RAIS WA RT AMPONGEZA RAIS WA TFF KUTEULIWA MJUMBE KAMATI YA MAENDELEO FIFA Jamal Malinzi

 DAR ES SALAAM, JANUARI 20, 2017; 
 RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, amempongeza Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kwa kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).


 Kwa mujibu wa taarifa ya Fifa ya Januari 18, 2017, iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura, Malinzi ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo kuanzia  mwaka huu 2017 hadi 2017.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, Kamati hiyo inaongozwa na Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Asia, ina majukumu ya kusimamia mipango ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani kote.

Nikiwa Rais wa RT, nachukua nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Malinzi kwa kuaminiwa kwako Fifa na kuteuliwa katika nafasi hiyo, uteuzi ambao unaongeza heshima ya taifa letu katika medani ya michezo.
RT inakuahidi Bw. Malinzi kuwa tutakupa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji mwema wa majukumu yako, ndani na nje ya kamati hiyo, ili kuendelea kujenga taswira nje kwa shirikisho lililokuamini na kukupa jukumu hilo.

Naamini Fifa haijakosea kukupa ujumbe wa kamati hiyo, kwani umekuwa na taswira za kimaendeleo, kama ulivyothibitisha katika harakati zako za kukuza soka la Tanzania katika kipindi kifupi cha uwepo wako madarakani.

Nakutakia kila la kheri katika nafasi mpya, tukiamini kwa pamoja tutashirikiana nawe katika majukumu yako kama mjumbe wa kamati hiyo muhimu ya Fifa.

Ahsante

Anthony Mtaka

Rais RT na
Mjumbe Kamisheni ya Mipango, Ushauri, Mawasiliano na Mikakati Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF)

Januari 20, 2017