WAFANYABIASHARA WAILALAMIKIA HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA ,WAPINGA NOTISI WALIYOPEWA

Image result for WAFANYABIASHARA WA MADUKA ARUSHA

Na Woinde Shizza, Arusha

WAFANYABIASHARA wa maduka jijini Arusha,wameilalamikia halmashauri hiyo ,wakipinga notisi ya miezi mitatu waliopewa ,inayowataka kuondoka katika maduka hayo,ifikapo Machi 30,mwaka huu, kufuatia maduka yao kudaiwa kumilikiwa ma madalali na hivyo kuikosesha  mapato halmashauri hiyo.
Aidha walidai kuwa hawapo tayari kuhama na hawatambuni notisi hiyo na wataendelea kufanyabiashara zao kama kawaida kwa kuwa wamekuwa wakilipa mapato ya halmashauri kama inavyopaswa.
Wakizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, uliolenga kujadili notisi hiyo, mwenyekiti wa wafanyabiashara hao jijini Arusha, Loken Masawe alisema halmashauri hiyo imetoa notisi kwa lengo la kutangaza tenda kwenye maduka hayo ,hatua hiyo walisema haiwatendei haki kwani wengi wao  walijenga maduka hayo na hatua hiyo itawasababisha washindwe kulipa fedha walizokopa kwenye mabenki mablimbali.
‘’Sisi hatujakataa tenda wanayotaka kutangaza kwenye maduka hayo ila kwanini wanataka kuweka watu wao ili sisi tufe njaa ,familia zetu tutazilisha nini ,tunachosema tenda hii sio halali na hatutakubali’’alisema Masawe.
Wafanyabiashara hao  ambao ni zaidi ya 1200 wanaomiliki maduka katika maeneo mbalimbali katika jiji hilo,walienda mbali zaidi kwa kumtaka rais John Magufuli kuingilia kati ili kuwanusuru na kadhia hiyo inayolenga kuwadhalilisha wao na familia zao
Naye mfanyabiashara Meja willson Lukumamu alisema kuwa walijenga maduka katika eneo la stand ndogo kwa gharama zao ,wakati huo eneo hilo lilikuwa pori na kwamba hadi sasa hawakuwahi kurejeshewe gharama zao .
‘’Huu mpango unaofanywa na manispaa ni batili kwani sisi kama wafanyabiashara hatujawahi kushirikishwa ,tunachotaka usitishwe na biashara zetu ziendelee kama kwaida’’alisema
Akizungumzia malalamiko ya wafanyabiashara hao,Meya wa jiji la Arusha, Kalisti Lazaro alisema kimsingi madai yao hayana msingi, kwani mpango huo ni utekelezaji wa maoni ya tume iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo iliyolenga kuchunguza uhalali wa umiliki wa maduka hayo.
Kalisti alisema kuwa halmashauri hiyo haitarudi nyuma katika mpango huo kwani imekuwa ikipozeza zaidi ya shilingi bilioni 2.1 kutokana na maduka hayo kumilikiwa na madalali ambao huwapangishia wafanyabiashara kwa gharama kubwa huku halmashauri hiyo ikipata mapato kiduchu.
‘’Baada ya tume kuundwa  na mkuu wa mkoa ,Mrisho Gambo ilifanyakazi ya kuchunguza uhalali wa umiliki wa maduka hayo na kubaini kuwa wamiliki wa maduka hayo wengi wao ni madalali na wamekuwa wakipangisha maduka hao kwa gharama kubwa na kuilipa halimashauri kiwango kidogo’’alisema Meya.
Alitolea mfano mfanyabiashara Morice Makoi kuwa anamiliki maduka 27, eneo la kituo cha daladala na amepangisha kwa shilingi laki tano hadi laki nane kwa  duka moja huku yeye akiilipa halmashauri hiyo shllingi 50,000 kwa mwezi,jambo ambalo alisema halikubaliki.
Alisisitiza kuwa halmashauri hiyo haina mpango wa kuwafukuza wafanyabiashara hao ila inachofanya ni kutangaza tenda upya ili kila mmoja aweze kuomba umiliki na atakayeshinda atakabidhiwa duka lake kwa mkataba maalumu .
Aliwataka wafanyabiashara hao kuacha kulalamika badala yake wafuate taratibu ikiwemo kuleta maombi mapya ya barua yatakayoambatana na TIN namba, Leseni na kwamba watakao kidhi vigezo hivyo watakabidhiwa duka mara moja.