Featured Post

UFISADI UJENZI WA BWAWA WAKWAMISHA EKARI 400 ZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Diwani wa Kata ya Magulilwa wilayani Iringa, Ernest Kasike, akiwaonyesha waandishi wa Kwanza Jamii bwawa lililojengwa chini ya kiwango.


Na Daniel Mbega, Iringa
JUMLA ya ekari 400 zililengwa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Kata ya Magulilwa zimekwama kwa miaka saba sasa kutokana na ufisadi uliofanyika wakati wa ujenzi wa bwawa la maji.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, bwawa hilo lililojengwa katika Kijiji cha Magulilwa mwaka 2009, lililenga kuwanufaisha wakazi 13,639 wa kata hiyo – wanaume 6,663 na wanawake 6,976 – wakazi wa vijiji vitatu kati ya sita (6) vinavyounda kata hiyo, ambao walidhani mradi huo ungewakomboa kiuchumi.
Vijijini ambavyo vingenufaika moja kwa moja na mradi huo ni Magulilwa, Ng'enza na Mlanda. Vijiji vingine vya kata hiyo ni Ndiwili, Negabihi na Msuluti.
“Ndoto hizo za kilimo cha umwagiliaji zimetoweka, achilia mbali huduma nyingine za kijamii ikiwemo josho la kuogeshea mifugo hapa kijijini, ambalo limejengwa lakini si katika kiwango na ufanisi uliotakiwa,” anaeleza Isidory Mwakikoti, mkazi wa kijiji hicho.
Mwakikoti anasema kwamba, kwa takriban miaka saba sasa, bwawa hilo limeshindwa kufanya kazi baada ya kujengwa chini ya kiwango licha ya kugharimu Shs. 47 milioni.
Uchunguzi wa Fikra Pevu umebaini kwamba, fedha zilizotumika kwenye ujenzi wa bwawa hilo zilitoka kwenye Mradi Shirikishi wa Maendeleo ya Kilimo na Uwezeshaji (Padep – Participatory Agricultural Development and Empowerment Project), Halmashauri ya Wilaya pamoja na nguvu ya wananchi.
Aidha, mradi huo wa bwawa la Magulilwa ndio uliokuwa pekee kwa Mkoa wa Iringa kati ya miradi 69 ya malambo na visima iliyofadhiliwa na Padep nchi nzima tangu mwaka 2004 ambapo hadi mwaka 2007 yalikuwa yamegharimu jumla ya Shs. 3,003,785,439.
Mikoa mingine na idadi ya malambo ikiwa kwenye mabano ni Arusha (5), Kilimanjaro (1), Manyara (28), Tabora (2) na Singida (32).
“Usimamizi mbovu ndio uliofanya bwawa hili lijengwe kienyeji na chini ya kiwango licha ya kutumia fedha nyingi, lakini hili ndilo lingekuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa Magulilwa kiuchumi kwa sababu kuna eneo kubwa la bonde kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,” alisema Ernest Kasike, Diwani wa Kata ya Magulilwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Diwani huyo alisema, hata miundombinu ya bwawa hilo ikiwemo mifereji, ni mibovu hali ambayo inazua maswali mengi hasa kuhusu suala la usimamizi wa miradi ya jamii pamoja na fedha za umma.
“Serikali imepanga kulijenga upya ingawa bado upembuzi yakinifu haujafanyika ikiwa ni pamoja na kujua gharama za ujenzi huo.
“Tumeambiwa kwamba inabidi wayakaushe maji yote yaliyoko bwawani na kuanza ujenzi, lakini hawajasema gharama zake zitakuwa kiasi gani,” alisema na kuongeza kwamba tayari bwawa hilo lilikuwa limeanza kuzalisha samaki kwa wingi pamoja na kufuga bata maji.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Magulilwa, Majeshi Richard Ndambo, alisema wanufaika wa mradi wa bwawa hilo ni wengi kwa maana endapo litakamilika kuna ekari 400 zitakazotumika kwa kilimo cha umwagiliaji.
Alisema ekari hizo ni kati ya ekari 600 zinazofaa kwa umwagiliaji katika kata nzima, ambapo kwa sasa zinazolimwa ni karibu 200 tu.
“Tunaamini kama bwawa hili litakapokamilika na kuanza kutumika wananchi wengi wa kata hii watanufaika na watakuwa na kilimo endelevu cha masika na kiangazi, kwa sababu maeneo ni mengi yanayofaa kwa kilimo hicho,” alisema.
Hata hivyo, wananchi wengi wanaendelea kulima nyanya, maharage, pilipili hoho, bamia na njegere kwenye eneo lisilozidi ekari 50 katika bonde hilo wakitegemea zaidi unyevunyevu.
“Kama maji yangekuwepo hali singekuwa hivi, naamini mazao yangestawi vizuri kwa sababu wangeyamwagilia,” anasema Ndambo.
Ndambo anasema, kukamilika kwa bwawa hilo kungewanufaisha pia wafugaji, kwani wangeyatumia maji hayo pia kwa ajili ya josho lao la kuogeshea mifugo lililoko kijijini hapo.
Kwa sasa, anasema, wanapata maji kwa shida kwani wanalazimika kujaza maji kwa kuteka kwa ndoo kutoka umbali mrefu.
Miundombinu duni ya kilimo cha umwagiliaji inakwamisha kwa kiasi kikubwa uzalishaji huku wananchi wengi wakitegemea zaidi visima vya kienyeji.
Diwani Kasike alisema kwamba, ni muhimu kuhakikisha miundombinu bora inajengwa kwenye bonde linalotegemea uwepo wa bwawa hilo na hata bonde lililo kando kando ya Mto Ruaha.
Ofisa Mifugo na Kilimo wa Kata ya Maguliwa, Shaaban Ngwenga, alisema wananchi wa kata hiyo wanalima zaidi mahindi na maharage huku mahindi yakipewa kipaumbele zaidi ambayo hulima kwa ajili ya chakula na biashara, hususan mahindi mabichi, maarufu kama ‘gobo’.
“Tumepanga program ya kila mkulima awe na ekari tatu, ili ekari mbili azitumie kwa gobo na moja kwa ajili ya chakula,” anasema Ngwenga.

Miradi ya umwagiliaji
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuna miradi mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji ambapo mmojawapo ni mradi wa Bwawa la Maji la Mkungugu ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi wa Kijiji cha Mkungugu na vijiji vya Kising’a na Uhominyi katika Kata ya Kising’a, katika Tarafa ya Ismani.
Tarafa ya Isimani kwa miaka mingi inakabiliwa na ukame hata wakati wa masika kwa kukosa mvua za kutosha, hivyo kusababisha wananchi wengi kukabiliwa na njaa kila mwaka kutokana na kutegemea kilimo cha msimu ambacho nacho kimekuwa cha mashaka.
Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutoa taswira mpya ya ukombozi wa kiuchumi kutokana na kuwepo kwa bwawa hilo, ambalo inaelezwa kwamba limegharimu kiasi cha Shs. 1.2 bilioni hadi kukamilika.
Mbali ya kilimo, lakini kujengwa kwa bwawa hilo kutaondoa shida ya maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo huku pia likitumika kwa shughuli za uvuvi na samaki.
“Tumeanza kuvua samaki ingawa siyo wengi, lakini si haba, wanapatikana wa kitoweo,” anasema Simon Muhema, mvuvi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maji ya Kijiji.
Muhema anasema, kuwepo kwa bwawa hilo kumemfanya arejee kijijini hapo baada ya kutumia muda mwingi akivua samaki katika Bwawa la Mtera, ambako ameshuhudia wenzake wengi wakipoteza maisha na viungo kutokana na kujeruhiwa na mamba bwawani humo.
“Muda mwingi nimekuwa nikivua Mtera, lakini matukio ya mamba kujeruhi na hata kuua wavuvi yamenifanya nije nipumzike huku nyumbani. Nashukuru wakati nakuja na serikali nayo imetujengea bwawa hili,” anasema.
Mradi mwingine ni ule wa Skimu ya Umwagiliaji Mlambalasi katika Kijiji cha Kiwere wilayani humo, inayofadhiliwa na serikali na tayari imekwisha onyesha ukombozi kwa wananchi wa maeneo hayo tangu mwaka 2013 ulipokamilika, ambapo unawanufaisha wakulima kutoka kaya 1,000.
Mradi huo wa umwagiliaji kwenye eneo la hekta 500 (takriban ekari 1,250), ambao ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya serikali ya ‘Kilimo Kwanza’, ni wa pili katika Kijiji cha Kiwere, ambapo wa kwanza uliopo pembezoni mwa kijiji hiyo umekwishazaa matunda hasa kwa kilimo cha nyanya, mpunga, mahindi na bamia.
Ofisa Msimamizi wa Mradi, Joseph Hango, alisema ujenzi wa mfereji wa skimu hiyo wenye urefu wa kilometa 6.5, ukitokea katika Mto Ruaha, uligharimu Shs. 700 milioni.
“Awamu ya kwanza zilitumika karibu Shs. 400 milioni na awamu ya pili zilitumika Shs. 300 milioni ambazo zote zilitolewa na Serikali Kuu,” alisema Hango.
Hango anaongeza kwamba, endapo hekta zote 500 za umwagiliaji zitalimwa mpunga, kuna matarajio ya kuvuna wastani wa tani 2,500 kwa awamu moja, hivyo kuondoa tatizo la njaa.
Mfereji huo wenye ukubwa wa meta moja una uwezo wa kupitisha meta moja ya ujazo ya maji kwa sekunde (sawa na lita 1,000 kwa sekunde), kiwango ambacho kitatosha kumwagilia hekta 500 kwa uhakika.
Taarifa zinaeleza kwamba, mpango uliopo wa serikali ni kuhakikisha mfereji huo unajengwa hadi katika eneo la Muhunga, kiasi cha kilometa 18 kutoka yalipo maingilio ya mfereji huo kwenye Mto Ruaha.
Hata hivyo, mradi wa bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Mgama ambao ulipaswa wakulima takriban 3,000 wa vijiji vya Ibumila na Mgama umekwama baada ya kujengwa chini ya kiwango.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgama, John Kitime, anasema ujenzi wa bwawa hilo ulianza mwaka 2012 ulikuwa ukamilike mwaka 2015, lakini kwa kuwa ulijengwa chini ya kiwango ukingo wote wenye urefu wa meta 200 ukasombwa na maji.
Mradi huo ulikuwa unajengwa na kampuni ya GNMS Contractors Co. Limited ya mjini Iringa, inayomilikiwa na William Mungai.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mgama, William Msofu, alisema kukamilika kwa bwawa hilo kungeongeza tija kutokana na kilimo cha umwagiliaji hasa kwa mazao ya mboga mboga.
Alisema mashamba mengi ambayo yamekuwa yakitegemea mvua za masika yangebadilika na kuwa ya umwagiliaji katika majira yote ya mwaka, kwani uhakika wa kupatikana kwa maji ungekuwepo.
“Wakulima wengi wa Mgama wanalima nyanya, lakini wanategemea zaidi mvua za masika, ikiwa bwawa litakamilika, basi kilimo chao kitakuwa endelevu katika majira yote ya mwaka.

Usalama wa chakula
Idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Iringa Vijijini, hususan Tarafa ya Isimani, kwa miaka mingi wamekuwa wakikumbwa na uhaba wa chakula kutokana na ukosefu wa mbinu bora za kilimo pamoja na ukame.
Serikali inaendelea na utaratibu wa kugharimia miradi ya Umwagiliaji kupitia Programu ya Kilimo Endelevu (ASDP) ambapo miradi inaibuliwa na kuwekwa katika Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADP) na kuombewa fedha katika Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ngazi ya Wilaya (DIDF) kwa miradi midogo na ngazi ya Taifa (NEDF) kwa miradi mikubwa.
Kwa upande mwingine, Mfuko wa Maendeleo ya Hifadhi ya Jamii (Tasaf) nao umejitahidi kutatua kero ya maji kwenye Tarafa ya Ismani ambapo kwa mwaka 2011 ulitenga Shs. 102 milioni ili kujenga mabwawa matatu katika vijiji vitatu vya Kata ya Nyang'oro kwa lengo la kuwawezesha wananchi katika vijiji husika kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo, umwagiliaji wa bustani na kusaidia katika ujenzi wa nyumba bora na kuwaondolea kero ya usumbufu wa kufuata maji umbali mrefu.
Mratibu wa Tasaf katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Christopher Kajange alikaririwa mwaka 2013 akivitaja vijiji ambavyo vingenufaika na kuchimbiwa mabwawa katika tarafa ya Isimani kuwa ni Mangawe, Ikengeza na Mawindi.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu, alisema, program za umwagiliaji zinaendeshwa wilayani humo na kwa sasa kuna skimu 30 za jadi, miongoni mwazo 13 zimekarabatiwa yakiwemo mabwawa.
Alizitaja baadhi ya skimu hizo kuwa ni Tanangozi na Igingilanyi kwenye umwagiliaji wa matone, Mlenge, Magozi, Kiwere, Mlambalasi, Cherehani-Mkoga, Ipwasi-Ndorobo, Tungamalenga, Wangama na Ilolompya, wakati ambapo mabwawa yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa ni Mkungugu, Mgama, Ulongambi, Ikengeza, Nyang’oro na Malengamakali.
Mradi wa umwagiliaji wa Igingilanyi umetumia kiasi cha Shs. 1 bilioni ambapo jumla ya hekta 15 zinalimwa mazao mbalimbali.
Nyalu alisema, miradi ya Idodi na Nyang’oro ni ya uchimbaji mabwawa, ambapo jumla ya Shs. 6.5 bilioni zilikuwa zinahitaji kuweza kuikamilisha.
“Jumla ya hekta 43,000.7 zimeainishwa kama maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji lakini kwa sasa tuna eneo la hekta 21,000 tu linalotumika ambalo linawanufaisha wakulima zaidi ya 40,000. Changamoto kubwa inayotukabili ni fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji,” aliongeza Nyalu.
Mwaka 2011, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ilitenga Shs. 24 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kugharimia ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Vijiji vya Kiwere, Tungamalenga, Ipwasi-Ndorobo na Cherehani-Mkoga.
Mkurugenzi wa zamani wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Pudenciana Kisaka, alikaririwa wakati huo akisema miradi iliyoibuliwa na wananchi na kusaidiwa fedha na Tasaf ni ujenzi wa mifereji mitatu katika Kata ya Idodi, Kijiji cha Mfyome na Kata ya Kiwere.
“Mifereji mitatu ya Kata ya Idodi imejengwa katika vijiji vitatu ambapo ujenzi wake umegharimu jumla ya Shs. 107,537,008,” alisema.
Alifafanua kwamba, katika Kijiji cha Mahuninga mfereji uligharimu Shs. 35,762,568, katika Kijiji cha Makifu ujenzi wa mfereji uligharimu Shs. 35,982,522 na katika Kijiji cha Idodi ujenzi uligharimu Shs. 35,793,918.

0656-331974
CHANZO: FIKRAP

Comments