Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (26)




Nikamtazama akikatiza kwenye chumba hicho na kwenda mahali simu ilikokuwa kwenye baa. Wakati alipokuwa anapiga simu, mmoja wa mabaharia wa Kimarekani akamwendea na kuweka mkono wake begani mwake. Akamwashiria anyamaze ambapo Mmarekani huyo aligeuka kunitazama na kunipungia. Nami nikampungia. Mazingira ya kwenye baa hii yalikuwa tulivu mno na rahisi. Hakukuwa na ugumu wowote katika biashara hii niliyotaka kuifanya. Wakati mwanamke aliporudisha mkonga wa simu chini, kila mmoja, wakiwemo wahudumu, walijua nilikuwa nimeagiza msichana na alikuwa njiani anakuja. Wote walionekana kufurahia tukio hilo.

Mwanamke yule akazungumza na baharia na akanyanyua mkonga tena. Biashara ilionekana kwenda vizuri.
Nilimaliza kinywaji changu, nikawasha sigara, halafu nikamuashiria muhudumu aniletee kinywaji kingine.
Wamarekani wawili waliovalia mashati ya fujo, walikuja na kuketi kwenye meza mbali kidogo na mimi. Baada ya mwanamke wa Kichina kumaliza kupiga simu akanijia.
“Atawasili baada ya dakika kumi,” akasema. “Nitakueleza mara baada ya kuwasili,” na baada ya kumwitikia, akawaendea Wamarekani wawili na kuketi nao. Baada ya mazungumzo ya dakika tano akainuka na kwenda kupiga simu tena.
Takriban robo saa baadaye, mlango wa baa ukafunguliwa na binti wa Kichina akaingia. Alikuwa mrefu na amejengeka vizuri. Alikuwa amevalia gauni la Ki-Ulaya lililombana lenye rangi nyeusi na nyeupe. Mkoba wenye rangi nyeusi na nyeupe ulining’inia kwenye mkanda ambao aliuzungusha kwenye mkono wake. Alikuwa mzuri, mrembo na mwenye mvuto. Alimtazama mwanamke wa Kichina ambaye alimuashiria kwangu. Binti huyo akanitazama na kutabasamu, halafu akakatisha kwenye baa, akitembea kwa madoido huku baadhi ya mabaharia wa Kimarekani wakimtazama, na kunionyesha ishara ya kukubali.
Akaketi pembeni yangu.
“Hello,” akasema. “Unaitwa nani?”
“Nelson,” nikamwambia. “Wewe unaitwa nani?”
“Jo-An.”
“Jo-An—nani?”
Akanyoosha mkono na kuchukua sigara katika paketi yangu iliyokuwa mezani.
“Ni Jo-An tu.”
“Siyo Wing Cheung?”
Akanitazama ghafla na kutabasamu. Alikuwa na meno mazuri meupe.
“Hilo ni jina langu. Umejuaje?”
“Rafiki yangu alikuwa hapa mwaka jana,” nikamwambia, nikijua kwamba alikuwa ananidanganya. “Aliniambia nikutafute nikija.”
“Nimefurahi sana.” Aliiweka sigara katikati ya midomo yake na kuiwasha. “Unanipenda?”
“Tena sana.”
“Tunaweza kuondoka?”
“hakuna shida.”
“Unaweza kunipa denye dhahabu.
“Umeridhika naye?”
“Nani ambaye ahawezi kuridhika naye?”
Akachukua dola tatu.
“Njoo unitafute tena,” akasema. “Siku zote niko hapa.”
Binti aliyejiita mwenyewe Jo-An akasimama na kuelekea mlangoni. Nikamfuata, nikiwapungia kwa kuwaaga mabaharia. Mmojawao akatengeneza herufi ‘O’ kwa vidole vyake gumba na shahada. Nikaachana nao na kutoka nje ambako binti alikuwa ananisubiri.
“Ninaifahamu hoteli safi na nafuu,” akasema.
“Hata mimi naijua,” nikamwambia. “Nimefikia Celestial Empire. Tutakwenda pale.”
“Itakuwa vyema twende kwenye hoteli yangu.” Akanitazama kwa kijicho-pembe.
“Tutakwenda kwenye hoteli yangu,” nikasema, na kumkamata mkono, nikamuongoza katika ya msongamano wa watu mtaani kuelekea hotelini.
Akatembea pembeni yangu. Alikuwa amejipulizia manukano aghali sana. Sikujua ni aina gani, lakini yalikuwa mazuri. Uso wake ulionekana kuwa na mawazo mengi mno. Hatukuzungumza chochote wakati tukitembea. Alipandisha ngazi ndefu za hoteli. Umbile lake kwa nyuma lilivutia sana na miguu mizuri mirefu. Alitingisha nyunga yake kitaalam wakati akipanda ngazi moja hadi nyingine. Nikajikuta nimezama kuangalia mwendo wake kuliko hata hali iliyokuwepo mbele yangu.
Yule mzee wa mapokezi alikuwa anasinzia. Alifumbua jicho moja na kumtazama msichana, halafu mimi, akafumba jicho tena.
Nikamuongoza kwenye korido. Leila alikuwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake uliokuwa wazi, akipaka rangi kucha zake. Alimtazama msichana na kunikonyeza kwa dhihaka. Nami nikamkonyeza, nikafungua mlango na kumuongoza msichana wangu kwenye chumba chenye joto.
Nilifunga mlango na kuweka komeo.
Akaniambia, “Unaweza kuniongeza zaidi ya dola thelathini? Nitakuwa mzuri zaidi ukinipa hamsini.”
Akafungua zipu ya gauni lake kuonyesha umbile lake. Alikuwa amefungua nusu ya gauni lake kabla sijamzuia.
“Subiri kwanza,” nikamwambia, nikichukua pochi yangu. “Hatupaswi kuharakisha mambo katika hili.”
Akanitazama. Nikachukua picha ya marehemu Jo-An iliyopigwa akiwa mochwari na kumpatia. Uso wake mwembamba, wa kuvutia ukaonyesha mashaka. Akaitazama picha, halafu akanitazama.
“Hii ni nini?” akauliza.
“Picha ya Jo-An Wing Cheung,” nilisema, nikiketi kitandani.
Taratibu akaifunga zipu ya gauni lake. Uso wake sasa ukaonyesha fadhaa.
“Ningejuaje kama ulikuwa na picha yake?” akasema. “Madame alisema usingeweza kujua jinsi alivyo huyo msichana.”
“Ulikuwa unamfahamu?”
Akapandisha midomo yake hadi puani.
“Kwani yeye ni muhimu sana? Mimi ni mzuri kuliko yeye. Hupendi kufanya mapenzi na mimi?”
“Nimekuuliza tu kama ulimfahamu.”
“Hapana. Sikumfahamu kabisa.” Akasogea pembeni kwa mashaka. “Ninaweza kuchukua vitu vyangu?”
Nikahesabu noti tano za dola kumi kumi, nikazikunja na kuzishika mkononi ili azione.
“Aliolewa na Mmarekani. Jina lake alikuwa Herman Jefferson,” nikamwambia. “Ulikuwa unamfahamu huyo mwanamume?”
Akajifanya kama kukumbuka.
“Nilikutana naye.” Akaitazama tena picha ya Jo-Ann. “Kwanini anaonekana hivi. . . anaonekana kana kwamba amekufa.”
“Ndivyo alivyo.”
Akaidondosha picha chini kama imemng’ata.
“Ni mkosi kutazama picha za watu waliokufa,” akasema. “Nipe vitu vyangu. Nataka kuondoka.”
Nikachukua picha ya Herman Jefferson na kumuonyesha.
“Je, huyu ndiye mumewe?”
Hakuweza kuitazama vizuri picha hiyo.
“Nimekosea. Sijawahi kukutana na mumewe. Naomba vitu vyangu niondoke.”
“Umesema uliwahi kukutana naye.”
“Nimekosea.”
Tukatazamana. Nikaona kwa kumwangalia tu kwamba nilikuwa napoteza muda wangu. Hakuwa tayari kuniambia chochote. Nikampatia fedha ambazo aliziweka kwenye mkoba wake.
“Kuna fedha nyingi zilikotoka hizo kama unaweza kunipatia taarifa kuhusu Jefferson,” nikamwambia bila matumaini yoyote.
Akaelekea mlangoni.
“Sijui chochote kumhusu. Asante sana kwa kunipatia fedha.”
Akatoa komeo, akafungua mlango na kuondoka.
Nilijua alikuwa amedanganywa tu ili aje anidanganye, lakini kwa vile nilikuwa natumia fedha za Jefferson, sikufikiria lolote kuliko kama ningekuwa natumia fedha zangu mwenyewe.
Itaendelea Jumatatu…

Comments