RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (22)Mtu mnene, mwenye ndevu zilizoloa jasho na kichwa chenye kipara, aliinuka na kuinama kwa mbele kuchungulia dirishani wakati bango la ‘No Smoking’ lilipoonekana.
“Sawa, tumekwishaingia—Hong Kong,” alisema akigeuka kwa begani kunitazama. “Inaonekana ni pazuri. Wanasema hakuna mahali pazuri duniani kama hapa. Wanaweza wakawa sahihi.”

Wakati kichwa chake kikubwa kilipokuwa kinanikinga, nilikuwa nahangaika kuufunga mkanda wangu. Baadaye alipoketi na kuufunga mkanda wake, nikafanikiwa kuiona milima ya kijani, bahari ya buluu iliyong’ara na boti kadhaa kabla ya ndege kutua kwenye njia ya kurukia.
Mtu huyu mnene ambaye alikuwa jirani yangu tangu tulipoondoka Honolulu, alisimama kuchukua kamera yake na begi lenye nembo ya Pan-American Airways.
“Unafikia hoteli ya Peninsula?” akaniuliza.
“Mimi niko upande wa pili.” Nikamjibu.
Uso wake ulionyesha kutoridhika.
“Kowloon ni nzuri: maduka mazuri: hoteli nzuri, lakini pengine uko hapa kwa shughuli za biashara?”
“Ni kweli kabisa,” nilimjibu.
Jibu hilo lilionekana kumfurahisha.
Abiria wengine kwenye ndege wakaanza kuchukua mabegi yao. Pilika za daima za utulivu na kusukumana zikaendelea kwa muda kabla ya mimi kupata nafasi kutoka nje kwenye jua linaloangaza.
Ilikuwa safari nzuri, kidogo ndefu, lakini niliifurahia. Dakika kumi baadaye, nilikuwa nimepita kwenye forodha na kutoka nje kwenye kelele nyingi za uwanja wa ndege. Nilimuona jirani yangu akichukuliwa na basi la hoteli. Alinipungia mkono name nikampungia. Vijana kadhaa wa mikokoteni wakanizunguka, wakipiga kelele na kuninyooshea mikono. Walikuwa na nyuso zilizozeeka pengine kutokana na hali ya maisha. Wakati nikiwa nimesimama kwa kusita, Mchina mmoja mnene, mfupi, aliyevalia nadhifu suti maridadi, akanijia na kuinama kidogo.
“Samahani, tafadhali,” akasema. “Pegine naweza kukusaidia? Unahitaji teksi?”
“Nahitaji kufika Celestial Empire Hotel huko Wanchai,” nikamwambia.
“Hiyo iko kisiwani, mheshimiwa.” Alionekana kushangaa kwa namna ya ukarimu. “Itakuwa vyema ukichukua teksi hadi Feri halafu uvuke kwenda Wanchai. Hoteli ipo karibu na Feri kwa upande wa ng’ambo.”
“Asante sana,” Nikamwambia. “Dereva wa teksi atakuwa anafahamu kuzungumza Kiingereza?”
“Wengi wao wanafahamu Kiingereza kidogo.” Akamuashiria dereva wa teksi mmoja katika maegesho. “Kama utaniruhusu. . .”
Akanitangulia mbele. Nilibeba begi langu na kumfuata. Alizungumza na dereva kwa lugha ya Ki- Cantonese. Dereva mwenyewe Mchina, mwembamba na mchafu, aliguna, akanitazama, halafu akatazama pembeni.
“Atakupeleka Feri, mheshimiwa,” Mchina mfupi akaniambia. “Nauli yake ni dola moja: siyo dola ya Marekani, umeelewa, ni dola ya Hong Kong. Kama unavyofahamu, dola moja ya Marekani ni sawa na sola sita za Hong Kong.” Akatabasamu. Kila jino mdomoni mwake lilikuwa limepachikwa jino la dhahabu. “Huwezi kusumbuka kuipata hoteli utakapofika ng’ambo. Inatazamana na Feri.” Alisita kidogo, halafu akasema kwa hadhari, “Unajua hoteli hii mara nyingi Wamarekani huwa hawafikizii? Samahani kwa kuingilia, lakini Wamarekani wengi wanapendelea hoteli za Gloucester au Peninsula. Hii Celestial Empire ni kwa ajili ya Waasia.”
“Yeah, ni hapo ndipo ninataka kufikia,” nikamwambia. “Asante kwa msaada wako.”
“Karibu sana, mheshimiwa,” alisema, akachukua pochi yake na kunipatia kadi. “Unaweza kuhitaji muongozaji. Ndiyo kazi yangu kuwaongoza Wamarekani wanaotembelea Hong Kong. Wewe piga simu tu. . . .”
“Asante. Nitakumbuka.” Nikaibana kadi kwenye mkanda wa saa yangu ya mkononi, nikainama kidogo, na kuingia kwenye teksi.
Wakati nikiwa kwenye ndege nilikuwa nimepitia ramani ya Hong Kong, nikagundua kwamba upande wa bara mahalli ulipo uwanja wa ndege wa Kai Tak uliitwa Kowloon Peninsula na eneo la Straits lenye maji ni katikati ya kisiwa cha Hong Kong, ambacho kinafikiwa na boti za mwendokasi kwa mwezo wa dakika nne au tano.
Wanchai, ambako Jefferson alikuwa akiishi, lilikuwa eneo la mbele ya maji hapo Hong Kong.
Mwendo wa kutoka uwanja wa ndege hadi Feri ulichukua dakika chache tu. Eneo la ufukweni mwa Kowloon lilisheheni watu wengi wengine wakiwa wanakimbia. Ilionekana kwamba kuna Mzungu mmoja kati ya Wachina mia moja: hali iliyonikumbusha kwamba ni eneo lenye pilika za wenyeji. Makuli, wakiwa wamebeba mizigo mizito kwa kutumia fimbo za mianzi, walikimbia kukatiza barabarani, wakati mwingine wakkinusurika kugongwa na magari. Magari makubwa ya Kimarekani, yakiendeshwa na wafanyabiashara wanene wa Kichina, vijana wa mikokoteni wakiwa wamebeba makreti na bidhaa za ajabu na malori makubwa ndiyo yaliyojaza mtaa. Mabango ya rangi nyekundu yaliyoandikwa Kichina yalipamba sehemu za mbele za maduka. Watoto wadogo wa Kichina, wakiwa wamebeba watoto migongoni mwao, walikuwa wakicheza kwenye vibaraza na viambaza. Familia za Kichina zilikuwa zimechuchumaa kwenye viambaza mbele ya maduka yao, wakila wali kwa kutumia vijiti.
Nilipofika Feri, nilimlipa dereva wa teksi, nikannunua tiketi na kuingia kwenye boti ambayo tayari ilikuwa imesheheni wafanyabiashara wa Kichina, watalii wa Kimarekani na mabinti kadhaa wa Kichina waliovalia nguo aina ya Cheongsams, zilizokatwa pembeni kuonyesha miguu yao minene.
Nilipata siti karibu na ngazi na mara boti ilipoanza kukatisha maji ya Straits kuelekea kisiwa cha Hong Kong, nikajaribu kuyazowea mazingira yaliyonizunguka.
Itaendelea kesho…