OMARI NGOTWIKE: ALIACHANA NA AJIRA, AKAENDA SHAMBANI, SASA TEGEMEO LA MAMIA YA WAKULIMA KWA UZALISHAJI WA MITI YA MATUNDA


www.maendeleovijijini.blogspot.com
 
Maendeleo Vijijini
 Omari Ngotwike akichuma machungwa katika mojawapo ya miti iliyopo shambani kwake. Picha zote na Daniel Mbega wa MaendeleoVijijini.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
TAKRIBAN kilometa 9 kaskazini mwa mji wa Mkuranga kuna Kijiji cha Mwanadilatu.
Hiki ni miongoni mwa vijiji vya kwanza kabisa vya mfano ambavyo rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alihimiza vikaanzishwa katika utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea mwaka 1973.

Kama vilivyo vijiji vingi vya aina hiyo ambavyo vilishindwa kuendelezwa kwa sababu za kiutendaji kwa baadhi ya watendaji wa serikali, Mwanadilatu nacho kikabakia nyuma kimaendeleo.
Hata hivyo, katika mwitikio wa maendeleo vijijini ambapo watu wengi sasa wanakimbilia vijijini kwa ajili ya kilimo, Kijiji cha Mwanadilatu nacho kimeingia kwenye kasi hiyo ya maendeleo ambapo hivi sasa majumba makubwa na bora ya kisasa yamejengwa na baadhi ya watu wamenunua mashamba ili kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo.
Kwa bahati mbaya au nzuri, tayari kijiji hicho kimekwishaingizwa katika Halmashauri ya Mji wa Mkuranga, hivyo hata wenyeji wa kijiji hicho wameachana na utamaduni wa kumiliki mashamba makubwa na sasa wanauza vipande vya ardhi kama viwanja vya kujenga nyumba za makazi.
Ni katika kijiji hiki ambako MaendeleoVijijini ilimkuta mkulima Omari Ngotwike (59), ambaye hata nyakati za kiangazi shamba lake huendelea kuwa la kijani kutokana na kilimo endelevu cha matunda ambacho anakifanya.
“Nimekuja hapa mwaka 1995 baada ya kuacha kazi ya mshahara pale Tazara ambako nilikuwa mlinzi… niliamua kuja kijijini kwa sababu niliona nilikuwa napoteza muda wangu bure kwenye ajira wakati nguvu nilikuwa nazo na zaidi nilikuwa nimesomea masuala ya kilimo, hasa cha matunda,” anasema Ngotwike.
Mkulima huyo anasema kwamba, wakati alipohamia Mwanadilatu alianza na kilimo cha mihogo, mahindi na mboga mboga hasa baada ya kununua shamba la ekari tatu lililoko bondeni, kwa Shs. 20,000.
Wakati huo, anasema, mvua zilikuwa nyingi tofauti na sasa, hivyo mazao hayo yalizaa vyema.
Hata hivyo, mwaka 1997 akaamua kuanza kupanda miti ya matunda hasa michungwa na michenza kwa ajili ya matumizi ya familia huku akiendelea  na kilimo cha mahindi na mihogo pamoja na mpunga.
“Nilisomea masuala ya kilimo cha matunda kwenye Kituo cha Kibaha mwaka 1974 baada ya kupelekwa na serikali ya Kijiji cha Mabwepande. Huu ulikuwa ni utaratibu wa serikali kwamba kila kijiji lazima kiteue vijana wawili ambapo mmoja atasomea kilimo na mwingine biashara kwa ajili ya kusimamia miradi ya biashara ya kijiji, hasa duka. Mimi niliteuliwa kusomea kilimo,” ndivyo anavyosema.
Ngotwike anasema kwamba, baada ya kupata elimu hiyo alikaa kijijini hapo kwa miaka takribani nane kabla ya kuingia katikati ya jiji la Dar es Salaam kutafuta kazi kama ilivyo ada kwa vijana.
Anasema alifanya vibarua vya hapa na pale na kwa bahati nzuri akapata nafasi ya kwenda kwenye mafunzo ya Mgambo ambapo baada ya kuhitimu akapata ajira katika Shirika la Reli ya Tazara akiwa mlinzi.
“Nilifanya kazi kwa miaka minne tu kuanzia 1988 hadi 1992 nikaamua kuachana na ajira. Nilikaa kidogo mjini lakini nikaona hakuna kazi ninayoweza kuifanya kwa ufanisi isipokuwa kilimo, hivyo nikaamua kuja hapa Mwanadilatu,” anasema.
Mkulima huyo mpole na mkimya anasema kwamba, miaka kadhaa baada ya kuanzisha kilimo cha matunda kijijini hapo alishangaa kuona wanakijiji wengi wakija kwake, hasa nyakati za msimu wa mavuno ya matunda hayo, na ndipo akaona fursa ya kutumia elimu yake vyema kwa kuanza kuzalisha miche ya matunda na kuwagawia baadhi ya wakulima hao.
Kadiri siku zilivyozidi mahitaji nayo yakaongezeka, hasa kutokana na ujio wa watu wengi kutoka mjini ambao walikwenda kununua mashamba na kutaka kuyaendeleza kwa kupanda miti ya matunda.
“Sasa nikaona kumbe ninaweza kuzalisha miche mingi na kuiuza. Na kwa kweli mahitaji yamekuwa makubwa mno kushinda uwezo wangu wa kuzalisha,” anasema Ngotwike, ambaye anajivunia kilimo chake hicho pamoja na utaalam wake wa uzalishaji wa miche bora ya matunda ulivyomwezesha kujenga nyumba bora hapo hapo shambani kwake.
Ngotwike ni mtaalam hasa wa kilimo, ambaye  siyo tu elimu iko kichwani, bali anaitumia kila siku kwa vitendo.
Miche anayoizalisha kwa kuipandisha ama kuibebesha (budding and grafting) mara nyingi hutumia miaka mitatu tu tangu kupandikizwa shambani na kuanza kuzaa.
Maendeleo Vijijini
Kwake ukienda muda wote wa mwaka lazima utakula matunda – kama siyo embe, basi utapata chungwa ama chenza, achilia mbali mboga mboga.
“Lakini nataka kuongeza uzalishaji, hasa wa miche kwa sababu mahitaji ni makubwa. Changamoto niliyonayo kwa sasa ni uhaba wa maji kutokana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, zamani maji yalikuwa mengi, lakini hivi sasa hata visima vilivyopo vinakauka,” anasema.
Anasema kwamba, kama angeweza kupata msaada ama hata mkopo katika taasisi yoyote na kuchimba kisima kirefu, siyo tu angeweza kukifanya kilimo chake kuwa cha kibiashara zaidi, bali angeweza kupanua huduma zake za uzalishaji wa miche.
“Ninahitaji kiasi cha Shs. 12 milioni ili nichimbe kisima kirefu kitakachonipa uhakika wa maji majira yote, nikifanikiwa ninaweza kuzalisha miche karibu 20,000 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo uwezo wangu ni kuzalisha miche 800 tu kutokana na shida ya maji wakati tayari nina  oda ya michezo 1,500 kwa msimu huu pekee,” anasema.
Serikali ama taasisi binafsi zinazojihusisha na miradi ya maendeleo zinapaswa kuwatazama wakulima kama Ngotwike ili kuwawezesha walau mitaji hata ya vitendea kazi ili waweze kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi.
Msikilize mwenyewe akielezea: