Featured Post

WADAU 300 KUJADILI MATATIZO YA WAKULIMA

Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT Centre Limited, Jennifer Baarn

ZAIDI ya wadau 300 wa kilimo watakutana kujadili namna ya kuongeza thamani ya mazao na changamoto zinazowapata wakulima wadogo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Mradi wa Ukuzaji Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT Centre Limited, Jennifer Baarn aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa mkutano huo wa mwaka, ambao kaulimbiu ya ni kuibua fursa katika kilimo, utafanyika Machi 10, mwaka huu katika Jengo la LAPF jijini humo.
“Kuibuliwa fursa zaidi katika kilimo nchini kutatanua wigo kwa mazao yote yanayohitaji kuongezewa thamani,” alisema Baarn na kuongeza kuwa wadau wanapata fursa ya kubadilishana mawazo na kujadili kwa kina namna ya kuimarisha kilimo.
Mkutano namna huu utawakutanisha maofisa wa serikali, viongozi wa wakulima, taasisi za fedha na wadau wengine wa kilimo ikiwemo viwanda vinavyotegemea mazao kujiendesha.
Alisema kabla ya mkutano, Machi 7 na 8, mwaka huu, wadau watafanya ziara ya kutembelea kongani za Ihemi mkoani Iringa na ile ya Mbarali mkoani Mbeya kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali ya kilimo na ufugaji inayosimamiwa na SAGCOT.
“Wataona namna mazao kama mchele, soya, nyanya, chai na mifugo inavyosimamiwa kwa lengo la kuongeza thamani. Asilimia kubwa ni wakulima wadogo ambao awali walikuwa wakifanya kilimo kisicho na tija,” alieleza Baarn.
Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu huyo alisema kutakuwa na maonesho ya bidhaa na vifaa vya kilimo ili kudhihirisha namna mradi huo, unavyosaidia wakulima wadogo.
Akizungumzia makubaliano ya mkutano uliopita wa tatu, alisema walishauri wakulima kuendelea na majukumu yao ili kuongeza tija ya kilimo na vile vile walishauri viongozi wa serikali za mitaa na vijiji, kutoa ushirikiano kwa wakulima ili kuongeza ari na kuondoa vikwazo vitokanavyo na miundombinu au upatikanaji pembejeo za kilimo.
Kuhusu miundombinu, Baarn ambaye ni miongoni mwa waasisi wa SAGCOT, alisisitiza kuwa ushiriki wa serikali katika kuimarisha upatikanaji maji na nishati ya umeme pamoja na barabara zinazopitika kutawaondolea adha wakulima hasa katika maeneo ya vijijini.
“Miongoni mwa mambo mengine yatakayojadiliwa katika mkutano ujao ni upatikanaji maji na namna ya kuyadhitibi yasitumike vibaya na wakulima,” alisema na kuongeza kuwa tutaangalia pia namna ya kuboresha mazao ikiwemo nyanya, soya na ufugaji.
SAGCOT Centre Limited ilianzishwa miaka mitano iliyopita kwa lengo la kuinua kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania, ambapo hadi sasa mradi huo umeonesha mafanikio makubwa kutokana na kulenga wakulima wadogo ambao hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu kuongeza thamani ya mazao yao ili kupata faida kubwa.
CHANZO: HABARILEO

Comments