HATIMAYE PAUL MAKONDA AZUNGUMZA BAADA YA KUSAKAMWA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, leo amethubu kuongea baada ya kusakamwa kwa muda mrefu na vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
Na vita yake, ambayo ilianzia tangu wakati ule alipotangaza vita na operesheni dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kabla ya kupamba moto kuhusu tuhuma za kughushi vyeti na hatimaye kuvamia kituo cha runinga cha Clouds TV, imeonekana kuwa kubwa.

Ukubwa wa vita hiyo unachagizwa na kitendo cha Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuamua 'kupambana naye' akisaidiwa na 'jeshi la mtu mmoja' Mange Kimambi, ambaye ameweza kumpatia data nyingi Gwajima zinazomhusu Makonda na yeye akatumia madhabahu 'takatifu' kujitetea baada ya kutajwa kwenye orodha ya vigogo wa dawa za kulevya.
Vyombo vyote vya habari vimesusa kuandika habari za Makonda kutokana na kitendo cha kuvamia kituo cha Clouds TV na sasa Gwajima anaonekana kama 'shujaa wa Clouds na vyombo hivyo'.
Hakuna anayezungumzia tena vita dhidi ya dawa za kulevya wala kuona makosa mahali popote, isipokuwa wimbo uliopo ni kwa Rais John Magufuli kumfuta kazi Makonda kwa kughushi vyeti. Basi!
Lakini hatimaye leo Makonda mwenyewe akaandika hivi:
“They came for the Jews, I did not speak because I was not a Jew. They Came for the Socialists, I did not speak because I was not a Socialist. They came for the Catholics, I did not speak because I was not a Catholic. Then lastly they came for me, nobody was left to speak for me.”
Tafsiri isiyo halisi ya MaendeleoVijijini: "Waliwajia Wayahudi, mimi sikusema kwa sababu si Myahudi. Waliwajia Wajamaa, mimi sikusema kwa kuwa si Mjamaa. Waliwahia Wakatoliki, mimi sikusema kwa sababu si Mkatoliki. Hatimaye wakanijia mimi mwenyewe, hakuna aliyebaki kunisemea."