Featured Post

WASTAAFU WANAOLIPWA NA HAZINA WAJITOKEZA KUHAKIKIWA ZANZIBAR-WAILIIA SERIKALI IWAONGEZE PENSHENI

Zoezi la uhakiki likiwa linaendelea katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, kulia ni mstaafu Bw. Amir Apacho akifanyiwa uhakiki na Mkaguzi Bi. Mary Mauki.

Mkaguzi wa Ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango-Bara, Bw. Paison Mwamnyasi (aliyenyoosha mkono) akitoa maelekezo kwa wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliofika katika Ofisi za Wizara ya Fedha  na Mipango-Zanzibar, eneo la Vuga, kwa ajili ya uhakiki.

Benny Mwaipaja, WFM, Zanzibar

MAMIA ya wastaafu wa Taasisi za Muungano kutoka visiwa vya Pemba na Unguja-Zanzibar, wanaolipwa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamejitokeza kwa wingi kuhakikiwa huku wakiiomba Serikali iwaongezee pensheni kutokana na wengi wao kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Wakizunguza katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, iliyoko katika eneo la Vuga, wastaafu hao wamepongeza hatua ya Serikali ya kuwahakiki ili kufahamu hali zao na kwamba hatua hiyo itasaidia kuwabaini watu wasio na sifa ya kupata malipo hayo  kutoka Serikalini

Wastaafu Bi Sauda Ramadhani Mpambalyoto na Abuu Ali Hamisi, wameiomba Serikali iangalie namna ya kuwaongezea pensheni wataafu ambao wengi wao ni wagonjwa hawajiwezi na wengine wana afya njema, wanalima, lakini wanahitaji kuwezeshwa na Serikali ili waweze kumudu maisha ambayo wamesema yamepanda.

Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bw. Stanslaus Mpembe, amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango inaendesha zoezi la kuhakiki wastaafu wanaolipwa pensheni na wizara hiyo ili kuhuisha taarifa za wastaafu kwa lengo la kupata kanzidata (database) iliyo ili kuiwezesha Serikali kuwalipa wastaafu wanaostahili.

Amesema kuwa wastaafu wanaolipwa na Wizara hiyo ambao hawatahakikiwa wataondolewa kwenye orodha ya malipo ya pensheni kwa kuwa watakuwa wamekosa sifa.

Aidha Bw. Mpembe amesisitiza wastaafu hao kufika wenyewe na sio kutuma wawakilishi, wakiwa na nyaraka zote muhimu zikiwemo barua ya tuzo la kustaafu, barua ya kustaafu au kupunguzwa kazini, nakala ya hati ya malipo ya kiinua mgongo au mkupuo, barua ya ajira ya kwanza, kitambulisho cha pensheni, barua ya kuthibitishwa kazini, kadi ya benki na picha mbili ndogo zilizopigwa hivi karibuni.

Amesema kuwa zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina, litakamilika Mkoa wa Dar es salaam kuanzia Machi 6 hadi 10, mwaka huu 2017

Zoezi hilo la uhakiki linaloendelea Zanzibar, lilianza Oktoba 20, 2016 katika mkoa wa Pwani na limeshafanyika katika mikoa 25 ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Katavi, Rukwa, Morogoro, Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kigoma na Tabora, Lindi na Mtwara.

Comments