JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 13)

Nilimkuta Janet West akiwa kwenye ofisi pana iliyosheheni kila kitu. Aliketi kwenye dawati, vitabu vitatu vya hundi vikiwa mbele yake na lundo la nyaraka pembeni yake. Alikuwa anaandika hundi wakati nilipoingia chumbani humo. Akaangalia juu, macho yake yakichunguza. Alinipatia tabasamu jepesi ambalo lingeweza kumaanisha chochote na kunielekeza niketi kwenye kiti pembeni ya dawati hilo.
“Unakwenda Hong Kong, Bwana Ryan?” akaniuliza, akikisogeza kitabu cha hundi pembeni. Akanitazama wakati nikiketi.

“Ninadhani, lakini siwezi kuondoka mara moja. Ninaweza kuondoka mwishoni mwa wiki kama nitakuwa na bahati.”
“Utahitaji sindano ya chanjo ya ndui. Na chanjo ya kipindupindu pia itakuwa ni busara kuipata, lakini siyo lazima.”
“Nimepata kinga zangu zote.” Nikachukua paketi ya sigara, nikamkaribisha moja na alipotingisha kichwa kukataa, nikawasha na kuirejesha paketi mfukoni. “Bwana Jefferson amesema una baadhi ya barua kutoka kwa mwanaye. Ninahitaji kila dondoo ya taarifa nitakayoweza kuipata, vinginevyo itakuwa ni upotevu mkubwa wa muda kwenda huko.”
“Tayari nimekwishakuandalia.”
Alifungua saraka ya dawati na kutoa takriban barua sita ambazo alinikabidhi.
“Herman alikuwa akiandika mara moja tu kwa mwaka. Zaidi ya anuani, nina mashaka kama zinaweza kukupatia taarifa za kutosha.”
Nilizitazama hizo: zilikuwa fupi mno. Katika kila mojawapo kulikuwa na ombi la fedha la dharura. Herman Jefferson hakuwa mtu wa kuandika, lakini alionekana kuwa na mawazo ya fedha kichwani mwake. Ni mara chache sana alisema alikuwa katika afya njema na hakuwa na bahati yoyote hivyo alimuomba baba yake kumpatia kiasi cha fedha haraka iwezekanavyo. Barua ya kwanza iliandikwa miaka mitano iliyopita na kila barua iliandikwa kwa tofauti ya kipindi cha mwaka mmoja. Barua ya mwisho, hata hivyo, ilinivutia. Iliandikwa mwaka uliopita.

Celestial Empire Hotel,
Wanchai

Mpendwa Baba,
Nimekutana na binti wa Kichina na ninamuoa. Anaitwa Jo-An. Amekuwa na maisha magumu kwa kuwa yeye ni mkimbizi kutoka China, lakini ni mzuri mno, makini na ni aina ya mwanamke ninayempenda. Ninadhani hutaweza kuvutiwa na taarifa yangu, lakini daima umekuwa ukinieleza kwamba lazima niangalie maisha yangu hivyo ninamuoa. Nimeridhika kwamba atakuwa mke mwema kwangu. Ninatafuta nyumba ya kupanga lakini siyo jambo rahisi kwa sababu gharama ni kubwa. Tunaweza kkuamua kubaki hapa hotelini. Mazingira ni mazuri kwa namna fulani japokuwa ninapendelea kuwa na nyumba yangu mwenyewe.
Ninategemea utatupa baraka zako. Kama unahisi ungependa kutuma hundi kwa ajili ya suala la nyumba litakuwa jambo jema sana.
Wako daima,
Herman.

Nikaiweka chini barua hiyo.
“Hiyo ndiyo ilikuwa barua yake ya mwisho kuandika,” alisema Janet West taratibu, pengine alikuwa akiyasoma mawazo yangu na kunifuatilia wakati nikizipitia barua hizo. “Bwana Jefferson alikasirika mno. Alituma ujumbe, akiilaani ndoa hiyo. Hakusikia chochote kutoka kwa au kumhusu mwanaye hadi siku kumi zilizopita wakati barua hii ilipowasili.”
Akanikabidhi barua iliyoandikwa kwenye karatasi mbaya iliyonukia harufu ya msandali. Hati ya mwandiko ilikuwa mbaya na haikuwa kazi rahisi kuisoma.

Celestial Empire Hotel,
Wanchai

Bwana Jefferson,
Herman amefariki jana. Alipata ajali ya gari. Kila mara alikuwa akisema angependa kuzikwa nyumbani. Mimi sina fedha lakini kama utanitumia kiasi nitaleta maiti yake huko ili azikwe kwa kadiri alivyopenda mwenyewe. Sina fedha za kumzika hapa.

Jo-An Jefferson.

Barua hii ilinipa mshtuko mkubwa na nikahisi kwamba mwanamke yule wa Kichina ghafla alikuwa ameachwa mpweke na maiti ya mumewe, akiwa hana fedha wala hatma yoyote labda tu mkwewe kama angemhurumia.
“Kisha nini kilitokea?” nikamuuliza.
Janet West alizungusha peni yake ya rangi ya dhahabu. Mamcho yake yalionyesha kuzama mbali zaidi.
“Bwana Jefferson hakuamini kama barua hii ilikuwa halisi. Alihisi kwamba mwanamke huyu alitaka kujipatia tu fedha kutoka kwake na kwamba mwanaye hakuwa amekufa. Nilimpigia simu Balozi wa Marekani nchini Hong Kong na kuthibitishiwa kwamba Herman alikufa kwenye ajali ya gari. Bwana Jefferson akaniambia nimwandikie mwanamke huyu, kumweleza kwamba airejeshe maiti huku. Alishauri kwamba yeye abakie Hong Kong na angemwandalia utaratibu wa kumtumia fedha kila mara, lakini kama unavyojua, alikuja pamoja na maiti, japokuwa hakuja hapa.”
“Na maiti?”
Nilikuwa na hisia kwamba alikuwa anajizuia. Nilihisi mshtuko ndani yake japokuwa hakuuonyesha.
“Mazishi yatafanyika keshokutwa.”
“Hivi ni kazi gani ambayo Herman alikuwa akiifanya Hong Kong ya kumpatia kipato?”
“Hajui. Wakati alipokwenda kwa mara ya kwanza, baba yake alimwandaa akawe meneja msaidizi katika kampuni ya usafirishaji lakini baada ya miezi sita, Herman akaacha kazi. Tangu wakati huo, hakuwahi kumweleza baba yake kazi aliyokuwa akiifanya: ni haya tu maombi ya fedha ya kila mwaka.”
“Bwana  Jefferson alimpatia alichokihitaji?”
“Oh ndiyo. Kila alipoombwa, alimtumia fedha.”
“Kwa kuangalia barua hizi,” nikasema nikizigusa barua hizo, “Herman anaonekana aliomba fedha mara moja kwa mwaka. Kiasi allichopelekewa kilikuwa sawa na kilitosheleza kwa kipindi chote cha mwaka?”
“Hakuwahi kutumiwa zaidi ya dola mia tano.” 

Itaendelea kesho...