Featured Post

RC NCHIMBI APIGA MKWARA: SITAKI TENA KUSIKIA MSAMIATI 'MRADI UKO CHINI YA KIWANGO



Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi akipanda viazi lishe katika shamba la Mkulima wa viazi katika kijiji cha Nkungi Wilayani Mkalama katika ziara yake wilayani humo.


Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Jakson Masaka akishiri kupanda viazi lishe katika shamba la Mkulima katika kijiji cha Nkungi Wilayani humo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida  Dkt. Angelina Mageni Lutambi akipanda viazi lishe katika shamba la Mkulima wa viazi katika kijiji cha Nkungi Wilayani Mkalama.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Mhandisi Geofrey Sanga akipanda viazi lishe katika shamba la Mkulima wa viazi katika kijiji cha Nkungi Wilayani Mkalama.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi akisadiniana na mkulima kuandaa matuta kwa ajili ya kupanda viazi lishe katika shamba la Mkulima wa viazi katika kijiji cha Nkungi Wilayani Mkalama.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Mklama wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao juu ya uadilifu na kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya hapa kazi tu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi au “mama Nchimbi” kama anavyojulikana jana amefanya ziara ya kikazi Wilaya ya Mkalama na kuagiza watendaji kusimamia miradi kwa umakini kwakuwa hataki kusikia mradi wowote uko chini ya kiwango.

Dkt. Nchimbi amesema msamiati chini ya kiwango hataki kuusikia kwakuwa umekua ukifanya watendaji kuwa wazembe na kuongeza kuwa hatua kali zitachukulkiwa kwa viongozi wote ambao hawatasimamia ipasavyo utekelezaji wa maelekezo hayo.

Ameongeza kuwa watendaji wamekuwa wakiilalamikia serikali na kuirudisha nyuma kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kupelekea wananchi kuona serikali haifanyi chochote wakati inaleta pesa nyingi za miradi mbalimbali ambapo jukumu la watumishi ni kusimamia miradi ili ifanye kazi ipasavyo.

Dkt. Nchimbi amesema viongozi wote kabla ya kusaini mikataba yoyote ya halmashauri wanapaswa kukiri thamani ya mali zao zinazohamishika na zisizohamishika ili kama mradi utatekelezwa chini ya kiwango, mali zao zitumike kufidia pesa ya serikali iliyopotea.

“Mradi wakati unajengwa Mkurugenzi, Mwenyekiti wa halmashauri na wataalam wanauangalia bila kusema chochote, ukikamilika ndio wanakuambia umejengwa chini ya kiwango, kuanzia sasa sitaki kusikia msamiati wa ‘chini ya kiwango’ na endapo ikitokea chini ya kiwango tutahakikisha fedha ya serikali inarudi", amesema Dkt. Nchimbi.

Aidha katika kikao hicho na watumishi wote wa halmashauri hiyo amewaagiza wakuu wote wa shule za msingi na sekondari kuwaruhusu wanafunzi ambao hawana sare kuanza masomo huku utaratibu wa kuwafuatilia wazazi watimize majukumu yao ukiendelea.

 “ Baada ya elimu kuanza kutolewa bure, changamoto nyingine iliyobakia kwa baadhi ya wazazi ni uwezo wa kuwashonea watoto wao sare za shule, sasa ninaagiza wakuu wa shule za sekondari na Msingi wote Wilayani hapa kuwaruhusu watoto hao waingine madarasani hata kama hawajavaa sare za shule ili wasikose haki yao ya msingi kwa sababu ya sare tu”, ameagiza Dkt. Nchimbi.

Awali kabla ya kuzungumza na watumishi Dkt. Nchimbi alifanya ziara katika mashamba ya wakulima ili kujionea na kushiriki na wananchi shughuli za kilimo hasa mashamba ya viazi katika kijiji cha Nkungi na mashamba ya mtama katika kijiji cha Ilunda wilayani humo.

Dkt. Nchimbi akiwa katika shamba la mkulima wa viazi lishe katika kijiji cha Nkungi alipanda viazi na kuhamasisha wananchi wengine walime mazao ambayo yanatumia maji kwa ufanisi kama vile viazi, mihogo, matama na uwele kutoka na mabadilike ya tabia nchini ili kujihakikishia uwepo wa chakula.
  
Amewataka watendaji hasa wa kada za kilimo na ufugaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea hasa kuandaa taarifa za makaratasi bali wawatembelee wakulima na wafugaji katika maeneo wanayofanya shughuli zao ili waweze kutoa ushauri kwa kupata picha halisi.

“Sipendi kiongozi anayesema yupo karibu na wananchi kwa sababu hatuwezi kupima ukaribu uliopo hivyo ni vyema kuanzia sasa tuache kuwa karibu na badala yake tuwe pamoja nao”, amesema Dkt. Nchimbi. 

Comments