PROF. MAGHEMBE - NI MARUFUKU KUSAFIRISHA MKAA KUTOKA WILAYA MOJA KWENDA NYINGINE

NA HAMZA TEMBA - WMU
...................................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametangaza mabadiliko makubwa katika biashara ya mkaa nchini na kusema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu hakuna mkaa wowote utakaosafirishwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine ili kunusuru misitu inayoteketea kwa kasi hapa nchini.

Amesema hayo leo wakati akifungua mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka kwenye Idara, Vitengo na Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hiyo.

“Kuanzia mwezi Julai hakuna ruhusa ya kutoa vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya kwa ajili ya matumizi ya watanzania wanaohitaji nishati ya mkaa, lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar marufuku.

“Wamekata misitu yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwasababu watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu, Tanzania jamani sio shamba la bibi, wale wote watakaotoa mkaa kutoka eneo moja hadi jingine kinyume na sheria hii watashuulikiwa kwa utaratibu wa uhujumu uchumi”, amesema Maghembe.

Amesema kuwa kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa vibali maalumu katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Amesema mkaa huo hautakuwa na athari nyingi za kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.

Wakati huo huo, Waziri Maghembe amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kumuhamisha kituo cha kazi Mkuu wa Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu wa Wakala hiyo, Arjason Mloge kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo kwenda chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo mkoani Kilimanjaro na badala yake atafutwe mtu mwingine muaminifu.

Amesema uamuzi huo ni kufuatia udhaifu uliojitokeza katika usafirishaji wa rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi ikiwemo usafirishaji kwa kutumia nakala za vibali ambazo sio halisi, yaani “Photocopies”. “Agizo hili litekelezwe mara moja kabla ya saa sita mchana wa leo na niwe nimepewa nakala ya barua hiyo ya uhamisho” amesema.

Kufuatia uamuzi huo amepiga marufuku kuanzia leo usafirishaji wa mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi (Photocopies). Ameongeza kuwa katika kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda ya Serikali ya awamu ya tano hakuna gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Wawekezaji wanahimizwa kujenga viwanda vya kuchakata magogo hayo hapa nchini ili kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kutoa faida halisi inayotokana na rasilimali hizo kwenye uchumi wa taifa”, amesema.

Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 sehemu ya 21 (1) hairuhusiwi kabisha kuchunga mifugo katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Misitu. Amewataka watumishi wa Maliasili kusimamia Sheria hiyo pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuifuata kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Waziri Maghembe amewataka majangili wote nchini kuachana na biashara hiyo haramu ambayo hailipi kwa sasa na badala yake wachukue matrekta wakalime.

“Mtu ambaye alikuwa anaishi kwa kutegemea ujangili sasa atafute trekta akalime, kwa sababu akifanya ujangili tukamkamata tu, na tukimkamata atakaa kwenye hoteli ya mkuu wa magereza (magereza) kwa zaidi ya miaka 25”.

Aidha, Waziri Maghembe ametoa pongezi kwa watumishi wote wa Wizara ya Maliasili kwa kazi nzuri wanayofanya ya kupambana na ujangili nchini pamoja na ulinzi wa maliasili za taifa (Misitu, Wanyamapori na Mambo ya Kale) ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 20.5 kwenye pato la taifa. Amesema matokeo chanya ya kupambana na ujangili yameanza kuonekana japo ujangili bado upo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki amemueleza Waziri Maghembe kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yamepokelewa kwa ajili ya kuyafanyiwa kazi, huku Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa akimueleza Waziri huyo kuwa watalinda na kusimamia Malisili za Taifa na kwamba katu hawapo tayari kuandikwa kwenye vitabu kuwa walishiriki katika kutoweka kwa maliasili hizo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo terehe 10 Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Esther Malima. 
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati waliokaa) na wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo baada ya kufungua mkutano huo leo terehe 10 Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika leo terehe 10 Aprili, 2017 katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati) akiimba wimbo wa Umoja wa Wafanyakazi (Solidarity Forever) muda mfupi kabla ya kufunga mkutano huo leo terehe 10 Aprili, 2017 pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Baraza hilo, Esther Malima (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Mrimia Mchomvu.

 Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (wa pili kshoto) akizungumza katika mkutano huo leo terehe 10 Aprili, 2017.
 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa baraza hilo kutoka kwa Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe (hayuko pichani) katika ukumbi wa LAPF mjini Dodoma leo. 
 Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
 Baadhi ya wajumbe na wageni waalikwa katika mkutano huo.
 Baadhi ya wajumbe katika mkutano huo.
 Baadhi ya wajumbe na wageni waalikwa katika mkutano huo.
 Baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
 Baadhi ya wajumbe Sekretarieti wakiteta jambo nje ya ukumbi.