Featured Post

UBUNGE WA LEMA WAWEKWA REHANI, HATARINI KUUPOTEZA



Na Mwandishi Maalum
KAMA Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema alidhani kwamba kesi za lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli ambazo zinamkabili zinamuongezea umaarufu, inabidi ajifikirie upya.
Inaelezwa kwamba, kitendo cha kuendelea kusota rumande bila dhamana kimeuweka ubunge wake rehani wake, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya siasa.
Na ikiwa atabaini hilo, naamini anaweza asinyooshe vidole viwili kila anapokwenda mahakamani, badala yake anapaswa kunyoosha mikono yote juu kumuomba Mungu walau ajalie heri apate dhamana.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kwamba, kwa mujibu wa taratibu za Bunge, huenda Jimbo la Arusha Mjini likatangazwa kuwa wazi baada ya kupita siku 90 ikiwa Lema ataendelea kubaki mahabusu.
“Hii ni kwa sababu kisheria wananchi wa Arusha Mjini watakuwa hawana uwakilishi kutokana na mwakilishi wao kuwa mahabusu,” amedokeza mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Iringa (zamani Tumaini).
Jumatano, Januari 4, 2017 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilishindwa kusikiliza rufani ya Jamhuri kupinga dhamana ya Lema, baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha notisi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa wakipinga kusikilizwa kwa rufani hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Salma Maghimbi alitarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa ya Jamhuri iliyopinga Lema kupatiwa dhamana Novemba 11 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha katika kesi namba 440 na 441/2016 za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli, ambapo siku hiyo Jamhuri iliwasilisha notisi ya mdomo.
Kwahiyo, baada ya Lema kufikishwa mahakamani Januari 4, 2017 saa 3.25 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali, huku pia polisi wakiwa wametanda viwanja vya Mahakama Kuu ndani na nje sanjari na gari moja la maji ya kuwasha, na baada ya mawakili wa pande zote kujitambulisha, Jaji Maghimbi alisoma notisi ya Jamhuri kupeleka shauri hilo Mahakama ya Rufaa na kueleza kufungwa kisheria kutoa uamuzi wa rufani hiyo.
Hatua hii inamaanisha kwamba, shauri hilo sasa linahitaji kupangiwa tarehe na Jaji katika Mahakama ya Rufaa kwa ajili ya kutajwa kwanza kabla ya kuanza kusikilizwa, jambo ambalo linaweza kushuhudia Lema akiendelea kubaki mahabusu hadi mwishoni mwa Januari au mwanzoni mwa Februari, 2017.
Lema (40) alikamatwa na polisi Novemba 3, 2016 akiwa Bungeni Dodoma na kupelekwa Arusha ambako alifunguliwa mashtaka.
Ikumbukwe pia Lema na mkewe, Neema Lema (33), wana kesi nyingine ya kumtukana Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ambapo ilielezwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Arusha Agosti 20, 2016 kwamba, wakitumia simu na mkewe walimtumia ujumbe wenye lugha ya matusi mkuu huyo wa mkoa huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Ujumbe huo ulisema: “Karibu, tutakuthibiti kama Uarabuni wanavyothibiti mashoga.”
Kuhusu kesi ya uchochezi dhidi ya Rais Magufuli, Lema alipewa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, lakini kabla hakimu hajatoa masharti ya dhamana, upande wa Jamhuri ulisimama na kuweka pingamizi la mdomo na mahakama ikakubaliana nao bila kutekeleza uamuzi wa dhamana.
Katika kesi hizo, Lema alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 8, 2016 na kusomewa mashtaka ya uchochezi kwa viongozi wa serikali kwa maana ya kumtishia Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo pamoja na kauli dhidi ya Rais Magufuli kwamba asipojirekebisha atafariki.
Kauli kwamba Rais Magufuli asipojirekebisha atakufa aliitoa wakati akiwa Bungeni mjini Dodoma akichangia mjadala, ambapo alisema kwamba ‘ameoteshwa’ na Mungu.
“Mimi nimeoteshwa, kwamba Rais Magufuli asipojirekebisha atakufa,” alikaririwa akisema.
Lakini hofu ya kuupoteza ubunge kutokana na kuendelea kubaki mahabusu kwa kipindi kirefu siyo tu itamwathiri Lema na Chadema, bali hata serikali ambayo – ikiwa kweli hali hiyo itatokea – basi italazimika kutumia fedha nyingi kuandaa uchaguzi mdogo.

Comments