Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (25)




Nikashikana naye mikono na kutoka nje kwenye pilika katika Mtaa wa Queen’s Road. Muda ulikuwa saa kumi na mbili na nusu. Ubalozi wa Marekani utakuwa umefungwa: lakini sikuwa na uhakika wa kupata taarifa zozote ambazo zingenisaidia kuhusu Jefferson au mkewe. Kama nilitaka kupata taarifa nilizozihitaji ningetegemea jitihada zangu binafsi katika kuchimba hapa na pale, lakini wapi pa kuanzia ndilo swali lililonitatiza.

Nilizunguka mjini kwa takriban saa moja, nikiangalia maduka na kupunga hewa ya eneo hilo ambayo niliipenda mno. Baadaye nikaona kwamba kinywaji kkingeniweka sawa na nikaondoka kuelekea Wanchai. Hapo nikakuta baa kadhaa ndogo ndogo, kila moja ikiwa na kijana wa Kichina aliyechuchumaa ambaye aliniita kwa kunikonyeza ili niende hapo. Biashara ni mbinu, lazima ubuni namna ya kuwavutia wateja!
Nikaingia mojawapo ya baa hizo iliyokuwa na bango kubwa la tangazo la bia na kuketi kwenye meza mbali na kelele za muziki uliotoka kwenye juke-box. Mabaharia wa Kimarekani kama sita hivi walikuwa ndani ya baa hiyo, wakkinywa bia. Wafanyabiashara wawili wa Kichina wakaketi jjirani na mimi, wakizungumza kwa kunong’ona, faili la makaratasi likiwa mbele yao. Mabinti kadhaa wa Kichina waliketi kwenye benchi upande wa nyuma wa chumba hicho, wakizungumza hili na lile taratibu.
Mhudumu alinijia na nikamwambia aniletee Scotch na Coke. Baada ya kunihudumia, mwanamke mmoja wa makamo Mchina, akiwa amevaa Cheongsam ya rangi ya kijani, akatokea kutoka kusikojulikana na kujikaribisha kwenye kiti kilicho wazi kilichokuwa kikitazamana na mimi mezani kwangu.
“Habari za jioni,” akanisalimia, macho yake makali meusi yakinipeleleza. “Ndiyo mara ya kwanza kufika Hong Kong?”
“Yeah,” nikamjibu.
“Unaonaje kama nikikupa kampani hapa?”
“Hakuna shida. Ninaweza kukununulia kinywaji?”
Akatabasamu: meno yake yalikuwa yamepachikwa dhahabu.
“Ninapenda bilauri ya maziwa.”
Nikamwashiria mhudumu aje lakini inaonekana alijua nini alichotakiwa kukileta hivyo akaitikia, akaondoka na kuja na bilauri ya maziwa.
“Chakula cha hapa ni kizuri,” mwanamke huyo akaniambia, “kama utapendelea kula.”
“Bado mapema sana kwangu. Unatumia kitu kingine zaidi ya maziwa?”
“Hapana. Umefikia Gloucester? Ndiyo hoteli nzuri sana.”
“Nimeambiwa hivyo.”
Akanitazama kwa jicho la udadisi.
“Utapenda upatiwe binti mzuri? Nina wasichana wazuri na wabichi kabisa. Nitakachofanya ni kupiga simu na watamiminika hapa uchague. Hupaswi kuwa nao kama huhitaji. Nitawaita, lakini wasikutishe. Utaniambia kama mmojawao amekuvutia name nitaandaa kila kkitu.”
“Asante, lakini siyo sasa hivi. Unapata wakati mgumu kutafuta wasichana?”
Akacheka.
“Nina tatizo la kutowapata. Kuna wasichana wengi hapa Hong Kong. Kitu gani wanachoweza kukifanya kama si kuwaburudisha wanaume? Hong Kong imejaa wasichana warembo wadogo ambao wana hamu ya kutengeneza fedha kidogo.”
Hoteli ya Celestial Empire ilikuwa umbali wa yadi mia mbili au mia tatu kutoka hapa baa. Ilionekana kwamba kama mwanamke huyu alikuwa akiwadhibiti makahaba katika eneo hilo, lazima atakuwa anamfahamu Jo-An.
“Rafiki yangu alipokuwa hapa mwaka jana alikutana na msichana ambaye alimpenda sana,” nikamwambia. “Jina lake ni Jo-An Wing Cheung. Ningependa kukutana naye. Unamfahamu?”
Kwa kkitambo kidogo, mamcho yake meusi yalionyesha mshangao. Kama nisingekuwa namtazama kwa makini wala nisingegundua mabadiliko ya ghafla usoni mwake. Halafu akatabasamu, vidole vyake vyembamba vilivyopakwa rangi vikiwa vinachora tattoo mezani.
“Ndiyo, hakika namfahamu,” akasema. “Ni msichana mzuri. . . mrembo hasa. Utampenda sana. Ninaweza kumpigia simu sasa hivi kama unamtaka.”
Ilikuwa zamu yangu kuficha mshangao.
“Sawa, mpigie tu?” nikamwambia nikiwa na mshangao ambao nilijitahidi kutouonyesha.
“Ni msichana wangu bora zaidi,” mwanamke huyo akaendelea. “Unaweza kwenda naye hotelini kwako? Anaishi na wazazi wake na hawezi kumchukua mwanamume kumpeleka kwao. Itakuwa dola thelathini za Hong Kong kwake yeye na dola kumi kwa ajili ya chumba.” Akatabasamu na kuonyesha meno yake yenye dhahabu. “Na dola tatu kwangu mimi.”
Nilishangaa Mzee Jefferson angesemaje kama ningemuorodheshea vitu vyote hivi kwenye karatasi yangu ya matumizi.
“Hakuna shida,” nikamwambia, na ikawa zamu yangu kutabasamu. “Lakini nitajuaje msichana huyo kama ni Jo-An? Anaweza kuwa mwingine kabisa, au siyo?”
“Unapenda utani?” akauliza, akinitazama kwa makini. “Yeye ndiye Jo-An. Unadhani atakuwa nani tena?”
“Ni kweli kabisa. Ninapenda utani.”
Akainuka.
“Ngoja nipige simu.”
Itaendelea kesho…

Comments