- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF,
Julius Mtatiro (pichani) na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa
chama hicho, Abdul Kambaya kutuhuiwna, jana wamerushiana vijembe wakiwa katika
kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na Star TV.
Wiki iliyopita, aliyeanza kutoa tuhuma alikuwa Mtatiro
anayeunga mkono upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye
alieleza jinsi ruzuku ya chama Sh milioni 369, ilivyochukuliwa kinyume na
taratibu.
Baadaye Kambaya anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba,
alitoa tuhuma za uchotaji mwingine wa mamilioni ya fedha za chama hicho
unaodaiwa kufanywa na Mtatiro.
Jana, Kambaya akiwa mgeni Star TV Mwanza, Mtatiro
alishindwa kuhudhuria kwa upande wa Dar es Salaam kutokana na kuumwa ghafla
lakini baadaye alizungumza kwa njia ya simu.
Akizungumzia kuhusu walikopata fedha za kuzunguka, Kambaya
alisema hawezi kupewa fedha bila kuwa na utaratibu wa kikao.
“Hatuwezi kupewa fedha bila kuwa na utaratibu wa kikao na
msajili kuzuia ruzuku alikuwa na sababu za msingi. Wajumbe waliokutana pale
Ubungo Plaza tulilalamika kuwa mkutano huo haukuwa ni wa demokrasia.
“Baada ya malalamiko hayo kwa Msajili ndipo alipoamua
kusimamisha ruzuku kwa mwezi mmoja.
“Baada ofisi yake kutangaza kumtambua Lipumba kuwa ndiye
Mwenyekiti halali wa chama aliona mgogoro umekwisha ndipo akatuingizia fedha za
ruzuku hizo.
“Ofisi ya Katibu Mkuu iko pale Buguruni, aje pale kufanya
kazi. Kwa sasa nafasi ya Maalim anaisimamia Naibu Katibu Mkuu ambaye
atatekeleza wajibu wake hadi hapo atakapokuwa tayari,”alisema Kambaya.
Alipoulizwa kuhusiana na utaratibu ruzuku inapoingia,
Kambaya alisema: “Zinapangiwa kazi ruzuku wilayani na ndiyo maana Zanzibar wametoa
Sh milioni 86 hapo hawakuhusisha mtu zimeenda kufanya uchaguzi. Tuliandika
barua kwa msajili tukamweleza, hana sababu tena”.
Wakati anaendelea kutoa maelezo, Kambaya alihama kwenye hoja
na kumshambulia Mtatiro na baada ya muda mtangazaji alimtafuta Mtatiro
kupitia simu yake kiganjani naye alianza kujibu kama ifuatavyo;
Mtatiro
“Sijawahi kukimbia hata angekuwa Rais Magufuli…Kambaya
asijitape sana kwamba naweza kukimbia. Iko haja kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya
masuala ya msingi.
“Chama chochote cha siasa kinaongozwa na katiba yake…mgogoro
wa CUF ulitengenezwa mwaka 2015.
“Baraza Kuu la uongozi linaweza kuunda kamati maalum si
kweli katiba ya CUF haizungumzii Baraza Kuu kuunda kamati yoyote.
“Msajili wa vyama amealikwa na ameshiriki, Kambaya asiseme
Baraza Kuu halina uwezo wa kuunda Kamati ya Uongozi.
“Mkutano Mkuu uliandaa agenda, kwanza iliisha ya kukubali
kujiuzulu Lipumba. Na ajenda ya kumchagua mwenyekiti ndipo yale magenge ya
kukodiwa na watu wenye silaha ndipo tukaahirisha mkutano ule.
“Hao kina Kambaya wamekataliwa na Baraza Kuu na Mkutano Mkuu
halafu msajili anawapatia uhalali wao.
“Msajili wa Vyama vya Siasa aliwaandikia makatibu wakuu wa
vyama vyote akitaka makatibu wakuu wapeleke akaunti ya vyama.
“Kisheria fedha zinaratibiwa na makatibu wakuu wa vyama
hivyo na kama hawana muda wao ndiyo wanakasimu mtu kushughulikia, masuala
hayo hayabadilishwi,”alisema Mtatiro.
Mtangazaji wa kipindi hicho alipotaka kusoma maoni ya
watazamaji, Kambaya alimkataza asiyasome akisema ni ya vijana wa
Chadema.
“Wala usisome hayo maoni najua ya Chadema na hayanipi shida,
waliji-organize tangu jana (juzi) na wengine wana akaunti zaidi ya moja kwenye
mitandao ya jamii,” alisema.
Akijibu shutuma kwamba amekuwa ni wa kuteuliwa na si
kuchaguliwa, Mtatiro alisema:
“Kambaya anasema mimi sijawahi kuchaguliwa bali nateuliwa
tu, mimi nimegombea ubunge Segerea uchaguzi uliopita nikachaguliwa kwa kura
nyingi na nachangia ruzuku ya chama, yeye atuambie ameleta kura ngapi kuchangia
ruzuku?"
Comments
Post a Comment