RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (20)
Niliikumbuka bastola yangu ambayo ilikuwa makao makuu ya polisi. Nilikuwa naingiwa na mshtuko, lakini ningekuwa najiona salama kama ningekuwa na bastola yangu.
“Unafanya nini hapa?” nikathubutu kusema kwa ukali kidogo.

“Tulia, Buster: chuchumaa. Nina biashara ninataka kufanya na wewe.” Akanielekeza kwenye kiti. Nikaona kwamba alikuwa amevaa glavu nyeusi za pamba na hiyo ikanifanya nitokwe na jasho. Nilijua chokoraa huyu alikuwa muuaji na angenidhuru. Alikuwa anajiamini kupita kiasi: sana, alijiamini sana. Nikamtazama kwa karibu, mboni za macho yake zilionyesha ukatili wa dhahiri. Mamcho yake yalifichika kutokana na kofia yake.
“Ninakupa sekunde mbili kuondoka hapa kabla sijakutupa nje,” nilisema, nikiilazimisha sauti yangu iwe ya ukali.
Akabeua midomo yake, akiisugua ncha ya pua yake. Alikunjua miguu yake na gazeti likadondoka chini. Nikaiona bastola aina ya .45 ikiwa mapajani mwake. Ilikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti kilichotengenezwa kienyeji tu.
“Chuchuma, Buster,” akasema. “najua huna bastola.” Akaigusa bastola yake. “Haina sauti hii. Nimetengeneza kiwambo hiki mimi mwenyewe. Kinaweza kudumu kwa risasi tatu, lakini moja inatosha.”
Nikamtazama naye akanitazama, halafu kwa hadhari, nikaketi, nikimtazama. Kulikuwa na umbali wa futi sita tu kati yetu. Kutoka hapa nilipoketi niliweza kuisikia harufu yake. Alinuka uvundo, jasho na bangi.
“Unataka nini?” nikamuuliza.
“Umechoka kuishi, Buster?” akauliza, akijiweka sawa kwenye kiti kuubalance mwili wake mkubwa. “Nadhani umechoka kuishi. Huna muda mrefu wa kuishi.”
Kwa kuangalia macho hayo makatili na uso usio na chembe ya masikhara nilipata hofu kubwa.
“Nayapenda maishaI,” nikasema kwa nia tu ya kusema jambo lolote. “Ninaishi vizuri tu.”
“Mbaya sana.” Akaiweka sawa bastola hivyo kiwambo kikawa kinanitazama. “Unaye msichana?”
“Wapo kadhaa—kwa nini?”
“Nilikuwa najiuliza tu. Watasikitika watakaposikia umeuawa?”
“Mmoja au wawili watasikitika. Tazama, haya ni mazungumzo ya kipuuzi. Nini unachotaka kutoka kwangu? Nimekufanya nini?”
“Hakuna kitu, Buster.” Midomo yake myembamba ikajikunja kutengeneza tabasamu la kejeli. “Unaonekana ni mtu mwema sana. Una mahali pazuri pa kuishi. Nimekuona wakati unaingia. Una gari zuri.”
Nikavuta pumzi ndefu na kuzishusha.
“Unaonaje ukiweka kando bastola na tuzungumze kama marafiki,” nilisema bila matumaini ya kutosha. “Unaonaje kuhusu kinywaji?”
“Mimi sinywagi.”
“Hongera zako. Kuna nyakati ambazo hutamani nisinywe. Nahitaji kupata kinyaji sasa hivi. Je, hiyo haitakukwaza?”
Akatikisa kichwa.
“Hii siyo sherehe ya kunywa.”
Wakati mazungumzo haya ya kipuuzi yakiendelea, ubongo wangu ulikuwa kazini. Alikuwa mkubwa na mwenye nguvu. Kana isingekuwa bastola aliyonayo, ningekuwa tayari kukabiliana naye. Mimi si dhaifu kiasi hicho na nimejifunza mbinu kadhaa za kuwadhibiti watu wa aina yake wenye maumbile makubwa na nguvu nyingi. Nilikuwa katika umbali wa futi sita kutoka alipoketi. Ningeruka mara moja tu ningekuwa sawa naye kama si bastola aliyoishika.
“Ni sherehe ya aina gani sasa hii?” nikamuuliza, nikisogeza mguu wangu wa kulia ambao sasa ulikuwa nyuma ya mguu wa mbele wa kiti changu. Kwa staili hiyo nilikuwa na uwezo wa kujikunja na kuruka kumkabili kama ningepata nafasi.
“Sherehe ya kifo, Buster,” alisema kwa dharau.
“Nani anayeuawa?”
“Wewe, Buster.”
Nikatamani nisiwe natoka jasho namna hii. Ilinichanganya na kunisumbua. Nimewahi kuwa katika hatari hapo kabla, lakini si hatari kama iliyokuwa mbele yangu. Nilitamani nisijisikie mwoga. “Lakini kwa nini? Yote haya ni kwa nini?”
Aliinua bastola yake na kuanza kulikuna tundu mahali ambapo sikio lilipaswa kuwepo akitumia mtutu wake.
“Sielewi. Wala sijali,” alisema. “Mimi ninatengeneza fedha kidogo tu kirahisi.”
Nikailamba midomo yangu. Ulimi wangu ulikuwa mkavu kwahiyo ilikuwa ni kazi bure.
“Unalipwa kuniua mimi? Au siyo?”
Akainamisha kichwa chake upande mmoja.
“Kwa nini, ndiyo, Buster. Unadhani kwa nini ninataka kukuua?”
“Hebu nieleze,” nikasema kwa sauti ya mashaka. “Tuna muda wa kutosha. Nani anayekulipa ili uniue?”
Akapandisha mabega yake.
“Hata simuelewi, Buster. Nilikuwa nacheza pool wakati huyu jamaa alipokuja na kuniuliza kama ninaweza kufanya kazi itakayonipatia dola mia tano haraka. Tukasimama pembeni na akanipatia dola mia na kuniambia nije hapa kukutwanga risasi. Nikikamilisha kazi hiyo atanipatia dola mia nne zilizobaki. Kwa hiyo ndiyo maana nipo.”
“Huyo jamaa ni nani?”
Itaendelea kesho…