JENEZA KUTOKA HONG KONG - (SEHEMU YA 12)


Nilijiuliza nani ambaye atakuwa amemwambia hayo, lakini nikakausha na kuuweka uso wangu katika taswira nzuri bila kusema neno.
“Nimekuita hapa,” Jefferson akaendelea, “kwa sababu ningependa kusikia kutoka kwako moja kwa moja kuhusu huyu mtu aliyekupigia simu na namna, baadaye, ulivyomkuta mwanamke wa Kichina akiwa amekufa ofisini kwako.”

Nikabaini kwamba hakuwa anamwita mkamwana wake. Nikagundua pia kwamba wakati aliposema ‘mwanamke huyu wa Kichina’, mdomo wake uliyoa beuo na sauti yake ilikuwa ya dharau. Nahisi kwa mtu mzee na tajiri na maarufu kama yeye, taarifa kwamba mwanao pekee ameoa mwanamke wa Kichina zingekuja kama mshtuko.
Nikamweleza hadithi nzima, nikikumbuka kupaza sauti yangu.
Baada ya kumaliza, akasema, “Asante sana, Bwana Ryan. Unaweza kujua kwa nini alikuwa anataka kukuona?”
“Siwezi hata kubashiri.”
“Wala hujui nani aliyemuua?”
“Hapana.” Nikatulia kabla ya kuongeza, “Kuna uwezekano kwamba mtu huyu anayejiita John Hardwick anaweza kuwa ndiye aliyemuua ama ameshirikishwa.”
“Sna imani na Retnick,” Jefferson akasema. “Ni mjinga asiye na akili na hana hadhi ya kuwa katika nafasi aliyonayo. Ninataka mtu aliyemuua mke wa mwanangu akamatwe.” Akaangalia kwenye mikono yake iliyosheheni misuli, akafura kwa hasira. “Bahati mbaya, mwanangu na mimi hatukuwa tunaelewana. Kulikuwa na makosa ya kila upande kama yalivyo daima, lakini baada ya kufa ndiyo ninatambua kwamba ningeweza kumvumilia. Naamini ukosefu wangu wa stahamili na kukataa kwangu tabia yake ndiko kulikomfanya aharibike zaidi kuliko ambavyo alipaswa awe kama angekuwa ameeleweka. Mwanamke aliyemuoa ameuawa. Mwanangu asingeweza kutulia mpaka ampate muuaji. Naijua tabia yake ndiyo maana nina uhakika na hili. Mwanangu amekufa. Nahisi kitu pekee ambacho ninaweza kumfanyia sasa ni kumtafuta mtu aliyemuua mkewe. Kama nitafanikiwa, nitakuwa nimemtendea hisani kubwa ambayo ingeweza kuturejesha pamoja japo kwa uchache,” Alitulia na kutazama bustanini, uso wake wa kizee ukiwa mgumu na wenye huzuni. Upepo mwanana ulizitimu nywele zake nyeupe. Alionekana mzee sana lakini mwenye dhamira kubwa. Akageuka kunitazama. “Kama unavyoona, Bwana Ryan, mimi ni mzee. Siku zangu zimekwisha. Ninachoka haraka. Siko katika hali ya kuweza kumwinda muuaji na hiyo ndiyo sababu nimekuita wewe. Wewe ni mtu muhimu sana. Mwanamke huyu alikutwa ofisini kwako. Kwa sababu zozote muuaji alitaka kukutwisha mzigo. Ninakusudia kukulipa vizuri. Unaweza kumtafuta mtu huyu?”
Ingekuwa rahisi kusema ndiyo, nichukue fedha zake halafu nisubiri kama Retnick ataweza kumpata muuaji, lakini sikuwa nafanya kazi kwa staili hiyo. Nilikuwa na uhakika nisingeweza kumpata muuaji mimi mwenyewe.
“Upelelezi uko mikononi mwa polisi,” nikasema. “Ndio watu pekee watakaoweza kumpata mtu huyu—mimi siwezi. Kesi ya mauji iko nje ya kazi za mpelelezi wa kujitegemea. Retnick haruhusu watu wa nje wamtimulie vumbi. Mimi siwezi kuwahoji mashahidi wake. Atapata taarifa na nitajikuta matatani. Ningependa sana kupata fedha zako, Bwana Jefferson, lakini haitawezekana.”
Hakuonekana kushangazwa, lakini akaonekana kuwa mwenye dhamira kama awali.
“Ninalitambua hilo,” akasema. “Retnick ni mjinga. Anaonekana hana wazo lolote la namna ya kushughulikia kesi hii. Nilimshauri awasiliane na mamlaka za Uingereza huko Hong Kong kuona kama tunaweza kugundua chochote kuhusu mwanamke huyu. Hatujui chochote kumhusu yeye isipokuwa aliolewa na mwanangu na alikuwa mkimbizi kutoka Bara China. Ninajua hayo kwa sababu mwanangu aliniandikia barua mwaka jana akiniambia alikuwa anaoa mkimbizi wa Kichina.” Kwa mara nyingine akatazama bustanini  wakati akisema, “Kwa ujinga wangu niliikataa ndoa hiyo. Sikusikia chochote tena kutoka kwake.”
“Unadhani polisi wa Kiingereza watakuwa na taarifa za mwanamke huyu?” nikamuuliza.
Akatingisha kichwa chake.
“Inawezekana, lakini siyo sana. Kila mwaka zaidi ya mamia kwa maelfu ya wakimbizi wanaingia Hong Kong. Hawajulikani wanatoka nchi gani kwa sababu hawana nyaraka zozote. Nina watu kadhaa huko Hong Kong na ninajaribu kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu suala hili. Kwa kadiri ninavyojua, ni kwamba: wakimbizi wanaokimbia kutoka Bara China wanavushwa na kundi la watu na kuingia Macau ambako, kama unavyojua, ni himaya ya Wareno. Macau haiwezi kukabiliana na uvamizi huo na wala haipendi. Baadaye wakimbizi hawa wanasafirishwa na kundi jingine na kupelekwa Hong Kong. Polisi wa Uingereza wanafanya doria kuangalia uingiaji huo Hong Kong, lakini Wachina ni watulivu na wajanja wanapotafuta njia zao wenyewe. Kama meli itaonekana ikiwa na wakimbizi, boti za polisi zinaifuatilia, lakini baharini kuna mashua nyingi za uvuvi ambazo zinakwenda kisiwani humo. Kwa kawaida mashua zenye wakimbizi zinafanikiwa kwa kuchanganyika na zile za wavuvi ambazo zinazizingira kwa hifadhi na kwa kuwa mashua zote zinafanana, inakuwa vigumu kwa boti za polisi kuziona. Natambua kwmaba polisi wa Kiingereza wana huruma sana kuhusu wakimbizi: hata hivyo, walikuwa katika nyakati ngumu na wanakimbia kutoka kwa adui yule yule ambaye Waingereza wanapigana naye. Upekuzi wao hukoma mara baada ya mashua kuingia katika eneo la bahari la Hong Kong. Polisi wanaona kwamba kwa kuwa watu hao maskini wamefika mbali, haitakuwa jambo la kibinadamu kuwarudisha walikotoka. Lakini watu wote hawa hawafahamiki. Hawana nyaraka. Polisi wa Kiingereza wanawapatia nyaraka mpya, lakini hakuna namna yoyote ya kuchunguza hata majina yao. Mara tu wanapoingia Hong Kong, wanaanza maisha mapya wakiwa na majina mapya: wanakuwa wamezaliwa upya. Mke wa mwanangu alikuwa mmoja wao. Mpaka tujua alikuwa nani hasa na maisha yake ya nyuma yalikuwaje, vinginevyo sidhani kama tutaweza kujua ni kwa nini aliuawa na nani alimuua. Kwahiyo ninataka wewe uende Hong Kong na kuona kama unaweza kupata jambo lolote kuhusu yeye. Haitakuwa rahisi, lakini ni jambo ambalo Retnick hawezi kufanya na polisi wa Kiingereza hawawezi kulifanya pia. Nadhani unaweza kulifanya na nitagharamia kila kitu. Unasemaje kuhusu hilo?”
Nilikuwa nimevutiwa na wazo lake, lakini siyo furaha ya kufanya nisahau kwamba kunaweza kusiwe na mafanikio.
“Nitakwenda,” nikamwambia, “lakini itakuwa ni kupoteza muda. Siwezi kusema ninaweza kufanikiwa au la mpaka nifike kule, lakini kwa sasa, sidhani kama kuna uwezekano mkubwa.”
“Nenda azungumze na sekretari wangu. Atakuonyesha baadhi ya barua kutoka kwa mwanangu ambazo zinaweza kukusaidia. Jitahidi kwakadiri ya uwezo wako, Bwana Ryan.” Akaniashiria niondoke. “Utamkuta Bi. West katika chumba cha tatu kwenye korido upande wa kulia.”
“Unajua siwezi kwenda haraka hivyo?” nikamwambia, nikisimama. “Ninapaswa kudhuria uchunguzi wa daktari na ninatakiwa kupata ruhusa kutoka kwa Retnick kabla ya kuondoka.”
Akaitikia kwa kichwa. Alionekana amechoka sana.
“Nitahakikisha Retnick hawi kizuizi kwako. Nenda haraka unavyoweza.”
Nikaondoka, nikimwacha akitazama mbele yake: mpweke na mawazo machungu ya kumbukumbu za nyuma zilizokuwa zikimtafuna.
 
  Itaendelea kesho...