Featured Post

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU SIKU YA UKOMA DUNIANI JANUARI 29, 2017



Waziri Ummy Mwalimu

 TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY MWALIMU (MB) KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 29/01/2017

Ndugu wanahabari na wananchi
“Siku ya Ukoma Duniani” huadhimishwa kila mwaka, Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari. Mwaka huu maadhimisho yanafanyika tarehe 29 Januari 2017. Siku hii iliasisiwa na mwandishi wa habari mfaransa, Raoul Follereau aliyetumia muda wake mwingi kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma.


Lengo kuu la kuadhimisha siku hii ni kuukumbusha umma wa watanzania kuwa sote tunao wajibu wa kushiriki kikamilifu katika vita ya kupambana na ugonjwa wa ukoma nchini. Siku hii ni muhimu kwa jamii kukaa kitako na kutafakari madhara na shida zinazotokana na maradhi ya ukoma. Tatizo kubwa la ugonjwa huu ni kuvishambulia viungo vya mwili wa binadamu na kusababisha kukatika viungo na hivyo kupelekea ulemavu wa kudumu ambao ndio hasa huutambulisha ugonjwa huu kuliko hata dalili zake.

Ndugu wananchi na wanahabari
Maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani yanatupa fursa kama nchi kujitathmini na kuangalia harakati zetu katika kuutokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma katika Taifa letu. Kimsingi, napenda kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuwa ukoma bado upo hapa nchini kwetu na hivyo basi tuna wajibu wa kukabiliana nao. Takwimu zinatuonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa huu  kutoka kiwango cha utokomezaji cha watu 0.9  kati ya watu 10,000 mwaka 2006 na kufikia kiwango cha watu 0.4 kati ya watu 10,000 mwaka 2015. Kwa maana  nyingine katika kila watanzania 10,000 kiwango cha watu wenye ugonjwa wa ukoma sasa ni watu 0.4 mwaka 2015 kutoka wastani wa wagonjwa 0.9 katika watu 10,000 mwaka 2015. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa sababu kiwango cha kimataifa cha utokomezaji ukoma kinatakiwa  kuwa chini ya mgonjwa 1 katika watu 10,000.

Ndugu wananchi na wanahabari
Japokuwa mwelekeo wetu kama nchi unaonyesha tunapiga hatua nzuri, bado kuna wilaya na mikoa ambayo bado tatizo la ukoma lipo juu na watu wengi wanazidi kuathirika. Mikoa na wilaya ambazo bado zina wagonjwa wengi wa ukoma ni Lindi (Lindi Manispaa, Liwale, Lindi na Ruangwa), Morogoro (Halmashauri ya Ulanga, Kilombero na Mvomero), Dar es Salaam (Manispaa ya Temeke na Kigamboni), Tanga ( Halmashauri za Muheza, Mkinga  na Pangani), Mtwara (Halmashauri ya Nanyumbu na Newala), Rukwa (Halmashauri ya Nkasi), Pwani (Halmashauri ya Rufiji na Mkuranga), Geita (Halmashauri ya mji Geita na Halmashauri ya Chato), Tabora (Halmashauri ya Sikonge), Mwanza (Halmashauri ya Kwimba na Misungwi), na Ruvuma (Halmashauri ya Songea na Namtumbo). Mikoa na halmashauri hizi haina budi kuongeza juhudi za ziada na kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa ukoma kabla ya mwaka 2030 kama yalivyo malengo ya maendeleo endelevu ya dunia. Endapo tutaongeza jitihada katika maeneo haya, sina shaka kuwa nchi yetu itatokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma hata kabla ya mwaka 2030.

Ndugu wananchi na wanahabari
Ugonjwa wa ukoma unatibika na kupona kabisa. Mgonjwa akijitokeza na kugunduliwa mapema hupona vizuri bila madhara yoyote. Lakini, iwapo mgonjwa atachelewa kujitokeza na kupata matibabu mapema, atakuwa katika hatari kubwa ya kupata madhara ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu. Hivyo katika siku hii ya maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani nitoe rai kwa watu wote wanaougua ukoma nchini kwenda katika vituo vya tiba ili kupata huduma ya tiba.

Katika miaka 10 iliyopita, ugonjwa wa ukoma peke yake umeongeza idadi ya watu wenye ulemavu wa kudumu zaidi ya 2,800 hapa nchini na kwa mwaka 2015 tu, walemavu wapya wapatao 300 waligunduliwa miongoni mwa wagonjwa wapya wa ukoma, kati ya hao watoto walikuwa 26. Ulemavu unaotokana na ukoma unazuilika na hakuna sababu ya kuendelea kuona idadi kubwa ya nguvu kazi yetu inakuwa tegemezi na mzigo mkubwa kwa jamii yetu kwa sababu ya Ukoma. Tunapoadhimisha Siku ya Ukoma duniani, napenda kutoa rai kwa jamii kushiriki katika kuwabaini wagonjwa wa ugonjwa na kuwahimiza kwenda kwenye vituo vya tiba ili kuepusha ulemavu wa kudumu hasa miongoni mwa watoto.

Ugonjwa wa ukoma huchukua miaka mingi, hadi mpaka miaka 30 kati ya maambukizi hadi ugonjwa unapojitokeza na kuonyesha dalili. Hivyo tuonapo dalili za ugonjwa huu miongoni mwa watoto ni dhahiri ya kuwa ni maambukizi ya hivi karibuni na kuwa maambukizi bado yanaendelea katika jamii. Hali itakuwa mbaya zaidi kama mtoto hatagunduliwa mapema kabla ya kupata madhara ya ulemavu. Kazi kubwa iliyombele yetu sasa ni kuwaepusha watoto na ulemavu unaotokana na ukoma. Katika muktadha huu, Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”.

Kauli mbiu hii inatutaka wagonjwa wa ukoma hasa watoto wagunduliwe mapema kabla ya kupata ulemavu na hasa pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa huu. Hivyo basi, kila mmoja wetu katika maeneo ya mijini au vijijini nchini Tanzania, tujenge tabia ya kuwachunguza watoto wetu kama  wana dalili za ugonjwa huu au la. Na endapo tutabaini dalili za ugonjwa huu miongoni mwa watoto basi tuhakikishe tunawapeleke katika vituo vya kutoa tiba maramoja ili kuwezesha  ugonjwa kugunduliwa mapema kabla ya mtoto kupata ulemavu na hasa pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa wa ukoma.


Ndugu wananchi na wanahabari
Ukoma huenezwa kwa njia ya hewa toka kwa mtu anayeugua na ambaye hajaanza matibabu. Dalili za ukoma ni pamoja na baka au mabaka yenye rangi ya shaba mwilini.  Mabaka haya hayaumi wala hayawashi bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza  kujitokeza mahala popote mwilini, kuanzia kichwani hadi miguuni. Napenda kutoa wito kwa kila mtu na familia kujijengea tabia ya kujichunguza kila wakati na pale utakapoona dalili hizo nenda kituo cha huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na tiba.

Matibabu ya ukoma yanatolewa bila malipo yoyote katika vituo vyote vya huduma, vya serikali na pia vya binafsi. Serikali itahakikisha zipo dawa za kutosha na zinazopatikana kwa wakati wote na kwa kila mgonjwa wa ukoma mahali popote nchini. Tutaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma na kwa watoa huduma hususani katika maeneo ambayo bado ukoma ni tatizo kubwa.

Ningependa kutoa wito kwa halmashauri zote ambazo bado hazijafikia viwango vya utokomezaji wa ugonjwa wa ukoma kuweka katika mipango kazi yao huduma za uchunguzi wa ukoma ngazi ya kaya na hasa kuwafanyia uchunguzi wa mara kwa mara watu wanaoishi na wagonjwa wa ukoma.

Vile vile, naziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinawabaini walemavu wote, hasa wale wenye ulemavu unaotokana na ukoma na kuwaweka katika mpango wa matibabu ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kujitokeza baada ya kumaliza matibabu na kupona ukoma.

Aidha naziagiza halmashauri zote nchini kuendesha uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma kila wanapoendesha kampeni yoyote ya upimaji wa afya za wananchi katika maeneo yao. Mathalani, wakifanya kampeni ya upimaji wa mabusha, kichocho, kisukari au magonjwa mengineyo, wawapime pia na ukoma. Kwa njia hii, tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaokoa kwa kuwagundua na kuwaponyesha mapema na hivyo basi kulipunguza tatizo la ulemevu huu kama siyo kulikomesha kabisa.

Ndugu wananchi na wanahabari
Mwisho napenda kuwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wakitusaidia katika kudhibiti ukoma nchini wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Ukoma la Ujerumani (GLRA), Shirika la Madawa la NORVATIS, na Mhe. Yohaei Sasakawa, balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika harakati za kutokomeza ugonjwa wa ukoma.

Pia natoa shukrani za pekee kwa mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mama Janeth Magufuli kwa misaada ya hali na mali anayoitoa kwa walemavu walioathirika na ukoma katika makazi ya wasiojiweza sehemu mbalimbali nchini. Vile vile, natoa shukurani kwenu wanahabari kwa elimu mnayoitoa kwa wananchi kuhusu masuala mbali mbali ya uboreshaji wa afya ya watanzania, nawaomba muendelee na juhudi hizo na mshiriki pia kikamilifu kuuelimisha umma juu ya ugonjwa wa ukoma. Tulipofikia siyo pabaya lakini bado tunahitaji kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuumaliza ukoma na athari zake zote katika jamii na hasa ulemavu ambao kwa namna yoyote ile unazuilika.

Ukoma unatibika na mgonjwa kupona kabisa. Tujitokeze mapema wakati tukibaini dalili za awali ili tuchunguzwe, tutibiwe na kujiepusha kabisa na balaa la ulemavu usio wa lazima.

Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”.
Asanteni kwa kunisikiliza.
27/01/2017

Comments