RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (24)
Msichana wa Kichina alikuwa amesimama kwenye kizingiti cha mlango wa chumba kilichotazamana na changu. Alikuwa na umbile dogo, lakini lililojengeka vyema: nywele zake maridadi nyeusi zilikuwa zimesukwa na kuning’inia shingoni. Alikuwa amevalia lauzi nyeupe na sketi ya buluu nzito. Alivutia kumtazama bila kuwa mrembo. Alikuwa akinitazama kana kwamba alikuwa akisubiri kwa muda wote kwamba nitatokea.

“Hello, mheshimiwa,” akasema huku tabasamu pana likiwa limechanua usoni mwake. “Naitwa Leila. Jina lako nani?”
Nikalipenda tabasamu lake na nikayapenda meno yake meupe.
“Nelson Ryan,” nikamwambia, nikifunga mlango wangu. “Unaweza kuniita Nelson. Unaishi hapa?”
“Ndiyo.” Macho yake meusi ya kirafiki yakaanza kunisawiri. “Ni wanaume wachache wa Kimarekani wanaoishi hapa. Wewe unaishi hapa?” akaniuliza.
“Ndiyo maana yake, umekuwepo hapa muda mrefu?”
“Miezi kumi na nane.” Alikuwa na lafudhi ya kipekee. Ilibidi niwe makini kuweza kuelewa alichokuwa anasema. Alinitazama kwa mtazamo ule unaomaanisha alichokimaanisha. “Ukitaka kufanya mapenzi, utakuja kunichukua?”
Nilishtushwa kwa muda, halafu nikafanikiwa kutabasamu.
“Nitakumbuka, lakini usinitegemee sana.”
Mlango ukafunguliwa mbele kabisa ya korido na mtu mmoja mfupi ambaye angeweza kuwa Mtaliano au Mfaransa akatoka nje. Akaja haraka upande wangu, bila kunitazama. Alifuatiwa na msichana wa Kichina. Sidhani kama alikuwa na miaka zaidi ya kumi na sita, lakini ni vigumu kujua kwa watu hawa wenye maumbile madogo. Akanitazama kwa mvuto wakati akinipita. Mpaka wakati huo nikatambua ni hoteli gani hiyo niliyokuwa nimefikia.
Leila akaweka mikono yake mizuri chini ya matiti yake madogo na kuyapandisha juu.
“Ungeweza kuja kwangu sasa hivi?” akauliza kwa utulivu.
“Siyo wakati huu,” nikamwambia. “Nina kazi. Pengine wakati mwingine.”
“Wanaume wa Kimarekani kila wakati wako bize,” akasema. “Labda usiku, au?”
“Nitakwambia.”
Akakata tamaa.
“Hiyo haimaanishi chochote, unaweza kuja au usije.”
“Ndiyo maana yake,” nikamwambia. “Kwa sasa kuna mambo ninayafanya,” na nikaelekea kwenye ukumbi wa mapokezi ambako karani wa mapokezi mzee wa Kichina aliketi akiwa ametulia kama Buddha.
Nikateremka ngazi hadi mtaani kulikojaa watu, kelele na joto kali. Kijana wa mkokoteni akaja moja kwa moja kunifuata.
“Makao makuu ya polisi,” nikamwambia mara tu baada ya kuingia kwenye mkokoteni wake wa abiria.
Akaondoka akikimbia. Baada ya kuondoka umbali wa yadi mia mbili au mia tatu, nikagundua kosa nililolifanya kuchukua usafiri wa aina ile. Magari makubwa, ya kati na malori hayakuwathamini wenye mikokoteni. Kila sekunde nikahisi kwamba nitagongwa na lori au kwa gari kubwa lenye kasi la Kimarekani. Nikashusha pumzi baada ya kufika nje ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Hong Kong, nikishangaa kwamba bado nilikuwa katika hali salama.
Baada ya kueleza kilichonipeleka kwa sajini aliyekuwa mapokezi, hatimaye nikaelekezwa kwenye ofisi ndogo, safi ambako Inspekta Mkuu mwenye nywele nyeupe na sharubu za kijeshi akanitazama kwa jicho lisilo la kirafiki wakati akinielekeza kwenye kiti.
Nikamweleza mimi ni nani naye akanieleza jina lake. Jina lake alikuwa MacCarthy na alizungumza lafudhi ya Kiskochi.
“Jefferson?” Akazirudisha nywele zake kwa nyuma kwa kuinua kichwa na kunyanyua mtemba wa Dunhill ulioonekana kuzeeka. Wakati alipoanza kuujaza tumbaku, akaendelea, “Nini kilichokuvutia sana? Tayari nimekwishashughulikia suala hilo hilo baada ya kuulizwa na polisi wa Jiji la Pasadena kuhusu huyo mtu. Yeye ni nani kwako?”
Nikamwambia nilikuwa namwakilisha Mzee J. Wilbur Jefferson.
“Ninahitaji kupata taarifa za kutosha kuhusu mwanaye na mkewe wa Kichina kwa kadiri itakavyowezekana,” nikamwambia. “Chochote utakachoniambia kinaweza kusaidia.”
“Ubalozi wa Marekani unaweza kusaidia zaidi,” akasema, akiwasha mtemba wake. Akapuliza moshi wenye harufu ya tumbaku ghali kwangu. “Sifahamu mambo mengi kumhusu. Aliuawa kwenye ajali ya gari. Nadhani umesikia kuhusu hilo?”
“Ajali hiyo ilitokeaje?”
Akapandisha mabega yake.
“Alikuwa akiendesha kasi kwenye barabara yenye utelezi. Hakukuwa na cha ziada cha kuchukua wakati tulipomkuta. Alikuwa ndani ya gari ambalo liliungua moto baada ya kupata ajali.”
“Hakuwa na mtu yeyote?”
“Hapana.”
“Alikuwa anaelekea wapi?”
MacCarthy akaanza kunitazama kwa udadisi.
“Sifahamu. Ajali ilitokea yapata kilometa tano nje ya Kowloon katika eneo la New Territories. Pengine alikuwa anakwenda mahali.”
“Nani aliyemtambua?”
Akajiweka sawa, akionyesha utulivu wa kutosha.
“Mke wake.”
“Unaweza kunieleza kidogo historia yake? Alikuwa anapata riziki kwa kazi gani?”
“Sidhani kama ninaweza.” Akatoa mtemba mdomoni mwake na kutazama kitezo cha majivu. “Hakuwa mtu aliyenisumbua kwa bahati nzuri. Alijitahidi kuwa mbali nasi. Hapa hatuwafuatilii watu shughuli zao mpaka wanapofanya makosa na Jefferson alikuwa makini asifanye hivyo. Mara kadhaa tulikuwa tukipata taarifa zake hapa na pale. Hakuwa raia mwema. Hakuna mashaka yoyote kwamba alikuwa akitegemea mapato haramu ya mkewe, lakini hapa pia, hatuingilii maisha ya raia wa Marekani, kama nitaliweka sawa hilo.”
“Taarifa zozote kuhusu mwanamke?”
Alivuta moshi na kuonekana kuchoshwa.
“Alikuwa kahaba, ndio ukweli wenyewe. Hili ni tatizo tunalojitahidi kupambana nalo, lakini siyo rahisi. Hawa wasichana wakimbizi wanaishi kwa taabu kupata fedha: ukahaba ndiyo njia rahisi zaidi kwao. Taratibu tunasafisha mji, lakini ni kazi ngumu.”
“Najaribu kufikiria ni kwa nini aliuawa.”
Akapandisha mabega yake.
“Siwezi kusaidia kwa hilo.” Akatazama rundo la karatasi zilizokuwa kwenye dawati lake. “Nimetoa taarifa zote nilizonazo kuhusu hawa wawili kwa Luteni Retnick. Hakuna cha ziada ninachoweza kuongeza.”
Hapa tafsiri yake ilionekana kwamba baada ya Retnick, mimi ni mtu mwingine niliyepewa taarifa hizo. Nikasimama.
“Sawa, asante. Wacha ninuse mitaani. Pengine ninaweza kupata zaidi.”
“Sina uhakika.” Akazivuta karatasi upande wake. “Kama kutakuwa na lolote ninaloweza kulifanya. . . .”
Itaendelea kesho…