Featured Post

WANANCHI WAMPONGEZA MKUU WA WILAYA YA UBUNGO JIJINI DAR ES SALAAM

Na Dotto Mwaibale

WANANCHI wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam wamempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo, Kisare Matiku Makori kwa kuweka utaratibu wa kusikiliza kero zao kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti  jijini Dar es Salaam jana walisema utaratibu anaoufanya mkuu huyo wa wilaya unapaswa kuigwa na viongozi wengine kwani unakwenda na kasi ya kazi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ya hapa kazi tu.


"Binafsi nampongeza mkuu wetu wa wilaya kwa kazi hiyo anayoifanya ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wake na kuzitafutia utatuzi ni jambo zuri na hasa anapokuwa na wasaidizi wake, wanasheria na Katibu Tawala " alisema Fabiola Sumary mkazi wa Mbezi kwa Yusuph.

Sumary alisema anapowashirikisha wenzake hasa wataalamu wake wakati wa kusikiliza kero hizo inasaidia kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja bila ya kupoteza muda mwingi.


Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la mama Mshindo alisema mpango huo umesaidia kwa namna moja au nyingine kupunguza msongamano ofisi ya mkuu wa mkoa ambako wananchi wengi walikuwa wakikimbilia kupeleka malalamiko yao.

Mkazi mwingine Francis Malota alisema mkuu huyo wa wilaya bila ya kujali jua, mvua  na kula amekuwa akiwasikiliza wananchi wake zaidi ya 70 kila siku jambo linaloonyesha jinsi anavyowajali.

"Tangu asubuhi hadi saa moja usiku amekuwa akisikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wake tunamuombea kwa mungu amzidishie hekima hiyo" alisema Caroline Mwangoka mkazi wa Mbezi kwa Mangi.

Mkuu huyo wa wilaya kila wiki amejiwekea utaratibu wa kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wake ikiwemo migogoro ya ardhi, jamii na ndoa.


Comments