Featured Post

HAYA NI MAENEO 5 YANAYOKUMBWA NA MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAAM KILA MWAKA

Na Jumia Travel Tanzania

Kama sio mwenyeji wa jiji la Dar es Salaam basi ni vema ukauliza kwanza kabla ya kuhamia sehemu na kuanza kuishi. Usipofanya hivyo kwenye kipindi cha mvua kama hiki usishangae unaamka ukiwa umezungukwa na maji kama sio kuelea kabisa.

Kuwa na vipindi virefu vya jua na joto kali haimaanishi kuwa maeneo yote ya Dar es Salaam hubakia hivyo mwaka mzima. Jumia Travel imekusogezea maeneo haya 5 ambayo miaka nenda rudi lazima yakumbwe na mafuriko. 


Jangwani

Umaarufu wa Jangwani ni kwamba mvua ikinyesha tu, bila hata ya kutazama taarifa ya habari utajua ni lazima mafuriko yamelikumba eneo hilo. Na hii yote ni kutokana na jiografia ya eneo hili kupakana na mto Msimbazi ambao hupokea maji kutoka mito mbalimbali jijini Dar es Salaam kuelekea bahari ya Hindi ambayo ipo mita chache tu. Kwa muda mrefu wakazi wa eneo hili wamekuwa wakiambiwa na serikali kuhama lakini wamekuwa ni wakaidi. Sababu kubwa inayowafanya wakazi wengi kuling’ang’ania eneo hili ni kwa sababu lipo karibu na katikati ya jiji pamoja na huduma lukuki za kijamii kama vile usafiri. Wakazi wengi wanaoishi eneo hili hutembea kwa miguu kufika maeneo ya kazi.    
Tandale 

Kutokana na msongamano mkubwa wa makazi ya watu imekuwa ni vigumu sana kwa maji kupita kwenye njia yake. Kwa kiasi kikubwa eneo hili lipo kwenye mkondo wa maji na ndio sababu inayopelekea kukumbwa kwa urahisi na mafuriko. Urahisi wa upatikanaji na unafuu wa vyumba vya kupanga katika eneo hili usikudanganye na kujikuta ukataka kuishi. Siku zote nafuu ni gharama kama walivyosema wahenga. Ni kweli maisha ya Tandale ni ya chini sana lakini nakuhakikishia gharama utakazokuja kuingia kipindi cha mafuriko utajuta kulifahamu hilo eneo.

Buguruni kwa Mnyamani

Eneo la Buguruni lipo kwenye Wilaya ya Ilala ambayo ni maarufu kwa shughuli mbalimbali za kibiashara kama vile masoko ya Karume, Buguruni na Kariakoo. Ikiwa imezungukwa na biashara mbalimbali pamoja na huduma lukuki za kijamii, sio Buguruni yote ni mahali salama kwa makazi ya watu. Ikifika kipindi cha mafuriko Buguruni nayo huingia kwenye anga za habari za waathirika hususani eneo la kwa Mnyamani. Eneo hili kama maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko, wakazi wamejenga kwenye vyanzo vya maji na kuviziba kabisa. 
Kuna athari kubwa sana za kuzuia njia ya maji kwani yakifurika huwa hayachagui mahali pa kupita. Hivyo basi usije ukarogwa ukakubali kwenda kuishi eneo hili hata kama chumba ni bure.

Msasani Bonde la Mpunga

Kutokana na ukaribu wake na katikati ya jiji, eneo hili limevutia uwekezaji mkubwa wa majengo kadhaa ya kibiashara kama vile hoteli, maduka makubwa ya bidhaa, migahawa, ofisi, kumbi za filamu na mikutano, na kadhalika. Kwa asilimia kubwa wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha duni na wa hali ya kati. 

Eneo hili nalo ni sehemu ambayo miaka yote hukumbwa na mafuriko na sababu kubwa ni kwamba eneo hili lina asili ya majimaji. Sababu pekee ambazo zinawafanya watu kung’ang’ania eneo hili licha ya mafuriko ni upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii, uwepo wa vitega uchumi vingi hivyo kutoa fursa za ajira lakini pia ni takribani kilometa 6 mpaka kufika katikati ya jiji. Hivyo endapo utakwenda kuishi eneo hili tegemea kwamba kila ifikapo kipindi cha mvua basi ujue mafuriko ni lazima.  

Bonde la Mto Kigogo  

Eneo kubwa la Kigogo limepakana na mto Kigogo ambao hupokea maji kutoka mifereji mbalimbali na kisha kuungana na mto Msimbazi ambao humwaga maji yake katika bahari ya Hindi. Kutokana na wakazi wengi kujenga pembezoni mwa mto huu, ni jambo la kawaida ikifika kipindi cha mvua kukumbwa na mafuriko. 

Mvua zikiwa kubwa sana mto hutapika kwenye kingo zake na kusambaa eneo la karibu yake ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na makazi ya watu. Wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha ya chini na ya kati mbali na hapo pia ni karibu kufika katikati ya jiji ukiwa unaishi Kigogo. 
Kama utakuwa umegundua kitu ni kwamba wakazi wengi katika maeneo yaliyotajwa hapo juu wana sababu zinazofanana. Wengi wameng’ang’ania maeneo hayo kutokana na upatikanaji wa huduma za kijamii, unafuu wa maisha pamoja na ukaribu wa katikati ya jiji ambapo ndipo hufanyia shughuli zao. Lakini hizo hazitoshi kuwa sababu za kuhatarisha maisha yako, Jumia Travel inakushauri kwamba siku zote huduma za kijamii huwafuata watu na sio kinyume chake. 

Comments