake yote yalikuwa kwenye chakula na sikumlaumu. Tulimaliza kuku wetu, halafu akaagiza uyoga, ulanzi, tangawizi na keki. Mpaka hapo nilikuwa nimeshiba. Nikaketi, nikivuta sigara, nikitathmini kiasi cha chakula ambacho binti huyu anaweza kukijaza tumboni mwake. Baada ya dakika ishirini nyingine, akaweka chini vijiti vyake na kucheua kwa nguvu.
“Kilikuwa kizuri?” akasema, akiuliza.
Nilimkubalia kwa heshima kubwa. Mtu yeyote ambaye anaweza kula kiasi kama kile cha chakula kama alivyofanya yeye na kuendelea kuwa na umbile zuri alipaswa kuheshimiwa.
“Kilikuwa kizuri mno.” Nikamwambia.
Akatabasamu kwa bashasha.
“Ndiyo, kilikuwa kizuri. Samahani, unaweza kunipa sigara?”
Nikampatia sigara na kuiwasha. Aliutoa moshi kupitia kwenye midomo yake midogo na ghafla tabasamu lake likawa la kuvutia mno.
“Unataka kurudia hotelini sasa?” akasema. “Tunaweza kufanya mapenzi. Itakuwa vizuri baada ya chakula kama kile.”
“Bado mapema sana . . . tuna usiku mzima katikati yetu,” nikamwambia. “niambie zaidi kuhusu Herman Jefferson. Umesema alianza kutengeneza fedha baada ya kumuoa Jo-An. Alikuwa anatengenezaje?”
Akakunja uso. Niliona kwamba suala la Jefferson lilimkera.
“Sijui. Jo-An hakuwahi kuniambia. Siku moja nilimkuta peke yake akilia. Alisema Herman alikuwa amemwacha. Hakumhitaji tena kwa sababu alikuwa anatengeneza fedha nyingi wakati huo.”
“Hakukwambia alikuwa anatengeneza namna gani?”
“Kwanini aniambie? Haikunihusu mimi.”
“Aliwahi kurudi tena?”
“Oh, alikuja mara moja moja.” Leila akaonyesha uso wa furaha. “Wanaume wanarudi wanapotaka kubadilisha. Alikuja mara chache usiku na kuondoka.”
“Jo-An alifanya nini baada ya Herman kumwacha?”
“Kufanya nini?” Leila akanitazama. “Angefanya nini? Akaendelea kufanya kazi zake za kila siku zilizomweka mjini.”
“Kuwastarehesha wanaume?”
“Kazi gani nyingine angeifanya ili aishi?”
“Lakini kama Jefferson alikuwa anatengeneza fedha na yeye alikuwa mekwe, hakika itakuwa alimpatia kiasi?”
“Hakumpa chochote.”
“Unafahamu alikokuwa anaishi baada ya kuondoka?”
“Jo-An aliniambia kwamba alikuwa amekodi hekalu kubwa lililomilikiwa na mcheza kamari wa Kichina huko Repulse Bay. Nimeliona eneo hilo.” Leila alivuta pumzi ndefu na kuzishusha. “Ni pazuri sana . . . hekalu kubwa jeupe lenye ngazi zinazoshuka baharini na bandari ndogo pamoja na boti.”
“Jo-An aliwahi kwenda huko?”
Leila akatikisa kichwa.
“Hakuwahi kukaribishwa.”
Mhudumu alikuja akitabasamu na kuinama. Akanipatia bili yangu. Gharama ya chakula ilikuwa ndogo ajabu. Nikalipa wakati Leila akinitazama kwa furaha kubwa usoni mwake.
“Umeridhika?” akauliza.
“Kilikuwa chakula kizuri.”
“Twende hotelini halafu tufanye mapenzi.”
Nilikuwa Hong Kong. Kulikuwa na mazingira haya ya kusalimu amri kwa hisia ambazo zilifanya malumbano yasiwepo. Pamoja na hayo, sikuwahi kufanya mapenzi na msichana wa Kichina. Kilikuwa ni kitu ambacho niliona inabidi nifanye.
“Sawa,” nikasema, nikisimama. “Twende hotelini.”
Tukaingia ukumbini kwenye kelele na hatimaye tukatoka nje.
Tukaanza kutembea kwenye Barabara ya Nathan.
“Pengine ungependa kuninunulia zawadi?” Leila akasema, akiuchukua mkono wangu na kutabasamu kwa kushawishi.
“Nilitaka nikueleze. Unapendelea nini?”
“Nitakuonyesha.”
Tukatembea kidogo, halafu akaniongoza kwenye mtaa mmoja wenye maduka madogo. Mbele ya kila duka, alisimama mchuuzi wa Kichina mwenye tabasamu.
“Ningependa uninunulie pete ili nikukumbuke,” alisema Leila. “Haipaswi kuwa ya gharama.”
Tukaingia kwenye doka mojawapo la sonara na akachagua pete. Haikuwa pete nzuri sana, lakini kwake ilionekana ya thamani. Muuzaji akaomba apatiwe dola arobaini za Hong Kong. Leila na muuzaji wakaanza kupatana na hatimaye wakafikia kwenye bei ya dola ishirini na tano.
“daima nitaivaa,” akasema, akitabasamu wakati akiitazama pete hiyo kidoleni mwake. “daima nitakukumbuka kwa pete hii. Sasa twende hotelini.”
Ilikuwa baada ya kushuka kwenye boti wakati nikipungia mkono teksi ndipo nilipogundua kwamba nimempoteza. Ni kitu ambacho sijakkielewa mpaka sasa. Wachina watatu wenye maumbile makubwa, waliovalia suti nyeusi, walinikinga wakati teksi iliponifikia. Mmojawao aliinama na kuomba radhi kwa Kiingereza kibovu wakati wenzake wawili wakinizunguka, halafu wote watatu wakaondoka kwenye gari lililokuwa linawasubiri. Nilipogeuka kumtazama Leila hakuwepo. Ilikuwa kana kwamba njia ilifunua kinywa na kummeza.
Itaendelea kesho…