RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (19)
Akafungua mlango wa gari na kuingia. Akaingia haraka na kwa nguo alizovaa, hata magoti hayakuonekana. Aliufunga mlango haraka kabla hata sijaugusa.
“Usiku mwema, Bwana Ryan,” alisema, na akawasha gari, akaendesha na kuondoka eneo hilo.

Niliitazama gari hadi ilipotokomea, halafu nikatazama saa yangu. Ilikuwa saa mbili na dakika thelathini na tano. Ningependa anipe kampani kwa chakula cha usiku. Usiku huo ukawa mrefu kwangu: mtupu na uliodumaa. Nilisimama kwenye maegesho na kuanza kuwafikiria kati ya wasichana wanne au watano niliowafahamu ambaye angeweza kuja kupata chakula cha usiku na mimi, lakini hakuna hata mmoja aliyemfikia Bi. West: hakuna hata mmoja ambaye angenipa wakati mzuri usiku huu kwahiyo nikaamua kwenda kununua sandwich nyingine na kurudi nyumbani kuangalia televisheni.
Nilifikiria Jay Wayde angesemaje kama angejua nilikuwa na mpango wa kuwa na Bi. West jioni ya leo. Kwa vyovyote vile angeshtuka na kutahayari. Angetegemea nitakuwa mahali nikizungumza kwa ukali na mrembo huyu au tukivutana na mrembo mwingine.
Nikaingia kwenye mgahawa. Muziki kutoka kwenye juke-box ulikuwa ukipigwa. Wasichana wawili waliovalia jeans na visweta vya kubana waliketi kwenye stuli katika baa, makalio yao yalionekana na mvuto, nywele zao zilisukwa katika staili ya Bardot, vidole vyao vikiwa na kucha ndefu.
Wakanitazama wakati ninaingia, macho yao makavu ya ujana yakaanza kunisawiri, halafu wakatazama pembeni. Waliona kama mzee, sina swagger wala mvuto.
Nilikula nyama na sandwich, nikionekana mwenye mawazo. Hata kwenda  Hong Kong asubuhi hakukuonyesha furaha yoyote. Nikachukua picha za Herman na Jo-An na kuziangalia kwa makini. Walinekana wako tofauti mno. Mwanamume ndiye aliyenitisha. Sikuweza kuelewa ni kwa nini msichana kama Jane West siyo tu kwamba alizama kwenye penzi bali alimzalia na mtoto.
Nikaachana nao na kuziweka picha mfukoni. Baada ya kulipia sandwich, nikaingia mitaani, nikitambua kwamba wasichana wale wawili walikuwa wanaendelea kunitazama. Mmoja wao akacheka kimbeya. Pengine aliona ninachekesha. Kuna nyakati ninaponyoa ndevu huwa najifikiria hivyo pia.
Nikaendesha hadi nyumbani kwangu, kwenye vyumba vya ghorofani, ambapo kulikuwa na sebule kubwa, chumba kidogo cha kulala na jiko dogo tu. Nimeishi hapo tangu nilipoingia jijini Pasadena. Ilikuwa ni katikati, gharama nafuu na mahali tulivu. Hakukuwa na lifti, lakini sikujali kabisa. Kupandisha ngazi za ghorofa tano kuliufanya mwili wangu uwe mkakamavu na ulimfanya adui yeyote akae mbali pindi tunapokabiliana kwa sababu ya wepesi wangu na mapigo matakatifu.
Nilikuwa ninahema kidogo wakati nilipoufikia mlango wangu. Wakati nikihangaika na ufunguo, nikajiambia kwamba inabidi nipunguze sigara, lakini nilikuwa najidanganya.
Niliufungua mlango na kuingia sebuleni. Sikumuona mpaka nilipokuwa nimeufunga mlango. Mwanga ulikuwa mdogo: kulikuwa na kiza kidogo na yeye alikuwa amevaa nguo nyeusi.
Kulikuwa na bango la tangazo mtaani ambalo mwanga wake wa buluu, kijani na mwekundu ulimulika dari yangu. Kama isingekuwa kwa bango hilo, wala nisingemuona kabisa.
Alikuwa ameketi kwenye kiti changu nilichokipendelea ambacho alikisogeza karibu na dirisha. Aliketi akiwa amekunja miguu yake, mikono yake ikiwa kwenye gazeti lililokunjwa mapajani na alitulia kabisa.
Kwa hakika alinipa mshtuko ambao ulifanya moyo wangu upoteze mapigo.
Swichi ya kuwashia taa ilikuwa jirani yangu. Nikaiwasha.
Alikuwa ni kijana mdogo tu: kama umri wa miaka kumi na nane au kumi ta tisa hivi, lakini mwenye umbile lenye nguvu na kifua kipana. Alivalia jaketi jeusi, kofia nyeusi na skafu chafu nyekundu, suruali aina ya corduroy nyeusi na kitambaa cheusi alichojifunga shingoni mwake.
Ni aina ya vijana ambao utawaona wakati wowote usiku wakiwa nje ya baa: uzao wa watoto wa mitaani: katili kama panya buku.
Ngozi yake ilikuwa chafu. Macho yake yalikuwa ya kikatili kama ya mvuta bangi na muuaji. Sikio lake la kulia lilikuwa limekatika na alikuwa na alama ya jeraha kubwa iliyotokana na kisu kwenye taya lake. Alikuwa ni miongoni mwa viumbe hatari ambao nimewahi kukutana nao.
Kwa kweli alinitisha mno.
Akanitazama kwa dharau na tabasamu la kejeli.
“Hallo, Buster, nilidhani huwezi kurudi kabisa,” alisema katika sauti ya jeuri inayokwaruza.
Itaendelea kesho…