- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mwandishi
wa makala haya, Bwana Daniel Mbega, akiwa na mganga wa jadi huko Kachwamba,
wilayani Chato. (Picha zote na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini)
Mwandishi
wa makala haya, Daniel Mbega, akiwa na mtoto Margreth Hamisi (6) mkazi wa Kona
Nne, Kijiji cha Mwakashanhala wilayani Nzega, baada ya kuokolewa na wanausalama
wakati akitaka kuuzwa mzima mzima na mjomba wake.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
Kahama: SHABAN
Kapulwa (siyo jina lake halisi) ni mganga wa jadi ambaye anajivunia ‘nguvu’ za
tiba zake asilia zilizomwezesha kukutana na watu wengi – wanasiasa kwa
wafanyabiashara – na ‘kuwasaidia’ kwenye mambo yao.
Anaishi katika eneo la Nyihogo kwenye Halmashauri ya Mji wa
Kahama, na siku zote anategemea uganga kuendesha maisha yake.
Zaidi anaheshimika na wakazi wa eneo hili kwa sababu ni ‘mfumu’ (mganga) na kila unapofika kwake
utashangaa kukuta watu wengi wakisubiri huduma.
Shaban anaishi kwenye nyumba nzuri ya kisasa na nje
ameegesha gari dogo aina ya Toyota Verossa, ambalo anasema alipewa zawadi na
mwanasiasa mmoja (hamtaji jina) baada ya ‘kumsaidia kupata ubunge’ katika
mojawapo ya majimbo ya Kanda ya Ziwa.
“Wanakuja, wengi tu – wanasiasa, wafanyabiashara, maofisa
wakubwa wa serikali na wengine – wanataka dawa ili ama wapate madaraka makubwa
au mafanikio katika biashara zao, wengine ukiwatazama tu unaona wamevurugwa na
maisha, wamejikati tamaa wenyewe, ninawasikiliza na kuwasaidia kwa kadili ya
utashi wao,” Shaban anamweleza mwandishi wa MaendeleoVijijini.
Japokuwa anaishi kwenye nyumba nzuri, lakini mazungumzo na
mwandishi wa makala haya yanafanyika kwenye kibanda maalum cha msonge
kilichosilibwa kwa udongo na kuezekwa nyasi (Wasukuma wanasema ‘Kizimba’),
ambacho ndicho hutumika kwa tiba zake.
Sakafu ya udongo imetandikwa mkeka mzuri ambao nao anasema
aliletewa na mfanyabiashara mmoja kutoka Arabuni.
Kizimba hiki kimejaa harufu nzito inayotokana na kuchomwa
kwa udi na ubani inayomfanya mwandishi apige chafya mara kadhaa.
Kizimba kimejaa pembe na tunguli nyingi pamoja na mikoba ya
ngozi za wanyama wa kila aina.
“Wateja wengi wanakuja na matatizo mengine nje ya tiba kama
kutaka madaraka, mafanikio katika kazi na biashara, ninawatibu kwa saikolojia
tu kwa sababu hakuna dawa inayoweza kukupatia utajiri na madaraka, labda kwa
njia za kichawi, ambao mimi siyo muumini wake,” anasema.
Shaban ameiambia
MaendeleoVijijini
kuwa, kutokana na ujinga na imani za kishirikina zilizotanda kwa jamii na
kuamini kila linalosemwa na waganga, ndiyo maana wamekuwa wakifanya mambo
magumu yanayokwenda kinyume hata katika jamii.
“Waganga
tumaaminika sana, na ninakuhakikisha, mganga akikwambia kalete mfupa wa Mwalimu
Nyerere ili ufanikiwe maishani, hata kama kaburi lile linalindwa, unaweza
kwenda kulivunja bila kujali athari utakazozipata, kwa kuwa tu umeaminishwa
ujinga,” anasema.
Anaongeza:
“Ukisikia mganga anakwambia kaleta ‘mweso wa kanyerere’ – yaani moyo wa
sisimizi – basi ogopa sana. Maana yake unatakiwa kwenye kuleta moyo wa mtu, na
ili uupate ni lazima umuue… tangu lini moyo wa sisimizi ukaonekana?”
Karatasi hii ilikutwa kwa mganga mmoja akiwa amemwandalia mteja wake maelekezo (Chiranduzi) ya vitu vinavyohitaji, ikiwemo kumtaka akalete 'moyo wa sisimizi' akiwa na maana ya kuua mtu.
Migeka
Mihagwa Masakilija (58) ni mganga wa jadi, mkazi wa Kachwamba, wilayani Chato
katika Mkoa wa Geita, ambaye ameiambia MaendeleoVijijini
kwamba, watu wametengenezwa ujinga wanaukubali na ndiyo maana matukio ya mauji
ya vikongwe na albino yameongezeka nchini Tanzania na hata Afrika Mashariki na
Kati.
Pichani inaonekana kipande cha ngozi ya na 'goroli' la Simba pamoja na simbi ambazo kwa mujibu wa mganga mmoja wa Kachwamba wilayani Chato, ikichanganywa na 'shingila' nyingine, inaweza kufanya mambo mengi. (Picha zote na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini)
Hata
hivyo, anafafanua kuwa kuna makundi manne yanayohusiana na uganga ambayo ni
wauaji (wakiwemo wakata mapanga), mawakala wa shingila (vichanganyio vya dawa), waganga walozi na waganga tiba.
Migeka
anasema: “Kundi la wauaji, ambalo linahusisha waganga matapeli wanaomiliki mitandao
ya wakata mapanga kazi yao kubwa ni kuua labda albino, kutafuta viungo vya
vichaa, viungo vya uzazi vya binadamu, mafuta ya binadamu, mafuta ya nyoka au
simba, mifupa ya watu maarufu – hata ya Mwalimu Nyerere – kama hakuna ulinzi
wanavunja lile kaburi. Hawa wanaweza kuteka nyara, wakakunyonga, wakakubanika
porini na kuchuja mafuta. Ndio wanaokwiba albino na kuchukua viungo. Wanaweza
kuwa na mifupa ya bundi, mbwa na takataka zote,” anasema.
Kuhusu mawakala wa shingila, Migeka anasema, hilo ni kundi muhimu katika masuala ya
uganga, kwani wakala huyo ndiye anayewasambazia waganga mahitaji yote.
Mifupa, pembe na vitu mbalimbali vinavyotumika kama 'shingila' baada ya kukamatwa nyumbani kwa mganga mmoja wa jadi huko Bariadi.
Hawa ni nyoka waliokaushwa ambao wanausalama walimkamata mganga mmoja wa Kilyamatundu, Sumbawanga mkoani Rukwa akiwa nao.
“Kama mganga yeyote anahitaji kazi fulani
ifanyike anamtafuta huyu wakala, ambaye naye anawasiliana na kundi la wauaji
ambao ndio wanaomletea viungo hivyo,” anasema na kusisitiza kwamba kuna mtandao
mkubwa kiasi kwamba kuuvunja ni shida.
MaendeleoVijijini imebaini kwamba, waganga
walozi hawajishughulishi na tiba bali hutafuta shingila kwa ajili ya kufanya kafara, hata ya kuua mtu.
“Hawa kazi yao ni makafara na kuloga watu,
unamwendea na kumwambia fulani amekutenda hivi na vile, yeye anakuuliza
‘unataka huyu tumfanye nini’, utakavyomwambia ndivyo atakavyofanya,” anasema
Migeka.
Anaongeza; “Waganga wa tiba ni sisi ambao tunatibu
watu waliologwa na waganga walozi.”
Imani kwa waganga
Mganga
Maria Masweduki, mkazi wa Buzirayombo wilayani Chato akiwa 'amepandisha
maruhani' kumpigia ramli mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)
baada ya kulipa Shs. 2,000 inayoonekana hapo.
Kwanini wanaheshimika?
Na tiba za kisaikolojia zikoje? Ni kweli zinasaidia kuwapatia watu madaraka na
utajiri?
Kabla ya Shaaban
Kapula kujibu maswali hayo, anatabasamu.
“Nilitegemea
utaniuliza hivyo. Ngoja nikwambie, kwanza jamii za Wasukuma wanaamini sana
masuala ya kishirikina. Hawawezi kufanya jambo lolote mpaka wakamuulize ‘mfumu’, na atakachowaeleza, hata kama
ni uongo, ndicho watakachoamini.
“Ninaheshimika
hapa kwa sababu mtandao wangu ni mkubwa kuliko waganga wenzangu, watu wanaona
magari ya kifahari yanakuja kila wakati, wanaamini mimi ni kiboko ndiyo maana
nina wateja wengi. Wakija na matatizo yao, ninawasikiliza na ninapoona
yamesababishwa na mkanganyiko tu wa maisha, nawapa dawa za uongo na kweli,
lakini kikubwa masharti ninayowapa ndiyo dawa.
“Ninawashauri
tu kwamba ili dawa zangu zifanye kazi wakaongeze bidii kazini na lazima bosi
wake atampandisha cheo, kama ni mfanyabiashara namwambia apunguze matumizi ili
apate mafanikio, kama ni mwanasiasa namwambia akazungumze sera zinazolenga
kutatua matatizo ya wananchi na atomize ahadi zake.
“Sasa
niambie, katika masharti hayo ni yapi ambayo yanahitaji dawa kama siyo
kubadilisha fikra za mtu afanye yaliyo sahihi?” anahoji Shaaban. “Ukiongeza bidii
kiongozi wako ataona mabadiliko, wengine wanajichukia wenyewe tu na kudhani
kuna watu wabaya wanawaloga, hata mtaani wanakoishi.”
Kwa upande
wake, Lumisha Nhinde (46), mganga wa jadi wa Kijiji cha Buhekela wilayani Igunga
mkoani Tabora, ameiambia MaendeleoVijijini
kuwa, watu wametengenezewa ujinga tangu enzi na enzi ambao wanauamini.
“Kwa mfano,
kuna msemo wa ‘mganga hajigangi’, maana yake unaijua? Maana yake ni ujinga tu,
hata yeye anaweza kutegemea mganga mwingine. Eti ili aweze kupona ni lazima
amtafute mwingine… ina maana dawa zake hazifanyi kazi. Wanatumia lugha hiyo
kama kinga ili usimhoji. Kama mganga anaamini dawa zake zinaleta utajiri, kwa
nini asitengeneze akapata utajiri? Kwani yeye hataki kuwa tajiri?” anaeleza.
Aidha, ameithibitishia
MaendeleoVijijini
kuwa, ujinga huo wa watu kuamini kuwa ufumbuzi wa matatizo yao utapatikana kwa
waganga wa jadi umewakumba hata wasomi, ambao, anabainisha kwamba, kwa miaka ya
karibuni ndio wengi wanaoingia kwenye vizimba.
“Wasomi ni
wajinga sana, wanajifanya wamesoma na kutuona sisi si lolote, nasi hutumia
nafasi hiyo kuwakomoa,” anasema huku akininong’oneza: “Tena tunawakomoa zaidi kwa
kulala na wake zao wakati wao wanahangaika usiku kwenye njiapanda wakipiga
manyanga.”
“Nikimuona
mjanja kama wewe lakini aliyeingia kwangu kwa dharau, nitamwambia ili tiba
ifanye kazi, basi amlete mkewe kwani ndiye atakayetengeneza dawa.
“Nikiona
mkewe ‘analipa’, usiku wa manane nitawaambia twende njiapanda ambako yeye
atakuwa anaoga dawa za uongo na kweli, halafu nitabaki na mkewe na kumwambia
tulale kwa sababu ni sehemu ya tiba ya mumewe, hawezi kukataa na inakuwa ni
siri kubwa, hawasemi,” anasema na kuongeza kuwa kama mteja ni mwanamke, atamweleza
kwamba kulala naye ni sehemu ya tiba yake.
Utajiri wa kishirikina ukoje?
Bi. Prisca Mpesya akiwa na watoto wake wawili wenye albinism, Lucia aliyembeba na Baraka ambaye alikatwa kiganja cha mkono. Hapa alikuwa akimuuguza Baraka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Lakini Shaaban
Kapulwa anasema, katika uhalisia, hakuna utajiri wa kishirikina bali ni imani
potofu zilizopandikizwa katika fikra za jamii kuwa wakitumia dawa wanaweza
kufanikiwa.
“Huu ni
utapeli wa wazi wazi, lakini ukimwambia mteja ukweli kuwa hakuna dawa ya
utajiri haamini na atakuona wewe ni mbabaishaji, kwa sababu yeye amefunga
safari kutoka huko mpaka kwako akiamini wewe unaweza kumpa ‘zari’, hivyo
tunalazimika kukubaliana na matakwa yao na kutengeneza dawa za uongo na kweli
na kuwapa masharti magumu,” anasema.
MaendeleoVijijini ilitaka kujua kama kuna
ukweli kwamba albino ni dili? Lakini Shaaban anajibu haraka kuwa hakuna kitu
kama hicho.
“Ni
utapeli tu kwamba kalete kiungo hiki cha albino ili wapate kupiga hela. Ninachokuthibitishia
ni kwamba, albino siyo biashara ila watu wameaminishwa tu. Watu ni wepesi
kuamini uongo kuliko ukweli,” anasema.
Shaaban anasema,
siku za nyuma waliwahi kufanya kikao cha waganga na wananchi ili kuwahamasisha
watu waondokane na dhana hiyo kwa sababu wanafahamu wanaosababisha mauaji ya
vikongwe na albino ni waganga.
“Kwa
sababu mganga anakuwa tayari amemtapeli sana mteja hivyo anamtengenezea
mazingira ili akamatwe na kufungwa kwa sababu hakuna dawa yoyote ya utajiri
ambayo unaweza kumpatia,” anasema.
Hata hivyo,
anakanusha kuwepo kwa utajiri wa ‘manyoka’ ambao kwa muda mrefu umevuma katika
jamii, akisema hizo ni fikra potofu na utapeli ambao waganga wa jadi wanaufanya
kuwapumbaza watu.
“Hata wewe
unaweza kufuga nyoka ilimradi tu mtu akukamatie. Ukishamchukua kwanza inabidi
umtoe meno yote kwa kumsugua kwa gunzi la mahindi, halafu na wewe unatakiwa
kukata kucha zako zote za mikono na miguu,” anaelezea.
Ameieleza MaendeleoVijijini
kwamba, kwa kawaida, nyoka anapouma sumu yake inapitia kwenye meno, hivyo
ukiyasugua maana yake hatakuwa na uwezo wa kuuma, ingawa meno ya baadhi ya
nyoka huota tena.
“Kila
kucha zako zinavyokua ndivyo na meno yake yanakua, kwa hiyo unatakiwa kumsugua
meno yake kila mara ili uwe salama. Wale ambao unasikia wameumwa ama kuuawa na
nyoka wao huwa wanakosea masharti hayo.
“Ukishamfuga
nyoka, mganga atakupa masharti kwamba, fedha zote unazozipata kwenye biashara
yako ni lazima uzitumbukize kwenye chumba alimo nyoka na usizitumie ovyo
isipokuwa tu unapochukua kiasi cha kufungia bidhaa. Kwa kukuangalia tu ataona
udhaifu wako uko wapi – kama siyo mlevi wa pombe basi utakuwa mzinifu na
vinginevyo – kwahiyo nitakwambia achana na starehe na anasa zote, na usitoe
fedha ovyo kwa watu. Hebu niambie, baada ya mwaka mmoja, fedha hizi zitakuwa
kiasi gani?” anahoji.
Wateja wao akina nani?
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, ACP Joseph Konyo, akiweka mchanga kwenye kaburi la marehemu Yohana Bahati (1) wa Kijiji cha Ilyamchele wilayani Chato aliyetekwa na kuuwa, kisha kuondolewa mikono na miguu na watu wasiojulikana.
Kaburi la marehemu Yohana likijengewa.
“Mashehe
na wachungaji, waimbaji wa injili, wasanii, wanamichezo, na wasomi kwa ujumla ni
wateja wetu wakubwa. Kama kuna mtu mwelewa kwamba kuna utapeli kwenye uganga basi
siyo wengi, vinginevyo tunawapata sana,” anasema.
Anasema,
suala la kiimani katika ushirikina hata watu wa Mungu wapo, wanaamini na
wanakwenda kwa waganga kutafuta ‘nguvu’ za kukubalika kwa waumini wao.
Ameithibitishia
MaendeleoVijijini kwamba,
wakati viongozi hao wa dini wanapohubiri kuhusu uchawi na kuwaita waumini watoe
ushuhuda maana yake wanakiri nguvu kubwa ya ushirikina na wanawanadi waganga na
wachawi na kuzidi kuwatengenezea waumini ujinga mwingine.
“Labda
nikupe mfano hai, niliwahi kupata wachungaji, kuna mchungaji mmoja wa Mbeya na
mwingine wa Dar es Salaam. Huyu wa Dar es Salaam, tena mtu maarufu sana
anatokea Kanda ya Ziwa (jina linahifadhiwa), alikuja akiwa amepewa anuani
yangu, kwamba nikimtengenezea dawa atakuwa na uwezo kila atakaloongea watu
wamsikilize na atajaza waumini kanisani mwake.
“Nikamuendelezea
ujinga kwamba kila utakachoongea kinakubalika. Sikumpa dawa ya maana, nilimjenga
kisaikolojia tu kwamba azungumze vitu vinavyoilenga jamii, halafu akachinje
kuku, achukua dawa aichanganye na damu aoge halafu, ile itakayobaki amwage damu
barabarani.
“Hakuna
dawa yoyote kubwa, nilimpa ya kawaida tu kwa kumwaminisha kwamba yale maneno
atakayoyasema yawe na nguvu. Hakujua ni yale maneno tu ambayo anayazungumza
kulenga jamii ndiyo yanayomfanya akubalike katika jamii. Sasa amejipatia
umaarufu mkubwa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.”
Anasema,
kwa kiongozi wa dini kuambiwa atoe Shs. 500,000 hadi milioni moja ni jambo la
kawaida na wengi wanatapeliwa kila siku lakini hawawezi kusema hadharani.
Anawataja
baadhi ya viongozi wakuu wa dini wanaoheshimika (majina yanahifadhiwa) ambao wanaendesha
utapeli hadi makanisani kwa sababu ya ujinga wanaoaminishwa na waganga.
“Sisi waganga
tunawafundisha mazingaombwe, kwa mfano, kubadilisha maji kuwa soda, ni akili
tu. Zinachukuliwa Juice Cola za pakti. Zinatafutwa tissue za kawaida, zile
pakti zinapasuliwa kama mbili na kuwekwa kwenye tissue.
“Halafu
yanaletwa maji, anawaambia waumini fumbeni macho waombe. Wanapofumba macho yeye
anaingiza mkono kwenye maji huku akiufikicha na kukoroga akiendelea kuomba. Wakifumbua
tayari wanaona maji yamebadilika rangi, anawaambia ni kwa uwezo wa Mungu wakati
ni utapeli,” anasema.
Aidha,
anasema ingawa siyo vyema kupinga Neno la Mungu, lakini ni wajibu wake
kuielimisha jamii kuhusu baadhi ya madhehebu ambayo yanawapotosha watu kiimani
kwa kutumia miujiza ambayo ni viinimacho.
Shaaban
anasema, kwa kuwa kizazi cha sasa watu wanataka kuona miujiza ndipo waamini,
wametokea watu ambao wanazifanyia biashara dini kwa mazingaombwe.
“Nenda
kwenye kanisa ambalo kiongozi wake anajitangaza kufanya miujiza utaona. Kuna
matayarisho makubwa ambayo wanafanya wanapodai kuwaombea walemavu na watu kama
hao, kama wewe si mmojawao huwezi kuanguka kwa mapepo kwa sababu hukuandaliwa,”
anasema.
Anaongeza:
“Mchungaji mmoja (jina linahifadhiwa) aliwahi kuja pale Kigoma akawaandaa watu
ili kujifanya walemavu. Akawapanga kesho yake alipokwenda mkutanoni akasema leo
anaomba kwa ajili ya vipofu na vilema. Wale watu walioandaliwa walijipanga mle
ndani sehemu tofauti tofauti. Aliposema sasa naombea wasioweza kutembea, wale
waliopangwa wakajitokeza haraka.
“Wanapofika
idadi fulani anayoijua yeye kwamba ndio ‘watu wake’ anasema nitawaombea hawa tu
leo. Anaanza kuomba pale na wale wanadondosha magongo na kuanza kuruka ruka,
halafu mkutano wanashangaa kuona miujiza hiyo na kumwamini.”
Kufunga kipindi
Kitanga cha mkono wa mtoto Baraka Cosmas kikiwa kimeoza na kutoa funza baada ya kupatikana.
Sajenti Kalinga Malonji, mkazi wa Kijiji cha Hanseketwa wilayani Mbozi akiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa akiwa na kiganja cha mtoto Baraka Cosmas.
MaendeleoVijijini imegundua kuwa waganga
wana lugha maarufu wanayoitumia pale wanapoona wamekwisha mtapeli mtu fedha
nyingi na bado anawafuatilia.
“Huwa
tunasema ‘tunafunga kipindi’, yaani inabidi utafute namna ya kumpoteza kabisa
mtu huyo asikufuatilie kwa sababu ulichomwaminisha kuwa ni dawa ni uongo tu
hazifanyi kazi yoyote,” anasema Shaaban.
Anasema
baadhi ya viongozi wa dini wametapeliwa na waganga mpaka Shs. 50 milioni wanapohitaji
dawa na mvuto wa waumini makanisani mwao, lakini katu hawawezi kulalamika
hadharani kwa sababu jamii itawashangaa.
“Kama
hawajafanikiwa watarudi tena kwa waganga, na kwa kuwa hakuna dawa yoyote ya maana,
inabidi umuuzie kesi – wengine wanaambiwa wakafanye makafara kwa kutumia viungo
vya binadamu au wakazini na watoto wadogo huku wakidanganywa kuwa hakuna
atakayewaona baada ya kuogeshwa dawa, matokeo yake wanajikuta wamekamatwa na
kufungwa jela,” anasema na kuongeza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuepukana na
mteja wa aina hiyo kwani tayari amemlia fedha na mwendelezo wa kumdanganya
hana.
Jiandae kusoma kitabu maalum cha ‘MAUAJI YA ALBINO NJE-NDANI’
kinachotokana na uchunguzi wa kipelelezi wa mwandishi DANIEL MBEGA alioufanya
kwa miezi nane katika mikoa 10 ya Tanzania iliyokumbwa na matukio hayo, huku nyakati nyingine akihatarisha maisha yake usiku na mchana. Kitabu
hicho kina ripoti za ndani kabisa kuhusu namna mauaji hayo yanavyofanyika,
wahusika wakuu, mtandao hatari uliopo na unawahusisha akina nani, jinsi polisi
wanavyopeleleza kesi hizo, rushwa ndani ya mahakama za sheria ili kuwalinda wahalifu,
mambo yanayotokea kwa waganga wa kienyeji na mengi kadha wa kadha ambayo
hayakuwahi kuripotiwa hadharani.
Comments
Post a Comment