LINDI ILIVYOELEMEWA NA WAGONJWA WA MACHO

Dk Mwita Machage akimchoma sindano maalumu mgonjwa, tayari kwa kuanza operesheni wakati akiwa kwenye mafunzo katika Hospitali ya KCMC, Kilimanjaro.

NA KENNEDY KISULA
“UMASIKINI wa kipato, kuamini tiba za kienyeji zisizo sahihi au kushiriki kwenye imani za kishirikina ni vitu vinavyowaweka katika hatari ya kutoona kabisa watu wenye matatizo ya macho mkoani Lindi, ikiwemo presha ya macho.”
Hayo yanasemwa na mratibu wa macho wa mkoa na mganga wa ugonjwa huo katika hospitali ya Rufaa ya Sokoine mkoani Lindi, Dk Mwita Machage, alipofanya mazungumzo na mwandishi wa makala haya hivi karibuni. Dk Machage anasema kwamba hali ni mbaya kwa jamii kwa kuwa kuna baadhi yao hawana tena uwezo wa kupona, kwa maana nyingine wameshakuwa vipofu.

Akitoa takwimu, Dk Machage anasema wagonjwa wenye presha ya macho na wale wa mtoto wa jicho (cataract) ambao wanahitaji kupatiwa huduma ya kufanyiwa operesheni kubwa ya macho wako takribani 854. Anasema kwamba licha ya kuhitajika kupatiwa huduma ndani ya wakati, wengi wao hawana fedha za matibabu. Anasema idadi inaweza kuwa kubwa kuliko hiyo kwani wengi hawafiki hospitalini.
“Kuna wengine hawafiki hospitalini lakini wanasumbuliwa na macho. Wanaamua tu kukaa kimya au kufanya utaalamu wanaoujua wao wenyewe,” anasema. Anasema kuwa kati ya mwezi Januari na Desemba mwaka jana hospitali hiyo iliorodhesha jumla ya wagonjwa 8,888 wenye matatizo ya macho. Anasema mbali na umasikini wa kipato, imani za kishirikina miongoni mwao ni jambo ambalo limetawala pia ambapo mtu anadhani amerogwa macho na hivyo kuliwa pesa zake na waganga matapeli badala ya kwenda hospitali.
Anasema kuna mgonjwa kutoka mtaa wa Tulieni katika Manispaa ya Lindi, alishaanzishiwa matibabu lakini mara alikatisha huduma hiyo na kwenda kwa mganga wa kienyeji. Anasema taarifa alizopata kupitia mgonjwa wake huyo zinaonesha kwamba huko kwa mganga wa jadi aliambiwa kwamba kwenye macho yake kuna mawe aliyoingiziwa kichawi na hivyo mganga wa jadi akawa anampa dawa ili kumtoa mawe hayo.
“Lakini hali ilipozidi kuwa mbaya alirudi tena hapa hospitalini. Lakini kwa sasa yuko hatarini kupatwa na upofu, kutokana kuwapo kwa uchafu (usaha) ndani ya jicho. Huyu hakupaswa kufikia kuhatarisha uoni wake kama angeendelea na matibabu tuliokuwa tunampa,” anasema. Anasema kwamba hali kama hiyo ilimpata mgonjwa mwingine kutoka wilaya ya Kilwa mkoani Lindi ambaye pia katika maelezo yake baada ya ‘kujisalimisha’ hospitalini yanaonesha kwamba alipokwenda kwa mganga wa jadi baada ya kusumbuliwa na macho aliambiwa kwamba eti ametupiwa kitu kibaya kinachomletea madhara machoni.
“Huyu naye baada ya kutopata nafuu, huku hali ikizidi kuwa mbaya, ndipo akalazimika kuja hosipitalini kupatiwa tiba. Lakini alikuja akiwa ameshachelewa sana,” anasema. Kuhusu gharama ambazo zinawashinda wengi, hususani wananchi wa vijijini, Dk Machage anasema mgonjwa mmoja anayetakiwa kufanyiwa operesheni kubwa inamgharimu kati ya Sh 200,000 na 300,000, kutegemea hali ya jicho na dawa zinazohitajika.
Anasema operesheni ndogo ya jicho inagharimu Sh 20,000. Hata hivyo, Dk Machage anasema hospitali hiyo ya Rufaa ya Sokoine, Lindi, ina upungufu wa vifaa tiba vya macho. “Hata hivi vichache vilivyopo nilivitafuta mwenyewe baada ya kumpata rafiki yangu kutoka nchini Ujerumani na kuniletea kwa gharama ya Sh milioni 2.4 mwaka jana,” anasena. Dk Machage anawaomba wadau wa afya ya macho kujitokeza kuwafadhili wagonjwa hao ambao wanazidi kuongezeka mkoani humo huku baadhi yao wakiwa katika hatari ya kupata upofu wa kudumu.
Ufadhili unaotakiwa ni pamoja na kuisaidia serikali kwa kununua vifaa tiba vya macho. Anafafanua kwamba, kama ambavyo umekuwa ukitolewa ufadhili wa magonjwa mbalimbali, ni vyema pia wagonjwa wa macho nchini, wakiwemo wale wa Lindi wakakumbukwa kwani wengi hawana uwezo wa kumudu gharama na hasa kwa kuzingatia kwamba macho ni kiungo muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu.
Anasema unapokuwa na watu takribani 800 wanaotishiwa na upofu kwa ajili ya umaskini, maana yake ni kwamba watu hawa watakuwa maskini zaidi watakapokuwa vipofu kwani itakuwa vigumu kwao kushiriki shughuli za uzalishaji mali. “Kama nilivyosema, wenye kipato cha chini hawawezi kumudu gharama za matibabu na hivyo huamua kwenda kwa wataalamu wa kienyeji au kuvumilia hatimaye kuwa vipofu,” anasema.
Anaongeza kwamba elimu pia kupitia vyombo vya habari inahitajika ili kuwafanya watu wenye matatizo ya macho waende hospitalini na siyo kwa waganga wa jadi. Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Lindi, Yusufu Sonda anakiri kuwapo na wagonjwa wengi wa macho mkoani humo. Anasema kwamba hali inayowakabili wagonjwa hao ni pamoja na elimu ndogo juu ya afya ya macho sambamba na umasikini wa kipato.
“Elimu au uelewa mdogo na wakati mwingine hali duni ya kipato ndio inayochangia watu kwenda kwa waganga wa jadi ambao hawana ujuzi na tiba za macho badala ya kukimbilia hospitali,” anasema Dk Sonda. Dk Sonda naye anakiri kwamba kuna upungufu wa vifaa tiba na kwamba hata wataalamu wa macho katika hospitali yake ni wachache wasiyokidhi mahitaji ya mkoa kuanzia ngazi ya wilaya hadi rufaa.
Anasema kwamba kuna umuhimu mkubwa wa wadau na wafadhili wanaoguswa kujitokeza ili kusaidia jamii ambayo iko hatarini kupatwa upofu. Anasema, hata hivyo, kwamba juhudi zinafanywa na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na taasisi ya ushawishi baina ya serikali ya China na Tanzania ili kuwaleta tena wataalamu bingwa wa magonjwa ya macho mkoani Lindi. Anasema wataalamu hao waliwahi kuja na kutibu wagonjwa wa macho kwa muda wa siku mbili, lakini wagonjwa hawakumalizika.
Anasema tatizo la macho ingawa ni kubwa kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60, lakini linawakabili hata wenye umri chini ya miaka hiyo hadi watoto. Anasema ukiacha wale wanaopata matatizo ya macho kutokana na magonjwa, wakazi wa vijijini hupata matatizo ya macho kutokana na shughuli zao zikiwemo za kukata kuni ambapo vijiti huwaingia machoni kwa bahati mbaya na kuwasababishia majeraha.
Hata hivyo, anasema presha ya macho ndilo tatizo kubwa hasa kwa wakazi wa Lindi wenye umri mkubwa na kwamba wanaochelewa kufika hosipitalini huweza kukabiliwa upofu. Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi anasema kwamba kutokana na ukubwa wa tatizo, juhudi zinafanyika ili kuleta wataalamu wa tiba kutoka China ili kutoa tena tiba hiyo ya macho pamoja na magonjwa mengine.
CHANZO: HABARILEO