MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU BAJETI YA TRILIONI 31.6 MWAKA 2017/2018
MAELEZO YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18MACHI 2017
DODOMA 

UTANGULIZI

1.           Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na  afya njema na kutuwezesha Wabunge wote kukutana hapa Dodoma kuanza kazi ya kuchambua mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia rasmi Makao Makuu Dodoma.
Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja, mshikamano na amani. Vile vile, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaponya Wabunge wenzetu ambao walinusurika katika ajali za barabarani na majini.  Nichukue fursa hii kuwapa pole sana Wabunge husika na pia wale wote waliofiwa na Ndugu na jamaa zao.

2.           Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kuwapongeza wenzetu walioteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni nikianza na Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela ambaye sasa amepewa dhamana ya kuongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mheshimiwa Prof. Palamagamba A. Kabudi (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria.  Aidha, natoa pongezi za dhati kwa Mama yetu Mheshimiwa Salma Kikwete kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Vile vile, ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliofunga ndoa baada ya Mkutano wa Sita wa Bunge la 11.

3.           Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2017/18. Mapendekezo haya yanawasilishwa kwa Wabunge kwa mujibu wa Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016 ili hatimaye Mheshimiwa Spika naye awasilishe Mapendekezo haya kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ili yafanyiwe uchambuzi na Kamati hiyo na kuzishauri kamati za kisekta pamoja na Serikali kuhusu mapendekezo haya kama inavyoelekezwa na Kanuni ya 97 fasili ya (4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

4.           Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni tathmini ya mwenendo wa uchumi na ustawi wa Jamii. Sehemu ya pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18. Sehemu ya tatu ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.

SEHEMU YA KWANZA

TATHMINI YA MWENENDO WA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII

5.  Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za awali zinaonesha kuwa, Pato la Taifa kwa mwaka 2016 lilikua kwa wastani wa asilimia 7.0, sawa na ilivyokuwa mwaka 2015. Hali hii imechangiwa na kasi kubwa ya ukuaji katika shughuli za: Uchimbaji Madini na Mawe (asilimia 16.5); Usafirishaji na Hifadhi ya Mizigo (asilimia 15.6); Habari na Mawasiliano (asilimia 13.5); na Huduma za Kifedha (asilimia 11.3). Aidha, kwa upande wa utekelezaji wa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda, shughuli za uzalishaji viwandani zilizidi kuimarika, zikiongezeka kwa asilimia 7.8, ikilinganishwa na asilimia 6.5 mwaka 2015.


7.  Mheshimiwa Mwenyekiti, Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Kimarekani milioni 4,325.6 Desemba 2016, kiasi ambacho kinatosheleza gharama ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.2. Katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Kimarekani ilibaki kuwa imara kufuatia usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti, ikishuka kwa wastani wa asilimia 1.2 kutoka shilingi 2,144.27 mwezi Desemba 2015 hadi shilingi 2,170.44 Desemba, 2016. Kwa upande wa Deni la Taifa, likijumuisha deni la ndani na nje, liliongezeka kufikia dola za Kimarekani milioni 19,021.9 Desemba 2016 ikilinganishwa na dola za Kimarekani milioni 18,459.3 Juni 2016, sawa na ongezeko la asilimia 3.05, lakini likibaki ndani ya vigezo vyote vya uhimilivu. Napenda kusisitiza kuwa, nchi kuwa na deni sio dhambi! Jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali (capital assets) ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kuendeleza Taifa lakini pia uwezo wa kulipa mikopo hiyo.

8.           Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ustawi wa jamii, idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini imeendelea kupungua kufuatia utekelezaji wa mikakati na sera za Serikali zinazolenga kuboresha maisha ya watu. Katika kufikia azma hiyo Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, umeme, barabara vijijini, nyumba na makazi bora. Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015/16, vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 51 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2010 hadi 43 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16. Vile vile, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 81 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2010 hadi 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16. Pamoja na kupunguza umasikini wa mahitaji ya msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa idadi ya Watanzania wanaokosa mlo kwa siku au kuishi kwa mlo mmoja inapungua kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 9.7 na kufikia asilimia 5.7 na 4.4 mwaka 2020 na 2025 kwa mtiririko huo. Hatua zinazochukuliwa ni kufikia lengo hilo ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa chakula na tija katika kaya, kuongeza fursa za ajira mijini na vijijini, na mpango wa kusaidia kaya masikini, kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mfuko wa Wanawake.

SEHEMU YA PILI

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2016/17 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18

A:      TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2016/17

9.           Mheshimiwa Mwenyekiti,  kwa mwaka 2016/17 Serikali ilitenga shilingi bilioni 11,820.503 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 8,702.697 zilikuwa za ndani na bilioni 3,117.805 fedha za nje. Hadi Februari 2017, fedha zilizokuwa zimetolewa ni shilingi bilioni 3,975.4, ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa Halmashauri, sawa na asilimia 34 ya bajeti ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 3,103.6 na fedha za nje shilingi bilioni 871.8. Kiwango kidogo cha fedha ya maendeleo iliyotolewa kilisababishwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuelekeza sehemu ya fedha za maendeleo kwenda kulipia madeni ya miradi ya maendeleo, lakini kiuandishi wa taarifa za kibajeti zinahesabiwa upande wa matumizi ya kawaida; Kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na Washirika wa Maendeleo kuchukua muda mrefu; na pia kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa. Hata hivyo, ni vema kutambua kuwa, mwenendo huu wa kupungua kwa misaada na mikopo haikuwa kwa Tanzania pekee. Nchi nyingine za Afrika zimekumbwa na hali hii. Mathalan, misaada ya maendeleo kwa kipindi cha 2009 hadi 2014 kwa nchi kama Zambia imepungua kutoka dola za Kimarekani milioni 1,267 hadi milioni 995; Cote d’Ivoire kutoka dola milioni 2,402 hadi milioni 922; Botswana kutoka dola milioni 209 hadi dola milioni 100; na Algeria kutoka dola milioni 318 mwaka 2009 hadi dola milioni 158. Kupungua kwa misaada kunafuatia kudorora kwa uchumi kwa baadhi ya nchi zinazotoa misaada, na kuchoka kuendelea kutoa misaada (aid fatigue) na mtazamo mpya kuhusu mfumo wa ushirikiano baina ya mataifa hayo na Afrika.

10.        Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, shilingi bilioni 161.639 za matumizi ya kawaida zimetumika katika mafungu mbalimbali kwa shughuli zenye asili ya maendeleo; na shilingi bilioni 192.609 zilipelekwa moja kwa moja na Washirika wa Maendeleo kwenye miradi ya maendeleo (D-funds) na hivyo kufanya fedha iliyotumika kwa shughuli za maendeleo kufikia shilingi bilioni 4,168.009 sawa na asilimia 35.26 ya bajeti ya maendeleo hadi Februari 2017. Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 59.896 zilichangiwa na mashirika ya umma na binafsi katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya kijamii (corporate social responsibility).

11.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Baadhi ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni pamoja na zifuatazo:

(i)        Makaa ya Mawe Mchuchuma na  Chuma Liganga – Njombe: maandalizi yote ya ujenzi wa miradi hii yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi. Vile vile, kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Corporation Ltd, ambayo ndio mbia katika miradi hii, wametenga jumla ya dola za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya kulipia sehemu ya mtaji (equity) wao katika miradi. Hatua iliyobaki ni kukamilisha mazungumzo kuhusu vivutio vya kodi vilivyoombwa na wawekezaji na bei ya mauziano ya umeme na TANESCO.


(ii)      Ujenzi wa Reli ya Kati: Mkandarasi kampuni ya YAPI MERKEZI ya Uturuki kwa kushirikiana na MOTA-ENGIL AFRIKA ya Ureno wamesaini mkataba wa kusanifu na kujenga awamu ya kwanza ya mradi kutoka Dar – Morogoro (Km 205) na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha. Kwa sehemu za reli hiyo kati  ya Morogoro na Makutupora (Km 336), Makutupora hadi Tabora (Km 294), Tabora hadi Isaka (Km 133) na Isaka hadi Mwanza (Km 249) taratibu zinaendelea za kupata fedha na Wakandarasi.

(iii)     Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Kazi zilizofanyika ni pamoja na kununua ndege mbili (2) zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. Ndege hizo zilianza kutoa huduma tangu Oktoba 2016. Maandalizi ya kununua ndege nyingine 4 yamekamilika na mikataba kusainiwa. Utekelezaji wa mkataba huu utagharimu dola za Marekani milioni 231.3, ambapo malipo ya awali ya kiasi cha dola za Marekani milioni 56.89 tayari yamefanyika. Kati ya ndege hizo, moja inategemewa kuwasili Julai 2017; mbili zinategemewa kuwasili Juni 2018, na ya mwisho, ambayo itakuwa ya masafa marefu inategemewa kuwasili Julai 2018.

(iv)     Ujenzi wa Mitambo ya Kusindika Gesi Kimiminika, Lindi: Hatua iliyofikiwa ni pamoja na: kupatikana kwa eneo la mradi, kule Likong’o mkoani Lindi; kuundwa kwa timu ya majadiliano na imefanikisha kuandaliwa kwa hadidu za rejea, kupitia nyaraka muhimu zinazohusu mradi (sera, sheria, mikataba, kanuni na mikakati ya Serikali); na kuanza kwa majadiliano na kampuni zinazoshiriki katika mradi juu ya masuala yatakayozingatiwa katika kuandaa mkataba kati ya makampuni husika na Serikali (Host Government Agreement – HGA).

(v)       Uendelezaji wa Maeneo Maaalum ya Kiuchumi
a.   Kituo cha Biashara cha Kurasini: kiasi cha fidia kilicholipwa kwa ajili ya kupata eneo la mradi ni Shilingi bilioni 101.04 na wananchi 1,019 tayari wamelipwa fidia na eneo hilo limetangazwa kwa wawekezaji tangu Desemba, 2016.

b.   Eneo Maalum la Uwekezaji la Bagamoyo: Hatua iliyofikiwa ni kulipwa fidia, ambapo shilingi bilioni 26.6 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi 1,155 kati ya 2,273 wanaopaswa kupisha mradi kwenye eneo la hekta 2,339.6. Kiasi cha Shillingi 51.3 bilioni kimebainishwa kuwa kinahitajika kukamilisha malipo katika eneo lililothaminishwa. Aidha, kiasi cha Shillingi billioni 81.45 kinakadiriwa kuhitajika kulipa fidia ili kupata eneo la hekta 3,257 ambalo bado halijafanyiwa uthamini.
c.    Eneo Maalum la Uwekezaji la Mtwara: Tayari eneo la hekta 110 kati ya hekta 2600 za eneo lililotengwa kwa ajili ya Mtwara SEZ limetangazwa kwa ajili ya matumizi ya bandari huru (Freeport Zone) na tayari maandalizi ya kuweka miundombinu, hususan barabara, kwa eneo hilo yanaendelea.

(vi)     Uanzishwaji wa Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari Mkulazi: Shilingi Billioni 2 ziliwekezwa katika mradi huu. Hatua iliyofikiwa pamoja ni: kupima ubora wa udongo; vitalu vya mbegu za miwa vimeandaliwa; na taratibu za kupata huduma ya wataalam wa kufanya upembuzi yakinifu, uchunguzi wa mbegu za miwa, upembuzi wa mazingira na utengenezaji wa barabara za kuingia katika eneo la mradi zinaendelea.

(vii)   Ununuzi na Ukarabati wa Meli Kwenye Maziwa Makuu: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea na taratibu za ununuzi wa ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika ziwa Victoria na ukarabati mkubwa wa Mv. Viktoria na Mv. Butiama. Kwa upande wa Mv. Liemba katika ziwa Tanganyika, mjenzi amepatikana ambaye ni M/S LEDA SHIPYARD. Kwa upande wa Ziwa Nyasa tayari meli mpya mbili za mizigo zimetengenezwa na zimeshafanyiwa majaribio. Fedha zimetengwa katika bajeti ya 2016/17 kwa shughuli zote hizi.

12.        Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda, mwelekeo umeanza kujipambanua vizuri. Miradi ya viwanda mbalimbali imeanzishwa kutokana na mchango wa sekta binafsi katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo mkoa wa Pwani unaongoza, ukiwa na jumla ya miradi mipya ya viwanda 82. Baadhi ya miradi mikubwa iliyozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi kwa mkoa wa Pwani ni pamoja na:- viwanda viwili vya kutengeneza marumaru (tiles), ambavyo vitakuwa vikubwa katika Afrika Mashariki na Kati vya Tywford Tiles (Chalinze) na Goodwill Ceramic (Mkuranga), ambapo uzalishaji unategemea kuanza mwezi Aprili, 2017; kiwanda cha nondo cha Kiluwa Steel Industries Ltd (Mlandizi Pwani) ambacho kimeanza uzalishaji; kiwanda cha Global Packaging (Mailimoja Pwani) kimefunguliwa na kinafanya kazi; kiwanda cha Bahkresa Food Product Ltd (Mkuranga) cha kutengeneza juisi ya matunda kimezinduliwa na kinafanya kazi; kiwanda cha Elyven Agric Co. Ltd (Bagamoyo); kiwanda cha Juisi cha Sayona Fruits Ltd (Mboga Pwani); kiwanda cha KEDS Tanzania Co. Ltd (Kibaha Pwani). Serikali imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia ujenzi wa viwanda hivi, ikiwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa ardhi, kuweka miundombinu inayohitajika, na kutoa vibali vya ujenzi na pia vivutio. Aidha, Halmashauri na Serikali za Mitaa katika maeneo haya zimekuwa na msaada na ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji ikiwemo kutoa maeneo ya viwanda ili kuhamasisha uwekezaji. Mathalan, Maswa wameanzisha kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Maswa Youth Enterprises Ltd kwa utaratibu huo. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na Serikali za Mitaa walioitikia kwa dhati wito wa Serikali kujielekeza katika kuvutia na kuwezesha uwekezaji. Niwatake pia viongozi wote nchini kuiga mfano wa wenzao wa mkoa wa Pwani.

13.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia kupitia mashirika yake mbalimbali imeanza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda, Mwitiko wa pekee na wa kupongezwa ni wa  Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambapo PPF na NSSF wanashirikiana kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na Mbigiri (Morogoro); LAPF wanajenga machinjio ya kisasa ya nyama (kwa Makunganya – Morogoro) na mifuko mingine inashiriki katika miradi mabalimbali. Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linashirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la viwanda la TAMCO – Kibaha kwa uendelezaji wa viwanda vya nguo na uunganishaji wa magari na matrekta, ambapo kiwanda cha kuunganisha matrekta kimefikia hatua ya kuanza majaribio. Aidha, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mifuko/vifungashio umeanza. Hatua nyingine zinazoendelea chini ya mashirika ya umma ni pamoja na jitihada za kufufua Kiwanda cha General Tyre (Arusha); hatua za awali za uwekezaji katika mradi wa uchenjuaji wa Magadi Soda (Bonde la Engaruka); na matayarisho ya kuanza kwa ujenzi wa kituo cha Biashara na Huduma Kurasini (Dar es Salaam), ambapo tayari makampuni mawili kutoka China yameonesha nia ya kujenga miundombinu ya majengo ya viwanda (industrial sheds).

14.        Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji miundombinu ya kuaminika. Kwa ajili hii Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha miundombinu na huduma za uchumi wa viwanda. Miongoni mwa miradi hii ni: ujenzi wa msingi kwa ajili ya mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi II (MW 240); ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 400  Iringa – Singida - Shinyanga (km 670); kV 220  Makambako – Songea (km 250); North West Grid kV 400 (Mbeya – Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi km 1,148); usambazaji umeme Vijijini na Makao Mkuu ya Wilaya (REA Turnkey Phase III), ambapo wateja 146,831 sawa na asilimia 58.7 ya lengo wameunganishwa; ukarabati wa njia ya reli ya kati na kuanza kwa taratibu za ujenzi wa reli ya kati kwa Standard Gauge na mkandarasi kwa ajili ya kusanifu na kujenga awamu ya kwanza amepatikana; ununuzi wa ndege mbili (2) za Serikali na nyingine kulipiwa malipo ya awali; kwa upande wa barabara mafanikio ni mazuri, ambapo barabara ya Masasi – Songea – Mbambabay, sehemu ya Namtumbo – Tunduru (km 193), na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala (km 202.5) zimekamilika; kwa barabara ya Ifakara – Mahenge Daraja la Kilombero limekamilika; ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati (km 261) umefikia asilimia 86.4; kwa barabara ya Bagamoyo – Msata na daraja la Ruvu chini imekamilika; barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 16.4; na ujenzi wa barabara za juu za TAZARA na Interchange ya Ubungo umeanza.

15.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa upande wa kufungamanisha ukuaji wa viwanda na maendeleo ya watu Serikali inaendelea kutekeleza sera ya elimumsingi bila malipo, uboreshaji wa miundombinu na huduma za ufundishaji na kufundishia, ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila; na kukamilika kwa ukarabati wa vyuo vya ualimu kumi. Aidha, katika kuimarisha ujuzi na stadi za kazi matayarisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2017, Miongozo ya Mafunzo Kazini kwa vitendo kwa wanafunzi (Apprenticeship Framework) na mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu (Internship Framework) yamekamilika na kuingiwa kwa mikataba na viwanda vya TOOKU Garment na Mazava Fabrics kwa ajili ya kutoa mafunzo ya stadi za ubunifu na ushonaji wa nguo. Maeneo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na kupanua upatikanaji wa maji mijini na vijijini; huduma za afya na upimaji wa maeneo ya makazi.

16.        Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine yaliyoendelea kutekelezwa ni yale yaliyotoa fursa za ajira na ushiriki wa wananchi wengi katika shughuli za uchumi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na: kuandaliwa kwa program ya muda mrefu na mfupi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi hususan kwa matumizi ya kilimo; kukamilika kwa ukarabati wa maghala 106 katika Halmashauri za Wilaya za Iringa, Mufindi, Mbeya, Songea, Kalambo, Mbozi, Momba na Njombe; kuingizwa nchini kwa tani 231,140 za mbolea; na tani 23,330 za mbegu bora zipo madukani kwa ajili ya matumizi katika msimu huu wa kilimo.

17.        Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kuhamishia Shughuli za Serikali Kuu Dodoma: awamu ya kwanza imekamilika ambapo majengo ya ofisi za wizara katika kipindi cha mpito na nyumba za makazi kwa baadhi ya viongozi zimepatikana. TBA na CDA wanaendelea na kukamilisha kukarabati nyumba za makazi na ofisi. Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba mpya 300 za makazi na zinazotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2017. Aidha, Serikali inaendelea na mazungumzo na makampuni binafsi kutoka Switzerland, China na Zimbabwe na pia ya ndani ambayo yameonesha  nia ya kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya maji kwa mji mpya wa Dodoma. Taasisi za Serikali kama vile TBA, CDA, TANESCO, SUMATRA, TEMESA, TANROADS, TTCL na Manispaa ya Dodoma zimekamilisha maandalizi ya awali ya kuboresha miundombinu muhimu inayohitajika kuwezesha uendeshaji wa  Serikali bila vikwazo katika kipindi hiki.

Changamoto za Utekelezaji wa Mpango wa Mwaka 2016/17 hadi Februari 2017

18.        Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2016/17 ni pamoja na ufinyu wa rasilimali fedha  na matayarisho hafifu ya miradi. Aidha, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija; Vile vile, hatua za makusudi zimechukuliwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu, kuhuisha Sheria, Kanuni, Taratibu na kupunguza ada, kodi na tozo za uwekezaji na uendeshaji biashara.

B:      MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18

19.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 ni wa pili katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na dhana yake kuu ni “Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu”. Maandalizi ya Mpango huu yameshirikisha wadau mbalimbali ikijumuisha Waheshimiwa Wabunge kupitia Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 walipojadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18, Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Taasisi za Utafiti na Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo.

20.        Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkutano tajwa, waheshimiwa wabunge walitoa maoni na mchango mkubwa uliotuwezesha kuandaa Mpango huu. Miongoni mwa maoni mahsusi ya Waheshimiwa Wabunge ni kuwa: Serikali ipunguze kukopa kutoka vyanzo vya ndani; Kukamilisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa njia za kielektroniki; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge upewe kipaumbele; TRA iandae mapema awamu ya pili ya ukusanyaji wa kodi ya majengo katika halmashuri na miji midogo iliyosalia; kutenga fedha za kutosha kugharamia utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia Makao Makuu – Dodoma; kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, hususan, bandari bubu na biashara za magendo na kubuni vyanzo vipya vya mapato; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; utekelezaji wa mkakati wa kujenga zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kila kata; kuimarisha upatikanaji wa madawa na vifaa tiba; kuongeza wigo wa fedha za mfuko wa maji; kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo, na maeneo mahsusi ya EPZ/SEZ; kutoa kipaumbele kwa utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma - Liganga; kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi; kuboresha miundombinu ya barabara; na kugharamia programu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

21.        Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na ushauri wa wadau wengine ambao umezingatiwa katika maandalizi ya Mpango huu ni pamoja na: Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango; kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya kufanyia biashara, hususan, upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu na miundombinu msingi ya barabara, reli, bandari na nishati ya umeme; na kuboresha utoaji wa huduma msingi za ustawi wa jamii zikijumuisha elimu, afya, maji, nyumba na makazi bora, umeme vijijini na utunzaji wa mazingira.

22.        Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2017/18, kimegawanyika katika sura kuu saba: Sura ya kwanza ni Utangulizi; Sura ya pili ni mapitio ya Hali ya Uchumi Duniani, Kikanda na Kitaifa; Sura ya tatu ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/17; Sura ya nne ni Maeneo ya Vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18; Sura ya tano ni Ugharamiaji wa Mpango; Sura ya sita ni usimamizi wa utekelezaji ikiainisha Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa; na Sura ya saba ni Vihatarishi vya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Kinga.

Maeneo ya Kipaumbele 2017/18

23.        Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi iliyobainishwa kuwa ya kielelezo. Miradi hii ni mahsusi kwa kuwa inatarajiwa kutoa matokeo makubwa kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wenyewe. Miradi hiyo ni:-
(i)           Ujenzi wa Reli ya Kati: ujenzi wa reli hususan sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro (km 205); kumpata mkandarasi wa kusanifu ujenzi kwa maeneo ya Morogoro hadi Makutupora (Km 336), Makutupora hadi Tabora (Km 294), Tabora hadi Isaka (Km 133) na Isaka hadi Mwanza (Km 249); kupata maeneo ya ardhi ya kuunganishia na kuanzishia treni ndefu kati ya Mpiji na Soga (Pwani), Buhongwa (Mwanza), na Ihumwa (Dodoma) kwa ajili ya kituo kikubwa cha treni za mizigo na makasha;

(ii)          Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania: kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege 3;

(iii)        Chuma Liganga – Njombe: kuimarisha ufuatiliaji na uratibu wa utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuratibu ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi; kupokea na kusafirisha mitambo, mashine na vifaa vya mradi hadi eneo la mradi; uwezeshaji wa ujenzi wa njia ya umeme ya Mchuchuma-Liganga, usimamizi wa ujenzi wa mgodi wa chuma na kiwanda cha chuma;

(iv)        Makaa ya Mawe Mchuchuma – Njombe: kusimamia ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi; kuratibu ununuzi, mapokezi na usafirishaji wa mitambo, mashine, na vifaa kutoka bandarini hadi eneo la mradi; na kusimamia ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe na kituo cha kufua umeme;

(v)          Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi: kuwezesha uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara, ikiwa ni pamoja na kusimamia ulipaji fidia; kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa Mipango Kabambe kwa uendelezaji wa miradi; kupima na kugawa viwanja kwa wawekezaji; kuandaa nyaraka za kisheria na kupata hati miliki za maeneo ya mradi;

(vi)        Mradi wa Liquified Natural Gas (LNG): kusimamia uhakiki wa thamani za mali za wananchi watakaolipwa fidia ili kupisha mradi; kuandaa michoro ya maeneo na mpango kazi wa kuwahamishia waathiriwa wa mradi; kuendesha majadiliano ya makubaliano baina ya makampuni na Serikali (Host Government Agreement); na kuandaa wataalam wazawa kwa ajili ya kuajiriwa na kuendesha shughuli za mradi; na

(vii)       Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi: Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF itaendelea na hatua za kuwekeza kwa ajili ya kilimo cha miwa kwa mashamba ya Mkulazi na Mbigiri na ujenzi wa kiwanda cha sukari.

24.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya kipaumbele, hususan, katika maeneo yafuatayo:

(a)        Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: eneo hili litahusisha miradi ya:- Uendelezaji wa Eneo la Viwanda TAMCO - Kibaha; Kiwanda cha General Tyre – Arusha; Mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Arusha; kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara; ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya; kuendeleza viwanda vya ngozi, pamba hadi nguo na madawa na vifaa tiba nchini. Aidha, hatua za kuhamashisha uwekezaji wa viwanda vinavyotumia malighafi inayopatikana kwa wingi nchini ikiwa ni pamoja na nyama, maziwa, maji, misitu, chokaa, mawe urembo, gypsum na mazao ya vyakula na matunda.

(b)        Kufungamanisha Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi katika eneo hili ni ile inayolenga kuimarisha: Elimu na Mafunzo ya Ufundi hususan: ugharamiaji wa Elimumsingi bila malipo; kutoa ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi na Sekondari; ununuzi wa vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum; ukarabati na upanuzi wa Maktaba ya Mkoa – Dodoma; na ujenzi wa Vyuo vitano vya VETA katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe, Rukwa na Kagera. Afya na Maendeleo ya Jamii: hatua zitaendelezwa za kuboresha Hospitali za Rufaa na mikoa; kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa; kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati; kuongeza udhibiti wa magonjwa ya kuambikiza; na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, hususan kwa vijana. Hatua zingine ni pamoja na kupanua upatikanaji wa Maji Safi, Usafi wa Mazingira, na Kinga dhidi ya Mabadiliko ya Tabia nchi. Miradi ya ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji Vijijini; kuboresha Huduma za Maji katika Jiji la Dar es Salaam; mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kahama, Nzega, Igunga, Tabora hadi Sikonge; ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji mijini na vijijini; na kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara-Mikindani; kujenga na kuimarisha hifadhi ya vyanzo vya maji na misitu, upandaji miti, uvunaji wa maji, kuhimiza matumizi ya teknologia jadidifu na hifadhi ya mazingira.

(c)         Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara: kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa miradi inayoendelea katika eneo hili; ukarabati wa miundombinu ya reli; miradi ya barabara na madaraja ikijumuisha barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Manyoni – Tabora – Uvinza, Tabora – Koga – Mpanda, barabara za juu za TAZARA na  Ubungo Interchange. Daraja la Selander na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (awamu ya II, III na IV) jijini Dar es Salaam. Aidha, miradi ya bandari ikijumuisha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Bagamoyo, na bandari kavu ya Ruvu na bandari za Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa). Kwa usafiri wa anga ni kuendelea na ujenzi wa jengo la abiria (terminal III) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere; upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora, Mwanza; ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Geita; Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara, Musoma, Iringa na Songea; na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro.

(d)        Maeneo Mengine Muhimu: hatua za kuimarisha mitaji na kutumia benki za ndani za maendeleo (TIB na TADB) kama vyombo vya kupanua upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu kwa wawekezaji; eneo hili linajumuisha miradi ya kuendeleza na kusimamia matumizi ya ardhi, maendeleo ya nyumba na makazi; ushirikiano wa kikanda na kimataifa; utawala bora na kuimarisha utawala wa sheria.

(e)        Kuhamishia Shughuli za Serikali Kuu Makao Makuu Dodoma: katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea na utekelezaji wa azma ya kuhamishia shughuli za Serikali makao makuu Dodoma. Katika utekelezaji wa azma hii, Wizara zimeelekezwa kutenga fedha za kugharamia stahiki za watumishi kwa kutumia ukomo wa bajeti uliotengwa kwenye mafungu yao. Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu upatikanaji wa maeneo ya kujenga ofisi na nyumba za viongozi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji na maboresho ya mpango wa ardhi katika mji wa Dodoma.

25.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka bayana imani yake katika mchango wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Lakini pia kuwa ushirikiano wake utakuwa kwa sekta binafsi ya kweli na yenye kufuata sheria na taratibu za nchi. Katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ili kuchochea ushiriki na maendeleo ya sekta binafsi, hususan, sekta binafsi ya ndani, katika utekelezaji wa Mpango na ujenzi wa viwanda. Kwa ajili hii, Serikali itaendelea kuboresha kanuni, taratibu na mifumo taasisi ya usimamizi wa biashara na uwekezaji nchini. Kwa kuzingatia hili, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
(i)         Kuweka sera, sheria na taratibu zinazochochea ushiriki wa sekta binafsi, ama kuwekeza moja kwa moja au kwa ubia na sekta ya umma;
(ii)        Kutenga maeneo ya uwekezaji ili kupunguzia sekta binafsi usumbufu hususan upatikanaji wa ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji (EPZ, SEZ na kuanzisha land bank chini ya TIC), na kuyawekea maeneo hayo miundombinu msingi, na kuikodisha kwa wawekezaji kwa gharama nafuu;
(iii)      Kujenga miundombinu wezeshi (barabara, umeme, maji na reli) na kuifikisha katika maeneo ya shughuli za wawekezaji;
(iv)      Kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu na kuhakikisha kuwepo kwa amani na usalama;
(v)        Kuanzisha mifuko maalum ya kuchochea ushiriki wa sekta binafsi, kwa mfano SAGCOT Catalytic Fund na PPP Facilitation Fund;
(vi)      Kuboresha huduma kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuanzisha “one stop centre” chini ya TIC, bandari ya Dar es Salaam na vituo vya utoaji huduma ya pamoja mipakani (one stop border post); na
(vii)     Kuweka utaratibu utakaoboresha upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha mitaji ya benki maalum za maendeleo (TADB) na (TIB).

Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa27.        Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vihatarishi mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo, vya ndani na nje. Baadhi ya vihatarishi vya nje ni pamoja na: mitikisiko ya kiuchumi, kikanda na kimataifa; majanga asilia na athari za mabadiliko ya tabianchi; na mabadiliko ya kiteknolojia. Kihatarishi kikuu cha ndani ni ufinyu wa rasilimali fedha na watu.

28.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau itakabiliana na vihatarishi kwa kuchukua hatua zifuatazo:- kupunguza utegemezi kwa kuwianisha mapato na matumizi, kuongeza mapato ya ndani; kuboresha mazingira ya biashara; na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Mpango na namna bora ya utekelezaji ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.
SEHEMU YA TATU

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2017/18

A:      TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17

Mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali Hadi Februari 2017
29.        Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Februari 2017, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia sh. bilioni 15,372.4 sawa na asilimia 79 ya lengo la kipindi hicho.  Kati ya hizo:
(i)           Mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 9,306.0 sawa na asilimia 95 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 9,764.2;
(ii)          Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,305.7 sawa na asilimia 72.5 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,806.2;
(iii)        Mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 310.6 sawa na asilimia 70 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 443.6;
(iv)        Mikopo ya ndani ilifikia shilingi bilioni 3,506.7 sawa na asilimia 78 ya makadirio ya shilingi bilioni 4,479.6 katika kipindi hicho; na
(v)          Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo  ilikuwa shilingi bilioni 1,253.6, sawa na asilimia 40 ya lengo la kipindi hicho la shilingi bilioni 3,117.2.

30.        Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kingine ambacho kilitarajiwa kuipatia Serikali fedha za utekelezaji wa bajeti ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara. Katika mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata hivyo, hadi kufikia Februari, 2017 Serikali haikuweza kukopa kutoka katika chanzo hiki kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17. Katika kipindi hicho, riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia 6 hadi wastani wa asilimia 9. Kutokana na sababu hiyo, Serikali iliahirisha mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo. Hata hivyo, gharama za ukopaji katika masoko ya Ulaya imeanza kuimarika, ambapo hadi sasa Serikali imesaini mkataba na  Kuwait Fund wa dola za Marekani milioni 51 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya – Nyahua. Vile vile, Serikali itasaini hivi karibuni mkataba na OPEC Fund wa dola za Marekani milioni 18 na Abudhabi Fund for Development (ADFD) wa dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Ilunde – Malagarasi. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na taasisi mbalimbali za kifedha ili kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo. Baadhi ya taasisi hizo ni Credit Suisse ya Uingereza (dola za Marekani milioni 300) na majadiliano yanaendelea na benki ya Barclays, HSBC na Citi Bank kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ambao unatarajia kugharimu Euro milioni 121.

31.        Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai, 2016 – Februari, 2017 jumla ya shilingi bilioni 16,152.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 12,177.1 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 126.3. Aidha, shilingi bilioni 3,975.4 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 177.6.

32.        Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa zinajumuisha shilingi bilioni 4,266.9 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Serikali, shilingi bilioni 6,135.0 kwa ajili ya mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali na shilingi bilioni 1,775.1 za Matumizi Mengineyo. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi bilioni 3,103.6 kama fedha za ndani na shilingi bilioni 871.8 fedha za nje sawa na asilimia 34 ya bajeti yote ya maendeleo.

Changamoto za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2016/17 hadi Februari 2017

33.        Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2016/17 ni pamoja na:
(i)           Mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki;
(ii)          Kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje; na
(iii)        Majadiliano ya muda mrefu yaliyopelekea kuchelewa kupatikana kwa fedha za Washirika wa Maendeleo.

34.        Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na:
(i)           Kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi  ya  mfumo wa EFDs;
(ii)          Kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa. Ili kupata suluhu ya kudumu, Serikali kwa sasa inafanya tathmini ya ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kazi ambayo inayoongozwa na aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Hatua hii inatarajia kuimarisha ushirikiano na kuwezesha upatikanaji wa fedha za uhakika katika bajeti ya Serikali;
(iii)        Kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki. Aidha, Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali  zinahimizwa kutumia mabenki katika kukusanya maduhuli.
(iv)        Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti kama ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015;
(v)          Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato; na kuendelea kuchukua hatua za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

B:      SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI  KWA MWAKA 2017/18

35.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2017/18, mapato ya ndani ya Serikali  yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza nakisi ya bajeti. Malengo ya mwaka 2017/18 ni: kuongeza mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; Kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 14.1 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; na kupunguza nakisi ya bajeti kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 hadi asilimia 3.8 mwaka 2017/18. Katika kutekeleza hili, Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua zifuatazo:

(i)           Kuendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
(ii)          Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi;
(iii)        Kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na kuboresha usimamizi wake;
(iv)        Kupanua wigo wa kukusanya  mapato yatokanayo na kodi ya majengo; na
(v)          Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

36.        Mheshimiwa mwenyekiti, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la ndani (domestic financial markets) ili kuwa na washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali kupata fedha za kuziba nakisi kwenye bajeti bila kulipa riba kubwa. Kuhusu fedha za nje, serikali itahakikisha kuwa mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya kibiashara unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo. Aidha, serikali itaboresha utaratibu wa mashauriano na majadiliano na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kama zilivyoahidiwa na kwa wakati. Kwa sasa Serikali inafanyia kazi mapendekezo yaliyomo katika taarifa ya washauri elekezi walioongozwa na  Bwana Donald Kaberuka aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kuhusu namna bora zaidi ya kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.
 
37.        Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo na tija, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo.

C:      MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2017/18

Mapato
38.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Bajeti ya mwaka 2017/18 inaonesha kuwa jumla ya shilingi bilioni 31,699.7 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 19,977.0 sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni shilingi bilioni 2,183.4 na shilingi bilioni 687.3 kwa mtiririko huo. Ili kuhakikisha upatikanaji wa mapato hayo, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato.

39.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote. Misaada na mikopo hii inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo; mifuko ya pamoja ya kisekta; na ya kibajeti (GBS). Aidha, Serikali inatarajia kukopa Sh. bilioni 6,156.7 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho sh. bilioni 4,948.2 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na kiasi cha Sh. bilioni 1,208.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa sh. bilioni 1,595.0 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.

Matumizi
40.        Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia shilingi bilioni 31,699.7 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 19,700.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la Taifa. Bajeti ya kulipia deni la Taifa imeongezeka kwa asilimia 18.3 kutoka shilingi bilioni 8,000 mwaka 2016/17 kutokana na kuiva kwa mikopo ya miaka ya nyuma iliyogharamia miradi ya maendeleo ambayo fedha za kulipia  mtaji na riba zimetengwa kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida. Matumizi mengineyo (OC) yametengewa jumla ya shilingi bilioni 3,033 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,085.2 ni matumizi yaliyolindwa na shilingi bilioni 274.9 ni matumizi yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 8,969.8 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 3,029.8 ni fedha za nje.

41.        Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2017/18, Serikali imeendelea kutenga fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo kama ilivyoanishwa katika  Awamu ya Pili ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2016/17 – 2020/21. Katika sura ya tano ya Mpango huo ambao ulipitishwa na Bunge, bajeti ya maendeleo inatakiwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi asilimia 40 ya bajeti yote. Hivyo, fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 11,820.5 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 11,999.6 kwa mwaka 2017/18, sawa na asilimia 38 ya bajeti yote. Ongezeko hili limezingatia misingi ya kibajeti pamoja na masuala mbalimbali kama ifuatavyo:

(i)           Kukamilika kwa baadhi ya miradi  ya maendeleo kama vile Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili – Kampasi ya Mloganzila ambayo inahitaji kutengewa fedha za uendeshaji badala ya fedha za maendeleo;
(ii)          Kuendelea kutenga fedha katika miradi inayoendelea kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ambao katika mwaka 2016/17 ulitengewa shilingi trilioni moja na kwa mwaka 2017/18 umetengewa shilingi bilioni 800 kulingana na mahitaji ya hatua ya ujenzi itakayoweza kutekelezwa katika kipindi hicho (absorptive capacity);
(iii)        Kuzingatia viwango vya mikataba katika miradi mbalimbali kama vile ununuzi wa ndege ambapo Serikali ilitenga kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya mwaka 2016/17 kugharamia ununuzi wa ndege mbili za Serikali na kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4. Kiasi kilichobaki kitalipwa kwa awamu katika bajeti ya mwaka 2017/18 na 2018/19 kulingana na viwango vya mikataba; na
(iv)        Kuendelea kupunguza mikopo ya masharti ya kibiashara ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuongeza mapato ya ndani na kupunguza nakisi ya bajeti ambayo kwa mwaka 2017/18 inakadiriwa kufikia asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.5 mwaka 2016/17 na hivyo kuendelea kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa.
42.        Mheshimiwa Mwenyekiti,. kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2017/18 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 1.

Jedwali Na. 1: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2017/18

HITIMISHO

43.        Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya mwaka 2017/18 yanalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuondoa vikwazo vya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda. Aidha, Serikali itaendelea kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi. Vile vile, Serikali  itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike katika uwekezaji wa miundombinu ya umma na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka. Suala hili linahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau wote kwa kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi.

44.        Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazopendekezwa katika Mpango huu zinalenga katika kujenga msingi madhubuti wa uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na biashara. Dhamira yetu sote ni kufikia kiwango cha uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025. Ili kushiriki katika mafanikio tarajiwa, kila mmoja wetu sharti ashiriki katika shughuli yoyote ya uzalishaji na afanye hivyo kwa juhudi na ufanisi ili kuleta tija. Kwa kila tunachokizalisha katika shughuli msingi (primary production) za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na misitu hakina budi kuongezewa thamani. Kwa kufanya hivi tutakuwa tumewajumuisha wananchi wengi katika mkondo wa uchumi wa kimataifa na mnyororo wa thamani kuwawezesha kuboresha maisha yao kwa kasi zaidi. Watanzania tukiwa na nia na kufanya jitihada, jambo lolote linawezekana na kila kitu kiko ndani ya uwezo wetu.

45.        Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi, mashirika ya umma na sekta binafsi kwa mwitikio wao walioonesha kwa kutekeleza kwa dhati azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda. Mwitikio huu unatuhakikishia kuwa tutaweza. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kufanya kila linalowezekana kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara. Aidha, Serikali itaendelea kudumisha majadiliano na ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi kuhusu mwenendo wa uchumi, utungaji sera na wajibu wa kila upande katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali.

46.        Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha