Featured Post

KITUO CHA FORODHA CHA MPAKA WA TUNDUMA/NAKONDE (TANZANIA NA ZAMBIA) CHAANZA KUFANYAKAZI

Kaimu Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha mpakani Tunduma/Nakonde, Bw. Tabaran Mzee, (aliyevaa sare za uhamiaji), akieleza namna idara hiyo ilivyoanza utekelezaji wa uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Forodha kati ya Tanzania na Zambia, ambapo wafanyakazi wa idara hizo kutoka nchi hizo mbili wanafanyakazi katika jengo moja kila upande wa nchi  ili kuboresha ufanyaji biashara mpakani.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (anayeshughulikia biashara na uwekezaji), Prof. Adolf Mkenda, akionesha kibao chenye namba za simu kilichowekwa Idara ya Forodha katika mpaka wa Tunduma/Nakonde zitakazotumiwa na wadau endapo watakuwa na malalamiko yoyote, lengo likiwa ni kuboresha huduma katika mpaka huo ambapo huduma ya pamoja ya forodha kati ya Tanzania na Zambia imeanza kutolewa rasmi tangu Februari mosi mwaka huu.
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Viwanda, na Mambo ya Ndani, wakizungumza na Afisa Forodha wa Zambia aliyeko katika Kituo cha Forodha cha Tunduma upande wa Tanzania, baada ya Ujumbe huo wa Serikali kutembelea mpaka huo kukagua shughuli za biashara ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuanza rasmi kwa huduma ya Kituo cha Pamoja cha Forodha katika mpaka huo wa Tunduma/Nakonde (Tanzania na Zambia).
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)


Benny Mwaipaja, WFM, Tunduma
KITUO cha Pamoja cha Forodha cha mpaka kati ya Tanzania na Zambia (Tunduma/Nakonde) kimeanza rasmi kutumika licha ya kukabiliwa na msongamano mkubwa wa magari unaotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Kituo hicho kimeanza kufanyakazi tangu Februari mosi mwaka huu, ambapo watumiaji wa mpaka huo watakuwa wakihudumiwa upande mmoja wa mpaka badala ya utaratibu uliokuwa ukitumika awali ambapo watumiaji walilazimika kukaguliwa mizigo yao kila upande hatua iliyokuwa ikichelewesha biashara katika mpaka huo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda na Naibu Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, wameeleza kuridhishwa na kazi inayofanyika mpakani hapo kupitia mfumo huo mpya.

Hata hivyo baadhi ya madereva wanaosafirisha bidhaa kupitia mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, pamoja na kupongeza utaratibu huo mpya, wameiomba Serikali iwasiliane na upande wa Zambia, ili waongeze kasi ya kuruhusu malori kuendelea na safari yanapofika mpakani hapo bila kucheleweshwa ili kwenda sambamba na kasi ya upande wa Tanzania, ambao umeboresha kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na watoa huduma katika mpaka huo yalikuwa ni kuwahudumia wadau wanaotumia mpaka huo kwa muda usiozidi siku moja na kuwataka madereva wa malori wanaokwazwa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika.

Prof. Mkenda amewaonya mawakala wa Forodha katika mipaka yote nchini watakao bainika kwa namna moja au nyingine kuwachelewesha wenye malori kwa makusudi watafutiwa leseni zao za kufanya biashara hiyo

“Tunataka mpaka huu wa Tunduma na Nakonde ufanye kazi kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu ili kuiwezesha bandari yetu ya Dar es Salaam kufanyakazi kwa kiwango cha juu ili kukuza biashara nchini” Alisisitiza Prof. Mkenda

Amesema kuwa Serikali imeunda timu ya wataalam wanaopitia kero mbalimbali za mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini, itakayo peleka mapendekezo namna ya kuboresha mazingira hayo kwa kuwa mchango wa sekta binafsi wakiwemo wawekezaji, unatambuliwa na Serikali

Kwa upande wao, Afisa Mfawidhi wa Forodha , Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa-Tunduma, Bw. Magori Magori, na Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka, wameelezea kukithiri kwa vitendo vya magendo mpakani na kero ya vizuizi lukuki kwenye njia kuu ya Dar es salaam hadi Tunduma, hatua inayokwaza biashara kati ya Tanzania na Zambia.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchunguza na kuishauri Serikali namna ya kuboresha matumizi ya pesa ya Zambia (kwacha) ili kupunguza changamoto ya ufanyaji holela wa biashara ya kubadilisha fedha hiyo katika mpaka wa Tunduma/Nakonde upande wa Tanzania na Zambia na mpaka wa Kasumulu/Songwe, upande wa Tanzania na Malawi.

Maagizo hayo yanafuatia kuwepo kwa biashara holela ya ubadilishaji fedha hiyo mpakani huku Benki Kuu ikieleza kuwa fedha hizo (kwacha) haziko kwenye orodha ya fedha za kigeni zinazotambulika rasmi hapa nchini hivyo kuwa vigumu kudhibiti mwenendo wake.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, ameahidi kuwa wizara yeke itaifanyia kazi changamoto ya uwepo wa vizuizi vingi vya malori yaendayo masafa marefu kwakuwa vinasababisha adha isiyo ya lazima na kukwamisha biashara nje ya nchi.

“Kwa kuwa malori mengi yaendayo masafa marefu kutoka Bandari ya Dar es Salaam yanafungwa vifaa maalumu vya ufuatiliaji mwenendo wake, hakuna sababu ya trafiki kuyasimamisha kila wakati, tunataka lori likikaguliwa Dar es Salaam lisafiri bila kusimamishwa hadi litakapofika mpakani ambapo litafanyiwa ukaguzi wa mwisho” aliongeza Balozi Yahya.

Kuanza kufanyakazi kwa kituo cha pamoja cha Forodha cha mpaka wa Tunduma/Nakonde kunafuatia maagizo yaliyotolewa na Marais Dkt. John Pombe Magufuli na Edgar Lungu wa Zambia, alipofanya ziara ya kikazi nchini Tanzania hivi karibuni ili kurahisisha biashara katika ya nchi hizo nan chi wanachama wa Jumuiya ya Madola-SADC, na kama mambo yatabaki kama yalivyopangwa, kitazinduliwa rasmi na Mawaziri wa kisekta mwezi Machi, mwaka huu.

Comments