RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (21)
“Simfahamu: ni jamaa tu. Ungependa risasi iingie wapi, Buster? Mimi ni mtaalamu wa bastola. Risasi ya kichwa ndiyo inayoondoa uhai haraka, lakini chagua mwenyewe.”
“Huyo jamaa alikuwa anafananaje?” nikamuuliza kwa shauku yenye hofu.
Akainyoosha bastola kuelekea kichwa changu.

“Huna haja ya kumhofia,” akasema, na kulikuwa na sauti ya kikatili. “Jihurumie mwenyewe.”
“Dola mia tano hazitoshi. Ninaweza kukuongezea hizo,” nikamwambia. “Unaonaje ukiiweka bastola hiyo pembeni name nikupatie dola elfu moja?”
Akanibeua.
“Ninapoweka mkataba, lazima niutekeleze,” akasema.
Simu ikaita ghafla.
Kwa sekunde ishirini zilizopita nilikuwa najipongeza mwenyewe. Kengele ya simu ikamshtua na akageuka kuitazama simu.
Nikamrukia pale pale, kichwa change kikilenga uso wake, mikono ikiifuata bastola.
Nilimtwanga kama roketi: kichwa change kikampasua mdomo na pua. Mikono yangu ikaifikia bastola, nikaipiga ikageukia pembeni huku ikifyatuka na kutoa mlio hafifu. Mikono yake ilikuwa imara mno.
Yeye na mimi na kiti tukaangukia nyuma kwa kishindo kikubwa.
Lakini alikuwa ngangari kweli kweli. Sikuweza kuichukua bastola mkononi mwake. Kidogo alionekana kushangazwa na kilichotokea, vinginevyo angenipiga risasi, lakini nilifanya haraka kumlalia na kumtwanga shingoni kwa karate kali iliyomlegeza. Mkono ukalegea na nikaichukua bastola. Kisha akanipiga katikati ya macho kwa ngumi nzito ambayo sijapata kukutana nayo maishani. Ilikuwa nzito kama nyundo.
Nikaiachia bastola. Kwa sekunde chache nilichoweza kukiona ni nyota zikicheza mbele yangu. Nilikuwa natambaa kwa magoti wakati naye akihangaika kuinuka kutoka sakafuni, damu ikivuja kutoka puani na mdomoni. Alirusha teke usoni mwangu, lakini halikuwa na nguvu. Nilikuwa nimemuumiza, na chokoraa kama huyu akiumizwa, anaumizwa hasa.
Nikalipangua teke hilo kwa mkono wangu, nikabingirika kutoka kwake na kusimama. Tukatazamana. Bastola ilikuwa sakafuni katikati yetu.
Aliniungurumia, lakini alikuwa mjanja kwa sababu hakuinama kuchukua bastola. Alijua nitamfinyanga kabla hajaifikia: badala yake akaja kasi kama nyati aliyejeruhiwa. Nilimtandika ngumi moja nzito usoni wakati akinivamia na sote tukadondoka chini na kudondosha makopo mawili ya rangi ya Rome ambayo nilikuwa nimeyaleta nyumbani kama kumbukumbu wakati nikiwa katika kazi moja.
Nilimtwanga kichwa usoni mwake tena na kumtandika ngumi sita za nguvu tumboni, huku nami nikipigwa ngumi mbili kichwani zilizofanya ubongo wangu uzubae kidogo. Akarudi nyuma. Ngumi mbili za tumboni zilikuwa zimemlainisha. Alionekana mnyama sasa. Nikamrukia, nikamtwanga tena. Aliyumba upande na nikaona amesehika kisu mkononi.
Tukatulia tukitazamana. Alikuwa ametepeta. Kichwa change kilikuwa kimeuharibu uso wake na damu zilimvuja mno, lakini bado alikuwa na nia ya kuua. Mtazamo wa macho yake na kisu mkononi vilinitisha.
Nikarudi nyuma.
Aliunguruma na kunijia kwa kasi ya ajabu.
Bega langu likagonga ukuta. Nilifua koti langu haraka na kwa kasi nikajifunga kwenye mkono wa kushoto. Alinijia kwa kasi kama nyoka anayetaka kugonga. Nilikishika kisu kwa kutumia mkono wenye koti na kumtandika ngumi shavuni kwa mkono wa kulia. Ilikuwa ngumi nzuri, yenye nguvu na madhara. Rangi nyeupe kwenye macho yake ilionekana na akarudi nyuma, akipiga magoti. Kisu kikadondoka mkononi mwake. Nikakipiga teke kikaenda upande mwingine wa sebule, halafu nilipojiweka sawa, akaanza kuangukia mbele. Nikamtandika ngumi nyingine shavuni iliyonichubua. Akadondoka chini kama gunia la pamba, akigonga kidevu chake sakafuni.
Nikaegemea ukuta, nikitweta. Nilikuwa nimechoka balaa. Nilitandikwa ngumi nzito ambazo sijawahi kupigwa na zilikuwa zimeniachia maumivu makali. Ilikuwa kana kwamba baadhi ya maisha yangu yalikuwa yameondoka mwilini.
Mlango ukafunguliwa na polisi wawili wakaingia, bunduki mikononi.
Huwezi kuanzisha aina hii ya vita chumbani mwangu bila kuwashtua wapangaji wote kwenye ghorofa hili.
Wakati wanaingia, Yule chokoraa alitambaa kiubavu. Alikuwa amedondokea kwenye bastola yake na sasa ilikuwa mkononi. Alikuwa bado anataka apate malipo yake ya kazi. Alifyatua risasi moja kwangu na nikahisi kitu kimepita usoni shaaa kabla ya kutoboa ukuta, na kudondosha udongo.
Polisi mmoja alifyatua risasi. Nilipiga kelele, lakini nilikuwa nimechelewa.
Kijana yule akafa, akiwa anajaribu kufyatua risasi nyingine kwangu. Alikuwa na ujasiri wa ajabu.
Itaendelea kesho…