Featured Post

KILIMO BORA CHA MIPAPAI




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
Utangulizi:
Mipapai ni moja ya miti ya matunda inayolimwa ulimwenguni kote na hapa Tanzania, miti hiyo inalimwa karibu kila mahali. Mipapai au kwa jina la kitaalam Carica papaya, ni miongoni mwa spishi 22 zinazokubalika katika jenasi ya Carica na familia ya Caricaceae.
Asili ya mipapai ni katika maeneo ya tropiki huko Amerika, pengine kusini mwa Mexico na nchi kadhaa za Amerika ya Kati. Kwa mara ya kwanza miti hii ililimwa nchini Mexico karne kabla ya kuibuka kwa ustaarabu wa Mesoamerican.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, tunda la papai lina sukari, Vitamini A na C kwa wingi na huweza kuliwa kama tunda. Pia huweza kutengenezwa saladi, jamu na kukamuliwa kupata juisi.
Utomvu wa papai bichi hutumika kulainisha nyama na kutengeneza dawa mbalimbali.
Nchini Tanzania, wastani wa uzalishaji ni tani 2,582 tu kwa mwaka.
Hata hivyo, India na Brazil ndizo nchi zinazoongoza kwa uzalishajji wa mapapai ulimwenguni, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) za mwaka 2013, nchi hizo kwa pamoja zilizalisha 57% ya tani milioni 12.4 zilizozalishwa mwaka huo.
Takwimu hizo, ambazo MaendeleoVijijini imeziona, zinaonyesha kwamba, kwa mwaka 2013, India ilizalisha tani milioni 5.5, Brazil tani milioni 1.6, Indonesia tani milioni 0.9, Nigeria tani milioni 0.8 na Mexico tani milioni 0.8.
Zao hili ambalo llimepata umaarufu mkubwa duniani miongoni mwa mazao yanayozalishwa katika nchi za tropiki kwa sasa linashika nafasi ya nne nyuma ya migomba, machungwa na maembe.
Kidunia, uzalishaji umeongezeka kwa kasi katika miaka michache iliyopita, hasa kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji nchini India. Mapapai yamekuwa miongoni mwa mazao ya kilimo yanayosafirishwa nje ya nchi katika nchi zinazoendelea, ambako mapato ya usafirishaji wa zao hilo yameongeza ustawi wa maelfu ya watu, hususan katika nchi za barani Asia na Amerika ya Kati.

Mazingira:
Ingawa asili ya zao hili ni kusini mwa Mexico (hasa maeneo ya Chiapas na Veracruz), Amerika ya Kati, na kaskazini mwa Bara la Amerika ya Kaskazini, kwa sasa mipapai inazalishwa kwa wingi katika nchi za kitropiki duniani.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, mipapai huanza kuzaa miaka mitatu tangu kupandwa shambani. Hata hivyo, ni zao ambalo halihitaji unyevu mwingi na ndiyo maana linalimwa zaidi kwenye nchi za kitropiki ambako kuna joto.
Mipapai huhitaji jjoto la wastani kati ya nyzi 22 na 26 za Sentigredi na mvua kiasi cha milimeta 1,000 na 1,800 kwa mwaka. Zao hili linastawi vizuri kwenye udongo usiotuamisha maji kwani yakisimama kwa saa 48 tu mpapai unaweza kufa, wenye rutuba ya kutosha kwani mipapai haina mzizi mrefu, haihitaji udongo wenye kina kirefu na lazima udongo uwe na uchachu kati ya pH 6 na pH 7.
Upepo mkali huangusha mipapai, hivyo inashauriwa kupanda miti pembeni mwa shamba la mipapai. Inashauriwa kupanda miti ya kukinga upepo kuzunguka shamba lako, miti kama miparachichi, migravilea, vibiriti (leucaena Spp) na miembe pia inafaa. Hakikisha miti ya kukinga upepo inakuwa mirefu kuzidi mipapai kwa mita 10 mpaka 20 juu zaidi.
Kipindi cha jua kali mpapai usiachwe zaidi ya wiki 8 bila kumwagiliwa maji kama hakuna mvua ingawa wakati wa mapapai kuiva kama kuna ukame basi hii huongeza ubora wa papai ikiwemo kutooza mapema sokoni.

Usipande mipapai mfululizo kwenye shamba moja kwa zaidi ya miaka mitano kwa sababu hiyo inaweza kusababisha usugu wa magonjwa. Unahitaji kubadilisha mazao japo kwa msimu mmoja ili kuua mzunguko wa magonjwa.
Mipapai inaweza kuchanganganywa na miembe na mimea jamii ya michungwa, pia mazao ya msimu kama mahindi, mtama, ufuta, alizeti na mboga mboga yanaweza kulimwa.

Aina za mipapai:
Kwa kawaida kwenye mipapai kuna mipapai ya jinsia tatu: midume, majike na yenye jinsia zote (hermaphrodite) ambayo huwa na mapapai marefu zaidi, na pia kuna isiyoeleweka ambayo huwa na mapapai mafupi sana. 
Papai dume hutoa poleni peke yake, siyo matunda. 
Papai jike linaweza kuzaa matunda madogo, yasiyolika ikiwa halikuchavushwa. 
 
Mpapai wenye jinsia zote mbili unaweza kujichavusha wenyewe kwa sababu maua yake yana stamens za kiume na mayai ya kike. Kwa kawaida bustani nyingi za mapapai ya bishara zina miti yenye jinsia zote, yaani hermaphrodite
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, kuna aina nyingi za mipapai lakini zinazolimwa zaidi nchini Tanzania ni aina ya Solo, Hortus Gold na aina za kienyeji.
Solo ni aina ya mipapai ambayo maua yake yana mbegu za kike na kiume katika ua moja. Mapapai ya Solo yana umbo lililochongoka kidogo mfano wa yai au kama tunda la peasi na nyama yake ni nyekundu. Matunda yake hukua hadi kufikia uzito wa nusu kilo.
 Hortus Gold ni aina ambayo mbegu za kiume na kike zinapatikana katika maua tofauti lakini katika mmea mmoja. Rangi ya nyama yake ni ya dhahabu na matunda yake hukua hadi kufikia uzito wa kilo moja na nusu mpaka kilo mbili. Mapapai ya Solo ni matamu zaidi kuliko ya Hortus Gold na ndiyo yenye soko kubwa.
Utayarishaji wa shamba:
Shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupanda. Wakati wa kutayarisha shamba punguza miti, ng’oa visiki na fyeka majani, halafu yakusanye pamoja na yachome.
Chimba mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 40 upana, urefu na kina. Nafasi kati ya shimo na shimo iwe meta mbili au tatu na mstari na mstari iwe meta mbili na nusu hadi tatu. Baada ya kuchimba mashimo jaza mbolea ya samadi au takataka zilizooza vizuri (mata mahuluku) kiasi cha debe mbili kwa kila shimo.

Upandaji:
Mbegu za mipapai zinaweza kupandwa moja kwa moja shambani au kuoteshwa kwanza kitaluni na baadaye miche kuhamishiwa na kupandikizwa shambani.
Kama zitaoteshwa kitaluni zipande katika nafasi ya sentimeta mbili na nusu kutoka shimo hadi shimo na sentimeta 10 kutoka mstari hadi mstari.
Mbegu za mipapai zinaweza kupandwa kwenye viriba vilivyojazwa mchanganyiko wa udongo na mbole za asili. Kwenye kila pakiti weka mbegu 2 – 3.
Kwa kawaida, mbegu huota baada ya wiki mbili na miche huwa tayari kupandikizwa shambani kuanzia wiki sita hadi nane ambapo wakati huo miche huwa na urefu wa sentimeta 20-40. Kama udongo unatuamisha maji panda kwenye matuta yenye urefu wa sentimeta 40 – 60.
yaliyokwishatayarishwa mapema. Mbegu nane zipandwe katika kila shimo maana miche mingine inaweza kufa kwa magonjwa, kuliwa na wadudu au ikaota dume.
Katika kuandaa mbegu, kusanya mbegu kutoka kwenye mapapai makubwa na yaliyokomaa na kuiva, kausha mbegu vizuri kabla ya kupanda. Kama utapata mbegu za kununua ni vizuri zaidi. Baada ya kukausha hakikisha unazipanda ndani ya wiki moja.

Utunzaji wa shamba la mipapai:
Kupunguza miche
Baada ya mbegu kuota, miche ipunguzwe na kuacha miche minne katika kila shimo. Maua yakishatoka mipapai isiyotakiwa. Baada ya miezi 3 – 5 tangu kupandwa shambani mipapai itatoa maua na hapo jinsia ya mipapai itajulikana na mingine itabidi ipunguzwe na hasa midume, mipapai yenye jinsi zote inatakiwa isizidi asilimia 10 – 20 na midume ibaki mmoja katika kila mijike 25. Kama umepanda aina ya mipapai ambayo maua yake yana mbegu za kiume na kike, ondoa mipapai yote ya kiume. Mimea yenye magonjwa pia inabidi ing’olewe.

Urutubishaji wa udongo
Ili mimea iweze kukua haraka, inashauriwa kuweka mbolea za kukuzia kama vile SA au Urea. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 200 za SA au kilo 100 za Urea kwa hekta moja. Mbolea za asili kama vile samadi na mbolea vunde ziwekwe kila mwaka kiasi cha kilo debe moja hadi mbili kwenye kila mpapai ili kuongeza ukuaji na uzazi. Mabaki ya mimea yanaweza pia kuwekwa kama matandazo na h ii ni muhimu zaidi kipindi cha kiangazi ili kuzuia unyevu usipotee.

Palizi
Palizi katika shamba la mipapai ni muhimu hasa wakati wa mwanzo. Mipapai inapopandwa tu inaweza kuwekewa matandazo kuizunguka ili kuzuia uoataji wa magugu. Magugu yang’olewe yakiwa machanga na epuka kuchimbua chini sana maana mizizi ya mipapai huwa juu juu. Njia nzuri ni kuweka matandazo kwenye shamba lote ili kuzuia uotaji wa magugu.
Mipapai iangaliwe dhidi ya magonjwa, ing’olewe na kuchomwa au kufukiwa chini ikiwa itabainika kuwa na magonjwa, piga dawa dhidi ya magonjwa ya fangasi na virusi mara yanapoibuka ili kuongeza uzaaji na kipato chako.
  • Ondoa matawi yote yatakayojitokeza pembeni ya mpapai wako, na hii ifanyike mapema kabla ya tawi kuwa kubwa.
  • Ondoa mapapi yote ambayo yatakuwa hayakuchavuliwa vizuri na acha yale yenye afya tu
  • Weka miti ya kuegemea kama mpapai utazaa matunda mengi na hasa wakati wa upepo mwingi ili kuzuia mipapai isivunjike
  • Mipapai ikitunzwa inaweza kuishi mika mingi, ila kwa ajili ya mazao bora ondoa mipapai na upande mingine baada ya kila miaka mitatu (3) kwani mpapai unapo kuwa mkubwa basi rutuba yote huishia kwenye mti wenyewe

Magonjwa na wadudu waharibifu:
a)  Magonjwa
Mipapai hushambuliwa zaidi na magonjwa ya ukungu na virusi.
Magonjwa ya ukungu
Magonjwa ya ukungu huababisha majani na matunda kuwa na uyoga mweupe na madoa mesui ya mviringo. Mizizi huoza kutokana na athari za magonjwa hayo na mmea hufa.

Kuzuia
-         Kupanda mipapai katika sehemu isiyotuamisha maji
-         Kuweka shamba safi wakati wote
-         Kuepuka kujeruhi mizizi wakati wa kupalilia
-         Kubadlisha mazao
-         Kunyunyiza dawa za ukungu kama vile Dithane M 45.

Magonjwa ya virusi
Magonjwa ya virusi husababisha mmea kudumaa, majani kukunjamana na kilele kuwa na kitita cha majani. Magonjwa hayo huenezwa na panzi na vijidudu aina ya vidukari.

Kuzuia
-         Kutumia dawa kama vile Sumithion au Killpest ili kuangamiza wadudu wanaoeneza magonjwa hayo.

b)  Wadudu waharibifu
Wadudu wanaoshambulia zaidi zao hili la mipapai ni vidukari na minyoofundo.

Vidukari
Vidukari hivi hufyonza utomvu wa majani.

Dalili
Mmea hudumaa.

Kuzuia
Nyunyizia mojawapo ya dawa kati ya Sumithion au Dimethoate.

Minyoofundo
Minyoofundo hushambulia mizizi na kuifanye iwe na nundunundu.

Kuzuia
Kubadliha mazao. Baada ya kung’oa mipapai panda aina nyingine ya mazao ambayo haishambiliwi na minyoofundo kama vile mahindi na mazao jamii ya mikunde.

Wadudu na wanyama wengine waharibifu ni ndege na panya.

Uvunaji:
Mipapai huanza kuzaa katika kipindi cha miezi minne had inane.
Mapapai kwa ajili ya matumizi ya nyumbani yavunwe wakati yanaanza kubadilika rangi kutoka kijani kibichi na kuwa njano. Mapapai kwa ajili ya kusafirishwa yachumwe yakiwa yamekomaa lakini bado yakiwa na rangi ya kijani.
Uvunaji wa mapapai ni wa kutumia mikono au kutumia vichumio maalum. Vuna mapapai na vikonyo vyake ili kurahisisha ubebaji na kuzuia kuingia kwa vimelea vya magonjwa. Weka mapapai kivulini baada ya kuvuna.
Mipapai iliyotunzwa vizuri inaweza kutoa tani 40 kwa hekta kwa mwaka kwa mzao wa kwanza na tani 25 kwa hekta kwa mzao wa pili. Mavuno hupungua katika mzao wa tatu na kuendelea.
(Imeandaliwa na MaendeleoVijijini)

Comments