Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG (18)




Majira ya saa kumi na mbili, nilifunga ofisi yangu na kurudi nyumbani. Nilipanga nguo kwenye begi langu: nikafanya mambo ya muhimu ambayo mtu anayesafiri kwa wiki kadhaa anapaswa kuyafanya, nikaoga, nikanyoa ndevu, nikavaa shati maridadi, kisha nikaendesha kuelekea Astor Bar, ambapo niliwasili saa mbili kasoro dakika tano.

Janet West aliwasili wakati mshale wa saa yangu ulipogonga saa mbili kamili. Aliingia akiwa na muonekano ule ule wa kujiamini akiwa amevaa maridadi, mwanamke mwenye sura jamali ambaye anafahamu jinsi anavyopendeza na anajivunia kwa jilo.
Vichwa vywa wanaume vikageuka kumtazama wakati akielekea kwenye meza ya pembeni nilikokuwa nimeketi. Tulizungumza mambo ya kawaida kama wageni waungwana wanavyoweza kuzungumza wanapokutana na nikamuagizia vodka martini wakati mimi nikinywa Scotch.
Akanipatia tiketi ya ndege na pochi ya ngozi.
“Nimekuwekea dola kadhaa za Hong Kong zikusaidie,” alisema. “Itaepusha usumbufu wakati utakapotua. Ungependa nipige simu wakuandalie chumba? Hoteli ya Peninsular au Mirama ni nzuri sana.”
“Asante, nitapenda kufikia hoteli ya Celestial Empire.”
Akaonyesha mshtuko wa haraka huku akisema, “Sawa, hakuna shaka.”
“Umekumbuka picha?”
Wakati mhudumu alipoweka vinywaji, alifungua mkoba wake wa ngozi ya kenge na kunipatia bahasha.
Picha ilionekana ilipigwa na mtaalam hasa. Mtu aliyepigwa alionekana alikuwa akiitazama kamera. Kulikuwa na tabasamu dogo, la kejeli kwenye macho yake: haukuwa uso unaovutia. Mweusi, na nyusi nyeusi, uso mpana, taya pana zilizopanuka, na mdomo mdogo. Ulikuwa ni uso ambao ungeweza kukutana nao katika orodha ya polisi ya wahalifu.
Nilishangaa. Sikutegemea Herman Jefferson angekuwa na sura ya aina hiyo. Nilikuwa nafikiria kwamba angekuwa na uso mtanashaji, usio na makuu, na ule unaowapagawisha mabinti. Mtu huyu angefanya lolote ambalo lingekuwa la hatari, na angelifanya vizuri kabisa.
Nikakumbuka ambacho aliniambia kuhusu Herman. Alikuwa mbaya na katili. Hakuwa na muonekano wa kufurahisha. Kwa kuangalia uso wa mtu huyu, nilikubaliana na maelezo yake.
Nikamtazama. Alikuwa akiniangalia: uso wake ukiwa hauna maelezo yoyote, lakini macho yake yalikuwa baridi.
“Nimeona unachomaanisha,” nikamwambia. “Hafanani kabisa na baba yake, au siyo?”
Hakusema chochote bali akaendelea kuniangalia wakati nikiiweka picha hiyo kwenye pochi yangu. Nilipata wazo la ghafla bila sababu zozote na kuitoa picha ya Jo-An.
“Uliniuliza kama (mwanamke) alikuwa mzuri,” nikamwambia. “Huyu hapa,” nikampatia ile picha.
Kwa muda mrefu hakuweza kuichukua. Pengine mwanga ulikuwa unahadaa, lakini niligundua kwamba alikuwa amebadilika rangi. Mkono wake ulikuwa imara wakati alipoichukua picha hiyo. Ilikuwa zamu yangu sasa kumtazama wakati akiichunguza picha hiyo. Aliitazama kwa muda mrefu, uso wake ukiwa hauonyeshi lolote. Sikujua nini kilichokuwa kinaendelea mawazoni mwake. Baadaye akanirejeshea picha hiyo.
“Ndiyo,” alisema, sauti yake ikiwa baridi na ya mkato.
Nilichukua glasi yangu naye akachukua yake. Tukanywa.
“Umesema maziko ni kesho?” nikamuuliza.
“Ndiyo.”
“Rafiki wa Herman aliniomba niulize muda na kama anaruhusiwa kuhudhuria. Ofisi yake iko jirani na yangu. Anaitwa Jay Wayde. Alisoma pamoja na Herman.”
Akaganda kwa muda.
“Ni Mzee Jefferson na mimi tu ndio tunaohudhuria,” alisema. “Hakuna rafiki hata mmoja wa Herman anayeruhusiwa.”
“Nitamweleza. Alitaka kuagiza maua.”
“Hakutakuwa na maua yoyote.” Aliiangalia saa yake, akainuka. “Mzee Jefferson ananisubiri. Ni lazima niondoke. Kuna chochote ninachoweza kukufanyia?”
Hata vinywaji vyenyewe tulikuwa hatujanywa. Nilikuwa nimefadhaika sana. Nilitegemea ningeweza kumfahamu zaidi, lakini ilikuwa kama kuzungumza na mtu aliye kwenye ukuta wenye urefu wa futi tisa.
“Hapana, asante. Ndege inaondika saa ngapi?”
“Saa tano. Unatakiwa kufika uwanjani saa nne na nusu.”
“Asante kwa kuweka mipangilio sawa.” Alipoanza kulekea mlango wa kutokea, kwa haraka nikazitumbukiza dola mbili kwa mhudumu na kumfuatilia mtaani.
Gari lake aina ya Jaguar lilikuwa limeegeshwa upande wa pili wa baa. Mimi nililazimika kuzunguka majengo mawili mara tatu kabla ya kupata maegesho takriban yadi mia moja kutoka hapo. Hiyo ilionyesha ni kwa jinsi gani yeye au Mzee Jefferson alivyo na nguvu kwenye jiji hili.
Alitulia kidogo kwenye gari.
“Nakutakia safari yenye mafanikio,” alisema. Hakukuwa na tabasamu. Macho yake yalionyesha kwamba alikuwa mbali sana. “Kama kuna lolote ambalo ninaweza kulifanya kwa ajili yako au unalihitaji kabla ya kuondoka, tafadhali nipigie.”
“Tafadhali kuwa na amani, huwezi kutulia?” nikamuuliza, nikitabasamu. “Huwa hupati muda wa ziada kupumzika na kutokuwa sekretari makini?”
Kwa kitambo kifupi kulikuwa na mshangao machoni kwake, lakini ghafla ukaondoka.
Itaendelea kesho…

Comments