Featured Post

HII NDIYO CCM BWANA: WALIAMBIWA WAJIVUE MAGAMBA WAKAGOMA, SASA WAMECHUNWA NGOZI LAIVU KAVU KAVU!



 Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu anaonekana haamini kinachoendelea.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
JUMAMOSI ya Machi 11, 2017 itabaki kubwa kumbukumbu ya aina yake kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wananchama wake baada ya kushuhudia Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ikitoa adhabu kali kwa wanachama walioonyesha usaliti walioufanya mwaka 2015 wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Adhabu zilizotolewa ni pamoja na kuwafukuza uanachama baadhi yao huku wengine wakivuliwa uongozi na kupewa maonyo mbalimbali.
Waliofukuzwa uanachama ni pamoja na mwanachama mkongwe na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba ambaye amepoteza rasmi nafasi yake ya Ubunge wa Viti Maalum na Uenyekiti wa UWT kwani nafasi hizo zinahitaji mtu ambaye ni mwanachama wa chama cha siasa.

Uamuzi huo unamaanisha kwamba, CCM italazimika kupeleka jina jingine Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteua mbunge wa kuziba nafasi ya Sophia, huku nafasi yake ya Uenyekiti UWT ikisubiri uchaguzi baadaye mwaka huu.
Wenyeviti wa mikoa waliofukuzwa ni Ramadhan Rashid Madabida (Dar es Salaam), Christopher Sanya (Mara), Erasto Izengo Kwirasa (Shinyanga), na Jesca Msambatavangu (Iringa).
Wenyeviti wa CCM Wilaya waliofukuzwa ni Salum Kondo Madenge (Kinondoni), Assa Harun Simba (Ilala), Makoi S Laizer (Longido), Wilfred Saileli Ole Mollel (Arusha Mjini), Omary Awadh (Gairo), (Muleba), Ally S. Msuya (Babati Mjini), na (Bunda).
Wajumbe wa Halamshauri Kuu (NEC) ya CCM waliofukuzwa ni Ali Khera Sumaye (NEC Arumeru), na Mathias Erasto Manga (Arumeru).
Mjumbe wa NEC, Adam Kimbisa, kutoka Dodoma Mjini amesamehewa wakati Dk. Emmanuel Nchimbi amepewa onyo kali, ambapo hataruhusiwa kugombea nafasi yoyote kwa miaka minne.
Wengine waliopewa onyo kali kwa makosa mbalimbali ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Ahmed Kiponza ambaye pia ameondolewa madarakani, Hamis J. Nguli (Mwenyeviti wa Wilaya ya Singida Mjini) ambaye ameachishwa uongozi, Hassan Mzala (M-NEC Singida), Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke, Ali Mchumo (M-NEC Kilwa), Chief Ally Kalolo (M-NEC Tunduru) ambaye amevuliwa ujumbe huo na kupewa onyo kali, Muhaji Bishako (Mwenyeviti wa Wilaya ya Muleba) amepewa onyo kali, na Valerian Alemreta (M-NEC- Kibaha Vijini) ambaye ameachishwa uongozi.
Kilichotokea Dodoma, ambacho wapinzani wamekuwa wakikilalamikia kuliko hata wanachama wenyewe wa CCM, ni matokeo ya msimamo makini wa uongozi wa sasa wa CCM chini ya Dk. John Magufuli katika hatua ya kutaka chama kizaliwe upya.
Wengi kati ya waliadhibiwa walikuwa kwenye kambi ya mwanasiasa Edward Lowassa na ndio waliokuwa mstari wa mbele kuimba ‘Tuna imani na Lowassa’ Jumamosi ya Julai 11, 2015 baada ya Kamati Kuu ya CCM kumwengua mwanasiasa huyo kugombea urais.
Lakini hawa pia wamechelewa ama kujichelewesha wenyewe, kwani hawakuwemo miongoni mwa kundi la wanaCCM walioamua ‘kujivua gamba’ na kumfuata Lowassa alipokimbilia upinzani mwaka huo 2015.
Wakati CCM ilipokuwa imetangaza wanachama wake wajivue magamba mwaka 2011, hawa hawakuwa tayari, na hata wenzao walipoondoka, wao wakaendelea kubaki ndani.
Inawezekana kabisa hata wakati wa kampeni ilipokuwa ikiripotiwa kwamba siri nyingi za chama zilikuwa zikivuja, wahusika walikuwa baadhi ya hao wananchama ambao ama wamefukuzwa, kuvuliwa uongozi au kupewa onyo kali.
Kama waligoma kujivua magamba, sasa CCM imeamua kuwachuna ngozi kavu kavu! Hii ndiyo tafsiri pekee ambayo inaweza kuelezwa.
Nitawakumbusha kidogo jinsi mhemko wa kisiasa kwa upande wa upinzani na ombwe la uongozi ndani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) vilipoleta mtikisiko mkubwa uliochangiwa na kashfa mfululizo zilizokuwa zikiwakabili vigogo wa CCM na serikali yake hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutuhumiwa kwa vigogo wengi wa serikali ya chama hicho wakiwemo waziri mkuu aliyelazimishwa kustaafu kwa kashfa ya mkataba wa kinyonyaji wa kampuni ya Richmond, Edward Lowassa, aliyekuwa Mbunge wa Igunga Rostam Abdulrasul Aziz na makada wengine wa chama kulikuwa kumelitikisa taifa kiasi kwamba hata wale wasiokuwa wanasiasa walijikuta wakizungumza siasa.
Wimbo wa ufisadi ukatanda kila kona huku CCM, chama kikongwe kabisa barani Afrika ambacho bado kingalipo madarakani mpaka sasa, kikiwa kimepoteza mwelekeo na kuonyesha mpasuko wa dhahiri huku hao hao waliotuhumiwa ufisadi wakianza pia kutuhumiwa kutaka kuihujumu serikali kwa kuandaa kambi kwa ajili ya kuusaka urais mwaka 2015.
CCM, ambayo iliendelea kutuhumiwa kwamba inalea na kuukumbati ufisadi, ikaona haina namna zaidi ya kujitafakari upya.
Chama hicho, kupitia vikao vyake maalum, kikaanzisha mkakati wa ‘kujivua gamba’, ambao kimsingi uliwataka wale wote waliotuhumiwa kwa namna yoyote ile kukiyumbisha chama, wajitafakari na ikibidi wajiondoe wenyewe kabla ya kuondolewa.
CCM ilikuwa imechukua hatua hiyo ili kujisafisha na kuzaliwa upya, baada ya kuandamwa na tuhuma za ufisadi na mitafaruku isiyokwisha katika ngazi zote za chama hicho kwa muda mrefu.
Ni katika mabadiliko hayo ambapo aliyekuwa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, aliondolewa katika nafasi hiyo, ambayo ilichukuliwa na Wilson Mukama.
Fagio hilo likawazoa baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti, huku wajumbe mashuhuri katika Kamati Kuu, Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz wakipoteza nafasi zao kwa madai ya kuzongwa na tuhuma za ufisadi.
Kwa muda mrefu, baadhi ya wananchi ndani na nje ya chama hicho walikuwa na dhana kwamba viongozi hao ni miongoni mwa wanachama wa CCM ambao wamekichafua chama hicho kutokana na tuhuma za ufisadi.
Kwa kufanya hivyo, chama hicho kikasema kuwa kimejivua gamba la zamani na kujivika gamba jipya.
Kwamba kwa kufanya hivyo, mshikamano ndani ya chama ungekuwepo na chama hicho kingekuwa na dira na mwelekeo na hatimaye kuwa na mvuto kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alikuwa miongoni mwa makada waliounga mkono hatua ya kujivua gamba ambapo Desemba 26, 2011, akiwa mjini Meatu, alikaririwa akisema: “Falsafa hii ni nzuri ikiwa kila mwanachama ataelewa vizuri maudhui yake hasa katika kipindi hiki ambacho CCM inakabiliwa na changamoto za ndani na nje ya chama.”
Akawashauri viongozi na wanachama wa CCM waondokane na kuitafsiri dhana hii kinyume cha maudhui yake halisi, tafsiri ambazo zimesababisha migawanyiko na kupandikiza chuki na kuleta mitafaruku ya ndani ya chama badala ya kujenga inatengeneza nyufa kubwa zisizo na maslahi ya chama.
Lakini katika hali ya kushangaza, Mgeja akawa kinara wa wale waliomfuata Lowassa kuhamia upinzani baada ya kutemwa CCM, hali iliyodhihirisha kwamba mara nyingi viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikubaliana mdomoni na siyo katika uhalisia.
Lakini kujivua gamba tu hakukutosha, kwa sababu hakuna aliyetekeleza hilo kwa vitendo – si wanachama waliokuwa wakituhumiwa wala viongozi ambao walipaswa kuwawajibisha.
Mnyukano ukaendelea ndani ya chama na kushuhudia makada kadhaa wakianza kulumbana hadharani hasa kuhusu suala la kugombea urais. Chama kikawekwa rehani mbele ya Watanzania ambao waliona kwamba kumbe wengi walikuwa wakiwaza maslahi yao ya uongozi na siyo kuwatumikia wananchi.
Ndiyo maana kwa kuliona hilo, mnamo Februari 18, 2014, Kamati Kuu ya CCM, ikatangaza jijini Dar es Salaam uamuzi mzito dhidi ya wanachama wake sita ambao walikuwa wameitwa na Kamati Ndogo ya Maadili na kuwahoji kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu wa urais wa mwaka 2015.
CCM ikawatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), hivyo kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kwa ujumla, suala la kujivua gamba likabaki midomoni mwa watendaji wa chama bila kutekelezaji wa dhati na watu walikuwa wakihoji, hivi Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Dk. Jakaya Kikwete, alikuwa anaogopa nini kuwawajibisha watu?
Kila wakati tulisikia kwamba ‘bado tunatafuta ushahidi’ wa suala hili au lile, na kampeni ndani ya CCM dhidi ya ‘mafisadi’ zikadumu hadi uchaguzi mkuu 2015.
Matokeo yake ni ule mgawanyiko mkubwa uliotokea, ambao ulishuhudia wimbi kubwa la wananchama wakihama kwenda upinzani kama nyumbu wa Serengeti!
Pale ndipo tulipoamini kwamba, kumbe lile gamba lililosemwa lilikuwa limevaliwa na wengi, na walifanya hadharani pale Dodoma wakati wa uteuzi wa mgombea urais ambapo walionyesha ‘mahaba yao’ yalikuwa upande gani.
Ndiyo maana wakati ule baadhi ya watu walikejeli uamuzi wa CCM kwamba kelele za kujivua gamba ulikuwa moto wa karatasi, kwa sababu mwaka 2015 tuliwaona kwa macho yetu wale wote waliokuwa kwenye kambi mbalimbali, hasa kambi ya Lowassa, ambaye hata wapinzani wenyewe walimtuhumu kwa ufisadi kabla ya ‘kumtakasa’.
Wenyeviti kadhaa wa mikoa na wilaya wa CCM wakahama naye kama nyumbu, wakaenda upinzani wakiamini huko wangeweza kupewa upendeleo na kuwania ubunge, wakanyimwa.
Lakini bado kuna wengine walisalia, na waliendelea kuchunguzwa kwa mienendo yao na sasa imebainika kwamba walikuwa wamekisaliti chama ama kukiuka misingi ya chama, hivyo adhabu walistahili.
Kusema ukweli ni kwamba, hekaheka ambazo chama hicho kinakabiliana nazo mpaka sasa, kwa kiasi kikubwa zimesababishwa na vuguvugu zilizoamshwa na vyama vya upinzani kuliko wakati mwingine wowote katika maisha ya CCM.
Chama hicho kilijisahau na kubakia na mfumo wa utendaji wa kizamani ambao uliwaweka kando wanachama wa ngazi za chini na kuwapa wanachama wachache wenye fedha, sauti na mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya wengi.
Hali hiyo ndiyo iliyoondoa Imani ya wananchi wengi, wakiwemo wanaCCM wenyewe, na kuupa nguvu upinzani kuonekana kwamba ndiyo kimbilio na mkombozi pekee dhidi ya dhuluma za wazi ambazo zilikuwa zikifanywa na watendaji wa chama na serikali.
Kutafunwa kwa rasilimali za nchi, mikataba ya kifisadi ambayo imelitia hasara taifa na mambo mengine mengi, yote yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na vigogo wa serikali na CCM na ndiyo maana ilikuwa vigumu kuufumua mfumo wa ufisadi, rushwa na ukwepaji kodi.
Ungewezaje kumgusa mfanyabiashara anayekwepa kodi wakati ndiye anayeifadhili CCM katika kampeni? Au ungewezaje kuinyima zabuni kampuni ya mfanyabiashara ambayo ndani yake wanahisa ni vigogo wa chama na serikali? Zabuni zote zilitolewa kwa upendeleo ilimradi tu ulikuwa ndani ya chama!
CCM ikawa pango la walanguzi na wanyang’anyi wa mali ya umma ambao hakuna aliyethubutu kuwakemea kwa sababu walikuwa wanakula na wakubwa ndani ya chama na serikali.
Majambazi na wauzaji wa dawa za kulevya nao wakatajwa kwamba wamejificha ndani ya chama, achilia mbali majangili waliopopoa tembo wetu pamoja na kusafirisha hai wanyama kupeleka nje.
Nimepata kuandika mara kadhaa kuhusu namna CCM ilivyobinafsishwa na wafanyabiashara na kukiuka misingi imara ya uanzishwaji wake. Kila wakati wapo waliolalamika kwamba nilikuwa natumia lugha kali.
Lakini utaachaje kuzungumza ukweli – ambao unaumiza – katika nyakati ambazo unaona kabisa chama ambacho serikali yake iko madarakani kimepoteza dira na mwelekeo?
Unawezaje kukaa kima wakati unapoona chama ambacho awali kilitajwa kwamba ni cha wakulima na wafanyakazi (kwa msingi wa alama ya jembe na nyundo) kimegeuzwa kuwa cha matajiri wachache ambao wanakitumia kama ngao kulifisidi taifa?
Tazama hata chaguzi zake zilivyojaa hila kutokana na matajiri hao wachache kuamua ‘kusimamia shoo’ kwa kuhakikisha wale wote wanaogombea na kuchaguliwa kwenye nafasi mbalimbali – ndani ya chama na hata serikalini kupitia kwenye chama hicho – wanakuwa ni ‘watu wao’ ili walinde maslahi yao.
Mfumo wa rushwa na ufisadi ndio uliotamalaki hata katika kuwania nafasi za uongozi bila kujali sifa za wagombea, bali utashi wa watu ama kikundi cha watu fulani waliotaka mambo yao yaende bila kubughudhiwa.
Ni mfumo huo ambao ulimpa wakati mgumu Rais John Magufuli wakati wa kuwania uteuzi ndani ya chama pamoja na urais wenyewe baada ya kuteuliwa.
Siyo siri kwamba, hakuna kipindi ambacho CCM ilipata wakati mgumu zaidi wa kumpata mgombea wake wa urais na hata urais wenyewe kama mwaka 2015.
Wakati wa kampeni za mwaka 2015, zile shamra shamra za “CCM nambari wani” na nyinginezo hazikusikika. Mabango yote ya kampeni yalisema “Chagua Magufuli” badala ya “Chagua CCM”.
Viongozi wa chama pamoja na mgombea mwenyewe walijaribu kukinadi chama na Ilani ya Uchaguzi, lakini hali ikawa ngumu.
Ndiyo maana baadaye Magufuli mwenyewe akaamua kubadili staili kwa kuanza kuwashawishi watu “Wachague Magufuli” huku akieleza vipaumbele vya serikali yake mara atakapoingia madarakani. Hiyo ndiyo iliyosaidia Magufuli akashinda, lakini siyo kwa nguvu ya CCM. Huu ndio ukweli wenyewe na haupingiki.
CCM kimekuwa chama cha mabwanyenye ambao kila siku ama wanafikiria namna ya kuingia madarakani au jinsi ya kuendelea kuchota na kukalia madaraka hata kwa kuzivunja zile ahadi za chama, ikiwemo kutumia rushwa ingawa midomoni mwao wanaimba kuwa ‘rushwa ni adui wa haki’, tena wengine wanaongeza kwamba ‘ni dhambi’!
Kupata uongozi ndani ya chama hivi sasa watu hawaangalii sifa, wanaangalia uko kwenye ‘mtandao’ wa nani na umetenga fungu kiasi gani. Uongozi ndani ya CCM ni zabuni, hivyo mwenye fedha – hata kama hana sifa – ndiye atakayeshinda huku maskini wenye sifa za kuongoza wakitelekezwa.
Chaguzi za ndani ya chama zimeshuhudia rushwa ikitolewa waziwazi. Hakuna mwenye ujasiri wa kumkemea mwenzake kwa sababu hata yeye naye aliingia kwa njia hizo hizo!
Ukitazama makundi yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa kura za maoni kwa mwaka 2015 ndani ya chama hicho utaamini kwamba CCM ni Chama cha Matajiri, si Chama cha Mapinduzi kama ambavyo tunaimba midomoni.
Wengi ni wanafiki na wazandiki wakubwa na wameanza kuitumbua nchi mara tu baada ya Mwalimu Nyerere kufariki dunia mwaka 1999.
Wengine tumezaliwa enzi za TANU, tukajifunza misingi ya TANU kabla hata ya kuanza shule, tukalelewa wakati wa CCM yenye hekima, ni wafuasi wakubwa wa falsafa za Mwalimu na ndiyo maana binafsi niliona fahari kupiga kwata la chipukizi kwa miezi mitatu kujiandaa na maadhimisho ya miaka 10 ya Chama pale Dodoma mwaka 1987.
Tunapata hasira tunapowaona wachache wakikiharibu Chama wapendavyo. Wamekuwa kama makambare ndani ya dimbwi la maji. Hujui baba ni nani; mama ni nani wala mtoto ni nani, maana kila mmoja ana ndevu!

Comments