MAJANGA DODOMA: NIMEPOTEZA NDUGU WATATU KATIKA MAFURIKO MPWAPWA!!Hii ndiyo nyumba ya marehemu Martha Mbega ambayo imesombwa na maji na kusababisha maafa makubwa.

MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo mjini Mpwapwa imenifanya nipoteze ndugu watatu kufuatia nyumba waliyokuwa wamelala kusombwa na mafuriko.
Waliofariki ni Martha Mbega (62) ambaye ni mtoto wa kaka yangu, na wajukuu zake wawili wa kike Shukuru Chinyanya (16) na Bernadeta Mabula (6).

Nimeambiwa kwamba maiti zote, ikiwemo nyingine ya mwanamke ambaye hakuweza kufahamika mara moja, zimepatikana na zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Mpwapwa.
Wajukuu wengine wawili wa marehemu (kwangu mimi ni vitukuu), Beka Ulanga (11) na Joseph Mabula (8) walinusurika baada ya kufanikiwa kukimbia, ambapo inaelezwa kwamba, Joseph alikutwa akiwa amekwea mti yapata kilometa mbili kutoka eneo la tukio huku mwenzake akikimbilia  kwenye nyumba ya jirani umbali wa meta 800.
Mume wa marehemu hakuwepo wakati wa tukio hilo, kwani alilala kwa mke mdogo.
Nimezungumza kwa simu na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mpwapwa (OCD) Mohammmed Rama Mhina ambaye amenithibitishia tukio hilo na kusema bado wanaendelea kupokea taarifa zaidi.
“Kwa sasa tunaweza kusema ni vifo hivi vinne tu pamoja na nyumba ya Mzee Mabula (mume wa marehemu Martha Mbega) ambayo imesombwa, lakini bado hatujasikia zaidi ya hayo,” alisema kamanda Mhina.