MASAUNI ATOA WIKI MOJA KWA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI KUANZISHA KITUO WILAYANI RUANGWANaibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi pamoja na Wakuu wa Vyombo vilivyo chini ya Wizara yake mkoani humo.  Katika mzungumzo hayo, Masauni aliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha Kituo cha Zimamoto wilayani hapo kuanzia mwezi Aprili mwaka huu pamoja maandilizi ya Ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi wilayani humo.  Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Na Felix Mwagara/MOHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha kituo cha zimamoto Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Masauni alisema Aprili Mosi mwaka huu Jeshi hilo litakuwa na ofisi wilayani humo ili askari wa Jeshi hilo waanze kutoa huduma sehemu mbalimbali ya Wilaya hiyo ambayo ni muhimu kituo hicho kuwepo kutokana na uwepo na machimbo ya madini ya dhahabu pamoja na mji kuendelea kukua kwa kasi.

“Tumekubaliana vizuri baada ya Kamanda wa Zimamoto mkoa kuwa ifikapo tarehe moja askari wa zimamoto watakuwepo hapa Ruangwa rasmi kwa ajili ya kuanza kazi, na watapewa ofisi na halmashauri ya Wilaya, hivyo utaratibu wa kupata vifaa vya awali uanze mara moja kama tulivyokubaliana,” alisema Masauni.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Lindi, Christina Sunga alimuhakikishia Naibu Waziri pamoja na Watendaji wa Wilaya hiyo, agizo hilo atalifanyia kazi haraka iwezekanavyo na mpaka ifikapo Aprili mosi mwaka huu tayari askari wawili watakuwa wameripoti mjini Ruangwa.

“Uwepo wa askari hawa kutarahisisha kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuzima moto pamoja na kupambana na uzimaji moto, licha ya kuwa tunakuwa na vifaa vya awali vya uzimaji moto mpaka hapo tutakapopata gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzimaji moto na utoaji elimu zaidi,” alisema Sunga na kuongeza;

“Tunashukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutupa ofisi kwa ajili ya askari wa zimamoto lakini pia kutuwezesha kupata vifaa hivyo vya awali vya uzimaji wa moto.”

Aidha, Masauni alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, (RPC) Renatha Mzinga kuandaa mchoro pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi cha Wilaya ya Ruangwa ili ujenzi huo uanze.

“Nimekagua eneo la ujenzi wa kituo kipya cha polisi, eneo zuri na linafaa kwa ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi, maandalizi tayari yameanza na hivi karibuni RPC atakamilisha mchoro pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo hicho hapa Ruangwa,” alisema Masauni.

Pia Masauni amesema Wizara yake itahakikisha inawajengea ofisi Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani humo ambapo kwasasa ofisi hizo zipo katika jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Naibu WaziriMasauni amemaliza ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na askari na maafisa wa vyombo walio chini ya wizara yake mkoani Lindi na tayari amesafiri mkoani Mtwara kuendelea na ziara yake.Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akimpa maelekezo Fundi Mkuu wa ujenzi wa Gereza Ruangwa (kushoto) wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo unaoendelea mjini Ruangwa. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Lindi, Tusekile Mwaisabila. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ruangwa, Joseph Kiyengi wakati alipokuwa akionyesha eneo litakalojengwa Kituo kipya cha Polisi wilayani humo. Maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho yameshaanza. Katika ziara yake Masauni pia aliagiza uanzishwaji wa Kituo cha Zimamoto wilayani humo haraka iwezekanavyo. Katikati ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Twaha Mpembenwe. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ruangwa, Joseph Kiyengi alipokuwa anatoa taarifa yake katika Kikao cha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ruangwa ambacho kilijumuisha Wakuu wa Vyombo vilivyo chini ya Wizara hiyo mkoani Lindi.  Katika mzungumzo hayo, Masauni aliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha Kituo cha Zimamoto wilayani hapo kuanzia mwezi Aprili mwaka huu pamoja maandilizi ya Ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi wilayani humo.  Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.