Featured Post

MAUAJI YA ALBINO - 1: NILIPAMBANA, NIKASIKIA PA! KICHWANI, NILIPOZINDUKA KIGANJA CHA BARAKA KILIKUWA KIMEKATWA

 Picha ya Baraka Cosmas
 Mtoto Baraka (6) akilia kwa maumivu makali wakati akiuguza mkono wake katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kitanga.



 Picha ya Prisca Mama Baraka

Bi. Prisca Mpesya akiwa na jeraha kichwani na mimba ikimuelemea huku mgongoni amembeba mwanawe Lucia (3) wakati akimuuguza mwanaye Baraka ambaye alikatwa kitanga cha mkono kwa kuwa tu ni albino. (PICHA NA DANIEL MBEGA/MAENDELEOVIJIJINI BLOG)

Na Daniel Mbega, Sumbawanga
PRISCA Shaaban Mpesya (29), mkazi wa Kitongoji cha Kikonde, Kijiji cha Kaoze katika Kata na Tarafa ya Kipeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, alikuwa analia kimya kimya.
Alimtazama mwanaye Baraka (6) aliyening’iniza mkono wa kulia huku akilia kwa maumivu baada ya kukatwa kitanga cha mkono na ‘watu wasiojulikana’ wanaosaka utajiri, kwa sababu yeye ni albino na wanadai viungo vyake ni ‘dili’.

Kwa Prisca, kuzaa watoto wenye albinism inaonekana ni majanga kwake na kizazi chake, hasa katika kipindi ambacho matukio ya mauaji, kutekwa nyara na kukatwa viungo vya albino yameshamiri Tanzania na Afrika Mashariki na Kati.
Anajaribu kukumbuka tukio hilo la usiku wa Jumamosi, Machi 7, 2015 alivyonusurika kufa yeye na mwanaye Baraka.
“Nilikuwa natoka nje kwenda kujisaidia, sijui ilikuwa saa ngapi kwa sababu sikuwa na saa, nje juu ya mlango tuliweka taa ya Mchina ya solar ambayo ilikuwa inaangaza, hivyo sikuwa na hofu,” ndivyo anavyoanza kumsimulia mwandishi wa MaendeleoVijijini wakati alipokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Anasema ghafla tu alipofika mlangoni akashtuka kuona mtu akija mbio, akaipiga taa na kuivunja, kukawa giza.
“Nikajua huyu hakuwa mwema, hivyo nikajiandaa kupambana naye, alikuwa mwanamume mwenye nguvu kunishinda, lakini nilimdhibiti kwa sababu alitaka kuingia ndani kwa nguvu nami sikutaka kwa sababu wanangu walikuwa wamelala chini angeweza kuwaumiza.
“Mara nikasikia kitu kikinipiga kichwani pa! Nikaanguka na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nikamwona mwanangu Baraka analia, kitanga cha mkono kimekatwa.” Akaongeza: “Natamani watu wanaofanya mambo haya wauawe hadharani.”
 michirizi ya damu
 Michirizi ya damu na alama za panga mahali ambapo Baraka alikatwa kiganja wakati akiwa amelala na ndugu zake.
 daniel mbega
 Mwandishi wa makala haya (mwenye jezi nyekundu na kofia la sweta) akiwa katika eneo la tukio pamoja na wanausalama.
 nyumba ya akina baraka
 Nyumba ya Cosmas Songoloka, baba wa Baraka, mahali tukio lilipofanyika.

Anasema, mumewe Cosmas Yoramu Songoloka hakuwepo kwani alikuwa ameaga tangu mchana kwamba anakwenda kilabuni kunywa pombe, na mpaka majira hayo hakujua kama alikuwa kilabuni ama alikwenda kwa mke mdogo ingawa haikuwa zamu yake.
Baraka Cosmas Yoramu alikatwa kitanga cha mkono wa kulia na watu ‘wasiojulikana’ Machi 7, 2015 majira ya saa 2 usiku kwa imani za kujipatia utajiri wa kishirikina.
Jitihada za kupata tiba katika kituo cha afya Kamsamba wilayani Sumbawanga zilishindikana, hivyo kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Prisca anasema, pamoja na ujauzito aliokuwa nao wakati huo, lakini hakuhisi chochote zaidi ya kuwalinda wanawe, zawadi pekee aliyopewa na Mwenyezi Mungu.
“Nimehangaika na mimba zao kwa nyakati tofauti, sikuwa tayari kuona wanapata madhara, ndiyo maana niliisahau hata hali yangu nikaamua kupambana,” anasema.
Maumivu ya jeraha lake la kichwani alilopata kwa kupigwa na ‘kitu kizito’ yalionekana siyo kitu kwa wakati huo, kwa sababu binti yake Lucia (3) ambaye ana albinism pia alikuwa anamsumbua hospitalini, na kwa umri wake, alikuwa hajui kinachoendelea.
Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mwanaye mchanga wa kiume aliye albino, ambaye ndiyo kwanza alikuwa ametoka kujifungua, naye alikuwa analia akitaka kunyonya.
Sasa anao watoto watatu wenye albinism kati ya wanne, akiwemo huyo mdogo ambaye kwa sasa ametimiza mwaka mmoja na nusu tangu alipozaliwa Aprili 2015 kwenye Hospitali ya Rufaa Mbeya wakati akiuguza jeraha lake kichwani pamoja na kumuuguza mwanaye Baraka jeraha la mkono.
Bi. Prisca alifikishwa hospitalini hapo Machi 8, 2015 huku akiwa amembeba mwanaye Lucia na mimba ya miezi karibu nane ikiwa imemuelemea.
“Nisingeweza kumwacha Lucia kule porini kwa sababu watu wabaya wangeweza kumjia,” alisema.
Mtoto wake mkubwa, Shukuru (8), alimwacha kijijini wakati mumewe Cosmas akiwa mahabusu kuhusiana na tukio hilo.
Mwandishi wa MaendeleoVijijini, ambaye amefanya utafiti wa mauaji ya albino kwa miezi nane mfululizo, alibahatika kuongozana na polisi katika msako wa ‘watu hao wasiojulikana’ kwenye matukio yaliyotokea mwaka 2015 likiwemo la kukatwa kiganja mtoto Baraka, ambapo alipiga kambi mjini Sumbawanga kwa takriban miezi miwili na kushuhudia maofisa wa polisi walivyowakamata wahusika wa tukio hilo, akiwemo Sajenti Kalinga Malonji, ‘tajiri’ ambaye ndiye aliyepelekewa kiganja hicho na kuahidi kuwapatia wenzake mamilioni ya fedha.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesha kwamba, haikuwa kazi rahisi kuwapata watuhumiwa, na hasa ‘tajiri’ mwenyewe, Sajenti, mkazi wa Kijiji cha Hanseketwa wilayani Mbozi mkoani Songwe, kwani mwanahabari huyu, akiongozana pia na maofisa hao wa polisi, walikesha kwa siku tatu mfululizo wakimsaka mtuhumiwa jijini Dar es Salaam na hatimaye saa 8:30 usiku wa kuamkia Aprili 25, 2015 akatiwa mbaroni na kurudishwa kijijini kwake kuonyesha kilipo kitanga hicho cha mkono.
 kitanga
 Kitanga cha mkono wa Baraka kikiwa kimeoza na kutoa funza baada ya kupatikana.
 sajenti malonji
 Mtuhumiwa Sajenti Kalinga Malonji akiwa na pingu mkononi baada ya kukishusha kitanga cha mkono wa Baraka ambacho alikuwa amekificha juu ya mti nyumbani kwake katika Kijiji cha Hanseketwa wilayani Mbozi mkoani Mbeya. Hii ni baada ya kukamatwa na wanausalama jijini Dar es Salaam na kwenda kukionyesha kiganja hicho.

Alikuwa amekificha juu ya mti, nje ya nyumba yake, na Aprili 26, 2015 majira ya saa 4:00 asubuhi, mbele ya viongozi wa kijiji na wananchi mbalimbali, akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha, alipanda mwenyewe juu ya mti na kukiteremsha chini. Tayari kilikwishaoza na kutoa funza.
Sajenti Kalinga, ambaye alitajwa na watuhumiwa wenzake waliokuwa mahabusu, akaunganishwa kwenye kesi hiyo pamoja na baba wa mtoto, Cosmas, Andius George Songoloka (mdogo wa Cosmas), Unela Jiloya Shinji Kuwilu Seme (anayedaiwa kukiri polisi kwamba ndiye aliyekata kiganja na ndiye aliyewaongoza polisi hadi kumkamata ‘tajiri’ Kalinga), na Mihambo Kanyenga Kamata maarufu kama Bichi (ambaye ni mganga wa jadi).
Mtuhumiwa mwingine Mwendesha William Mola alifutiwa mashtaka kwa utaratibu wa Nolle Prosequi katika kesi hiyo ambayo iko katika Mahakama Kuu, Sumbawanga.
Kalinga aliwaeleza wanausalama mara baada ya kukamatwa kwamba, yeye aliambiwa na mtu mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama) kuwa kuna ‘mzungu’ anataka mkono wa albino.
“Aliniambia kwamba, wazungu wenyewe ni wale Wachina wanaotengeneza barabara. Lakini tangu nikipate kiganja, nimekuwa nikimpigia simu yake haipatikani,” alikaririwa akisema.
Aidha, alisema hata kwenda kwake Dar es Salaam ilikuwa ni katika harakati za kutafuta wateja, ambao hakuwapata hadi alipotiwa mbaroni.
 Esther Jonas amelala hajitambui baada ya kupigwa panga usoni na kunusurika kifo wakati akipambana na watu waliomnyang'anya mwanawe Yohana.
Kisa cha Prisca hakina tofauti na kile cha Esther Jonas (31), mkazi wa Kitongoji cha Ilyamchele, Kijiji cha Ilelema, Kata ya Ipalamasa, Tarafa ya Buseresere wilayani Chato, ambaye Februari 15, 2015 saa 1:00 usiku alinyang’anywa mwanaye Yohana (1), mwenye albinism, ambaye alikuwa amembeba mgongoni.
Katika jitihada za kunyang’anyana mtoto ndipo ‘watu hao wasiojulikana’ wakamkata panga usoni, akadondoka chini na kupoteza fahamu huku akivuja damu nyingi.
Wakati tukio linatokea, mumewe, Bahati Misalaba Malyamchele (40) alikuwa anaota moto kwenye kikome, nje ya nyumba yao, na hakuweza kutoa msaada kwa mkewe ambaye aliendelea kupambana na watu hao kabla ya kumdhibiti kwa kumkata kwa panga usoni.
Watu hao wakaondoka na mtoto Yohana na kutokomea kusikojulikana huku mama huyo akikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza ambako ndiko walikonusuru maisha yake ingawa naye wamemwacha na ulemavu wa kudumu.
Lakini Februari 17, 2015 mwandishi wa makala haya alishuhudia polisi, wakiongozwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Joseph Konyo, pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, SP P. J. Kayumba, walipofanikiwa kuupata mwili wa marehemu Yohana ukiwa hauna mikono wala miguu.
Ni rahisi kutazama kuku aliyenyonyolewa manyoya na kukatwa vipapatio na miguu, lakini ni vigumu kukodolea macho kiwiliwili cha binadamu kikiwa katika taswira hiyo. 
Maiti ya Yohana Bahati baada ya kufukuliwa
Maiti ya marehemu Yohana Bahati baada ya kufukuliwa shambani. (Kunradhi kwa picha hii, lakini maudhui ya kuchapishwa kwake yamelenga kuonyesha unyama na ufedhuli unaofanywa na majahili wanaotafuta utajiri kwa njia za mkato kwa kuwaua ndugu na jamaa zetu albino).
Mwili huo ulikuwa umefukiwa katika shamba la mtu mmoja, Malunguzya Kerezia, katika Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha Lumasa, yapata kilometa 15 kutoka Kitongoji cha Ilyamchele, Ilelema ambako Yohana alikuwa akiishi na wazazi wake.
Katika tukio hilo, wananchi waliodai kuchoshwa na matukio hayo ya mauaji na kujeruhi watu wenye albinism, waliamua kwenda kuchoma nyumba ya mwanakijiji mmoja, Juma Lupemba Kilobelo (39), ambaye walimhisi kuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo, Yohana hakuwa mtoto pekee wa Esther mwenye albinism, kwani kati ya watoto wake saba aliokuwa nao, ni Kulwa na Doto (14), Hoja (10) na Mathias (8) tu ambao hawana ulemavu wa ngozi, lakini Shija (12) na Tabu (6) nao ni albino ambao kama wengine, maisha yao yako hatarini.
Kwa ujumla, Yohana hawezi kurudishiwa uhai wake, ingawa baadhi ya waliopata majeraha na ulemavu wa kudumu, wameweza kupatiwa viungo bandia walau ili waweze kumudu maisha.
Mwaka 2015, Baraka na watoto wengine albino waliopoteza viungo vyao kwa vitendo hivyo vya kikatili, walipelekwa jijini New York, Marekani kupitia Global Medical Relief Fund, mfuko wa hisani ulioanzishwa na mwanamama Elissa Montanti wa Kisiwa cha Staten mwaka 1997 ili kuwapatia msaada wa viungo vya bandia watu kutoka maeneo yenye migogoro.
 albino marekani
 Albino wa Tanzania wakikatiza mitaa ya New York, Marekani wakiwa na Elissa Montanti ambako walikwenda kuwekewa viungo vya bandia.
Baraka na Mwigulu Matonange
 Baraka (kulia) akimuonyesha rafiki yake Mwigulu Matonange mkono wake wa bandia wakati wakiwa Marekani.

Watoto wengine walikuwa Kabula Nkarango Masanja (17), Mwigulu Magesa Matonange (12), Emmanuel Festo Rutema (14) na Pendo Sengelema Noni (17).
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Kabula Nkrango Masanja, mkazi wa Luhaga, Kahama mkoani Shinyanga, alikatwa mkono wa kulia mwaka 2010 ambapo kesi yake ilikuwa na jalada lenye Kumb. KAH/IR/1770/2010.
Hata hivyo, baada ya kesi hiyo kusikilizwa, watuhumiwa wote watatu – Magobo Njige (56), Senga Mabirika (35) na Bupina Mhayo (43) wote wakazi wa Ilalwe, Ushirombo, waliachiliwa huru na Mahakama Kuu.
 mwigulu matonange
 Mwigulu Magesa Matonange akifanya mazoezi na kiungo cha bandia.

Mwigulu Magesa Matonange, mkazi wa Kijiji cha Nsia, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga, yeye alikatwa mkono wa kushoto wakati akiwa machungani.
Shauri hilo lenye majalada yenye Kumb. SUM/681/2013 na PI 13/2013 linawakabili washtakiwa 10 ambao ni Kulwa Mashiru, Peter Saidi Msabato, Ignas Sungura, Faraja Jailosi Mwezimpya, James Patrick Ngalamika, Weda Mashilimu, Ibrahim Tella, James Paschal, Nickson Ngalamika maarufu kama Kadogoo na Hamis Rashid Manyanywa.
Kumbukumbu za mahakama na polisi zinaonyesha kwamba, mtuhumiwa Manyanywa pia anakabiliwa na kesi ya mauaji ya Lugolola Bunzari (7), albino na mkazi wa Kitongoji cha Kinondoni, Kata ya Kanoge, Tarafa ya Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, mauaji ambayo yalitokea mwaka 2013.
Kesi hiyo iliyopewa majalada yenye Kumb. ULY/IR/45/2013 na MC 12/2013, inawahusisha watuhumiwa wengine ambao ni Simon Said Ndimawasha, Amon Ruben maarufu kama Anthony Mnembotoyi na Laurent Batakanywa Malembo, ambaye inaelezwa kwamba ndiye aliyekwamisha kusikilizwa kwa kesi hiyo baada ya kuugua ugonjwa wa akili na kupelekwa katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ya Mirembe, mjini Dodoma. Kesi hiyo iko Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na ilikuwa ianze kusikilizwa tangu Januari 2015.
Kwa upande mwingine, Pendo Sengelema Noni, mkazi wa Ugasa, Kata ya Usinge, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono wa kulia mwaka 2014.
Shauri hilo lililopewa majalada yenye Kumb. KAU/IR/835/2014 na CC. 63/2014 kwa kosa la ‘Kujaribu Kuua’, washtakiwa ni John Fumbuka na Maduka Nzuki, ambapo kesi hiyo inasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili jalada lipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
Emmanuel Rutema, mkazi wa Isebya, Kagoma wilayani Biharamulo, alikatwa mkono wa kushoto katika tukio lililotokea Jumatatu, Novemba 12, 2007 majira ya saa 1:30 usiku.
Mtuhumiwa Zacharia Petro (37), kabila Muha na mkazi wa Songambele – Kagoma, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kujaribu kuua. Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 4, 2011.
Wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Joseph Konyo, alisema, katika matukio mengi ya mauaji, kujeruhiwa na kutekwa nyara kwa albino, wahanga wakubwa ni wanawake ambao mara kadhaa hupambana ili kuwalinda ndugu ama watoto wao wenye albinism.
“Taarifa za kipelelezi zinaonyesha kuwa wanaume, wakiwemo wazazi na ndugu wa albino, ndio wanaohusishwa moja kwa moja kwa ama kupanga njama ama kushiriki vitendo hivyo,” alisema.
Alitolea mfano wa Bi. Esther Jonas, mama wa marehemu Yohana, jinsi alivyopambana na majahili kiasi cha kunusurika kupoteza uhai wake kabla ya wauaji hao hawajampora mtoto mgongoni na kwenda kumuua na kumkata viungo huku mumewe, ambaye alikuwa nje, akishindwa kutoa msaada wowote.
Kumbukumbu za kipolisi pia zinaonyesha kwamba, katika tukio la kutekwa nyara kwa mtoto Pendo Emmanuel Nundi huko Kwimba usiku wa Desemba 27, 2014, mama wa binti huyo ndiye aliyeonekana kupambana na watu hao waliovunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa (maarufu kama Fatuma) na kwenda kunyakua na kutokomea naye kusikojulikana.
Licha ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza wakati huo, SACP Valentino Mlowola (sasa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru), kutangaza dau la Shs. Milioni 3 kwa atakayetoa taarifa za kufanikisha kukamatwa kwa majahili na kupatikana kwa Pendo, lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote.
Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, wananchi bado wanabeza utendaji kazi wa vyombo vya dola wakisema hauonyeshi dhamira ya dhati ya kukomesha mauaji hayo.
“Serikali inaonekana haina dhamira ya dhati ya kukomesha mauaji haya, mbona tunasikia watu wamehukumiwa kunyongwa lakini hawanyongwi?” anahoji Petro Shija, mkazi wa Katoro wilayani Geita.
Shija anaongeza: “Matukio ya mauaji na kujeruhiwa kwa albino yanatishia usalama wa Watanzania wenzetu, ndugu zetu, wenye ulemavu wa ngozi na jamii kwa ujumla, kwa sababu wahusika wanaondoa roho za watu wasio na hatia huku wakiwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.”
Kauli ya Shija haina tofauti na ya Bi. Limi Lupamba, mkazi wa Kachwamba wilayani Chato, ambaye anasema kama serikali ingewanyonga wale waliopatikana na hatia ingeweza kuwatia hofu wengine ambao watafanya ama wanataka kufanya vitendo hivyo.
“Hawa watu wanyongwe tu, maana hata huko jela wanamaliza ugali wa bure,” anasema Limi.
Gerald Ruhere ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) mkoani Geita, ambaye anabainisha kwamba, lazima jamii ifike mahali na kubadilika kutokana na imani potofu kuwa viungo vya albino vinaleta utajiri au madaraka.
“Huu wote ni ujinga tu, inawezekanaje kiungo cha binadamu mwenzako kikakupatia utajiri, kama ni hivyo, yeye mwenyewe si angekuwa tajiri zaidi?” anasema.
Anahimiza kwamba, ni wajibu wa serikali pamoja na taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa jamii ili kuachana na imani hizo potofu na kuwataka wanajamii kuwa na hofu ya Mungu, kwani kuwanyonga wahusika tu hakuwezi kuwa suluhu ya tatizo lenyewe.
Wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wenye albinism duniani jijini Arusha Juni 13, 2015, Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliahidi kwamba angesaini hukumu ya kunyongwa kwa washtakiwa wa mauaji ya albino.
“Kati ya watu waliohukumiwa kunyongwa, wawili kesi zao ziko katika hatua ya mwisho kufikishwa kwangu, zitakapofika mezani kwangu nitazitendea haki stahiki,” alisema na kuonya kwamba, masuala hayo yanapaswa kuwa na subira.
Baadhi ya wananchi wanaeleza kwamba, mara baada ya Rais wa Tanzania kuchaguliwa, huwa anatoa kiapo kuilinda, kuitetea na kuitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo mojawapo la kikatiba likiwa kuidhinisha kutekelezwa kwa hukumu ya kifo inapotolewa na mahakama.
“Kuidhinisha hukumu ya kifo ni jambo ambalo marais karibu wote wa Tanzania wamekuwa wanakataa kulifanya,” anaeleza Kassimu Machimu, mkazi wa Kahama.
Machimu anasema, ingawa hapendezwi na hukumu za kifo kwa ujumla, lakini yuko radhi kuona washtakiwa wa mauuaji ya albino nchini wakinyongwa kwani kitendo wanachokifanya ni cha kinyama.
“Watanzania tumeshuhudia jinsi ndugu zetu albino wanavyouawa au kukatwa viungo kikatili na hawa watu kwa sababu ya kutafuta utajiri kwa njia za kishirikina… Kama Nyerere aliudhiwa sana na kifo cha Dk. Kleruu hadi kuidhinisha hukumu ya kifo bila kusita, ni wajibu wa rais wetu kusaini hukumu hizo ikiwa kweli naye anaudhiwa na mauaji haya ya albino.
“Mimi na Watanzania wenzangu, na dunia kwa ujumla, tunaudhiwa sana na ukatili huu dhidi ya albino. Hivyo tungependa kutoa ujumbe kwamba jambo hili linatuchukiza Watanzania kiasi kwamba hatusiti kuidhinisha hukumu ya kifo kwa wauaji, japo tunaweza tukawa hatuipendi hukumu ya kifo kwa ujumla. Tunataka kufanya hivi ili pia iwe ujumbe kwa wale wote wenye mawazo ya kudhuru ndugu zetu albino, kwamba tukiwashika, tutawanyonga hadi kufa,” anasema.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya sheria wanasema, suala la kusaini hukumu ya kunyongwa ni la kisheria linaloambatana na haki za binadamu, hivyo linahitaji kuchukuliwa kwa uzito unaostahili, huku wafungwa hao wakipewa haki ya kukata rufaa kupinga hukumu hizo.
Lakini kutosainiwa kwa hukumu hizo kumeendeleza ‘msimamo’ wa kutoidhinisha vifo wa wakuu wa nchi, akiwemo Mwalimu Julius Nyerere, ambaye katika utawala wake anadaiwa kusaini hukumu moja ya Said Mwamwindi, ambaye alimuua kwa risasi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kleruu na kwenda kuikabidhi maiti yake kituo cha polisi.

Waliohukumiwa kifo
Mpaka Kikwete anakabidhi madaraka Novemba 5, 2015, jumla ya washtakiwa 24 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya watu nane wenye albinism tangu mauaji hayo yalipoibuka mwaka 2006.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi katika kipindi cha miezi nane unaonyesha hata hivyo kwamba, mmoja kati ya waliohukumiwa kunyongwa alifia mahabusu wakati kesi ikiendelea.
Hukumu ya mwisho dhidi ya wauaji hao ilitolewa Septemba 16, 2015 na Jaji Robert Makaramba wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ambapo washtakiwa watano walihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Aaron Nongo, mkazi wa Ibanda-Relini jijini Mwanza.
Mwandishi wa makala haya alihudhuria kesi hiyo kwa siku tano mfululizo jijini Mwanza kabla ya kutolewa hukumu, ambapo ilielezwa mahakamani kwamba, marehemu Nongo aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake Ibanda-Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na kisha kumkata miguu yake yote miwili kwa kutumia shoka na kutoweka nayo pamoja na meno mawili ya mbele.
Waliokumbwa na adhabu hiyo katika shauri hilo Namba 213 la mwaka 2014 lenye kumbukumbu namba MWZ/IR/5397/2009 na MCC No. 32/2009 ni Chacha Jeremia Mlimi, Mathew Jeremia Mlimi (mdogo wa Chacha), Paschal Lugoye Mashiku na Joseph Bugwema au Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola Jangalu.
Mshtakiwa mwingine, Paulo Lumanija Genji alifariki katika mahabusu ya Magereza, wakati ambapo mganga wa jadi Kishosha Lutambi, ambaye anadaiwa kuchochea mauaji hayo, alifariki kufuatia kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira mwaka 2009.
Wakati wa usikilizaji wa mwenendo wa kesi hiyo, shahidi wa sita wa upande wa mashtaka, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (wakati huo akiwa Mkaguzi wa Polisi) David Mhanaya, Mei 12, 2015 aliifanya mahakama izizime kwa hofu na simanzi baada ya kutoa mfupa wa mguu wa marehemu ambao uliwasilishwa kama kielelezo mahakamani hapo baada ya kuthibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ndio wa marehemu Nongo.
Hukumu hiyo ilitolewa takriban miezi mitatu na nusu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kuwahukumu wengine wanne kunyongwa mpaka kufa.
Hukumu ya kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008 na PI 5/2013, ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Dk. Revila Jumanne, Juni 30, 2015 jijini Mbeya, ambapo washtakiwa wanne kati ya watano walihukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na mauaji ya kijana Henry Mwakajila (17) aliyekuwa na albinism.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Dk. Revila alisema mahakama ilijiridhisha pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba washtakiwa hao wanne walitenda kosa hilo na hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa ni mganga wa jadi Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga na Gerard Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje), na Leonard Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem Mwakalinga (wakazi wa Kiwira wilayani Rungwe).
Mshtakiwa wa nne, Mawazo Philemon Figomole, mkazi wa Kiwira wilayani Rungwe, aliachiliwa huru na mahakama hiyo baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushiriki wake katika mauaji hayo.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Februari 5, 2008 majira ya saa 12:00 na saa 1:00 jioni huko katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, washtakiwa hao walimteka nyara kijana Henry Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa mwenendo wa kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa wa kwanza Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya Ileje, alikutwa na utumbo unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.
Mshtakiwa wa pili, Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje alikutwa na vidole vinne na mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu na baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika kwamba ni viungo vya marehemu Henry.
Ilielezwa pia kwamba, washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon Figomole na Hakimu Mselem Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto huyo na kumuua, kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa wa tano, Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa mpaka kufa katika kesi nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Mei 19, 2011.
Inadaiwa kwamba, chanzo cha mauaji ya Mwankenja, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe, kilitokana na kiongozi huyo kufahamu kwamba hao ndio waliomuua albino Henry, na alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mshtakiwa Mwakalinga, ambaye ndiye aliyetekeleza mauaji ya Mwenyekiti huyo wa Halmashauri, alitajwa na washatakiwa wanne ambao tayari walikuwa mahabusu, hivyo akaamua kwenda kumuua kiongozi huyo ili kupoteza ushahidi akitumia bunduki ambayo ilidaiwa kuibwa nchini Zambia.
Hata hivyo, makachero wa Jeshi la Polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo na mbali ya kushtakiwa kwa mauaji ya mwenyekiti wa halmashauri, aliunganishwa pia kwenye kesi ya mauaji ya Mwakajila.
Hukumu ya kesi ya mauaji ya mwenyekiti wa halmashauri iliyokuwa na kumbukumbu Namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013 ambapo ilielezwa kwamba watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika Kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
Ingawa watuhumiwa walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya Jaji Samwel Karua iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza Hakimu Mwakalinga na mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo kwamba walihusika moja kwa moja na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji wakati mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika mauaji hayo ingawa hakuhusika na kitendo hicho moja kwa moja, hivyo wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa katika kesi nyingine kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, hukumu ya kwanza kabisa ya kunyongwa mpaka kufa katika mfululizo wa kesi za mauaji ya albino ilitolewa Januari 2, 2009 ikihusisha Shauri namba MCC 25/2008 na BAR/IR/2460/2008 la mauaji ya Lyaku Willy (50) wa Bariadi, ambapo washtakiwa wote wanne Mboje Mawe, Nchinyenye Kishiwa, Sayi Gamaya na Sayi Masizi walihukumiwa kunyongwa.
Washtakiwa Masumbuko Madata, Charles Karamji na Merdard Maziku walihukumiwa kunyongwa katika kesi mbili za mauaji ya albino, ya kwanza ikiwa ya Esther Charles (10) wa Shilela wilayani Kahama na Matatizo Dunia (13) wa Bunyihuna, Ushirombo, mkoani Geita, mauaji yote yakiwa yametokea mwaka 2008.
Katika Shauri la mauaji ya Esther Charles lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba KAH/IR/433/2008 washtakiwa wake Masumbuko Madata, Charles Karamuji na Merdard Maziku walihukumiwa Juni 3, 2011 na baadaye mwaka huo 2011 wakahukumiwa tena kunyongwa mpaka kufa katika Shauri la mauaji ya Matatizo Dunia lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba USH/IR/1879/2008. Marehemu Matatizo alikatwa mguu wa kulia ambao polisi waliukuta nyumbani kwa Masumbuko Madata.
Katika Shauri lenye jalada namba MCC No. 01/2007 la mauaji ya Mariam Emmanuel wa Kijiji cha Nyangomango wilayani Misungwi, washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa ni Kazimili Mashauri na Mathias Ikangalange. Tukio la mauaji hayo lilitokea Januari 21, 2007 majira ya saa 2:30 usiku katika kijiji hicho cha Nyangomango.
Shauri namba MCC No. 10/2008 la mauaji ya Zawadi Mgindu wa Kijiji cha Nyamalulu, Kata ya Imalambegete mkoani Geita aliyeuawa Machi 11, 2008 ndilo lilikuwa la kwanza kutolewa hukumu kama hiyo mwaka 2015 ambapo washtakiwa Nassoro Said Isakwisa, Singu Siyantemi, Masalu Kahindi na Ndahanya Lumola Ndahanya walihukumiwa kitanzi Machi 5, 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita.
Hukumu nyingine ya kunyongwa mpaka kufa ilitolewa Juni 15, 2015 katika Shauri lenye jalada namba MCC No.28/2009 la mauaji ya Jesca Charles Joshua wa Shamaliwa-Igoma jijini Mwanza aliyeuawa Juni 21, 2009 ambapo washtakiwa waliopewa adhabu ya kifo ni Malikiadi Christopher Manumbu na Yohana Maduka Mwanamalundi.
Fuatilia mfululizo wa ripoti hii maalum: Kuwanasa wauaji wa albino, hata mbinu za kivita zinatumika.

+255 656-331974

Comments