Featured Post

KUTOWEKA KWA BEN SAANANE NI MKAKATI WA KUTEKELEZA ‘OPERESHENI KATA FUNUA’!



Na Daniel Mbega
KUMBE unaweza kujitekenya mwenyewe ukacheka.
Naam. Ndivyo inavyoonekana kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema.
Tangu kutoweka kwa Ben Saanane, Katibu Myeka wa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, sasa tunashuhudia mambo mengi ambayo yanazidi kuwachanganya wananchi bila kujua hasa hatma ya mwanasiasa huyo kijana.

Ben anadaiwa kutoweka tangu Novemba 18, 2016 na mpaka sasa ‘hajulikani aliko’.
Kauli za viongozi wa chama hicho – Mwanasheria Tundu Lissu na Mwenyekiti Mbowe – zinaonekana kuwa na nyufa mahali fulani na kuzidisha mashaka.
Lissu akizungumza na wanahabari Jumatano, Desemba 14, 2016 alisema kwamba mara ya mwisho kwa Ben Saanane kuwasiliana na bosi wake Mbowe ilikuwa Novemba 14, 2016.
Lakini kuna taarifa nyingine zinazoelezea kwamba, Jumanne, Novemba 15, 2016, Ben alitambulishwa Bungeni kama mgeni wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa. Kwa maana nyingine alikuwepo ama alitakiwa kuwepo Bungeni siku hiyo.
Hii maana yake ni kwamba, Mbowe alikuwa na Ben siku hiyo huko Dodoma na inatengua kauli ya Lissu kwamba wawili hao waliwasiliana mara ya mwisho Novemba 14.
Alhamisi Desemba 22, 2016 wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa uliofanyika jijini Mbeya, hatimaye Mbowe naye akavunja ukimya, ikiwa ni siku 45 tangu Ben alipotoweka.
Mbowe alikaririwa akisema: “Mambo mengine yanapokuwa katika masuala ya kiuchunguzi siyo kila jambo litasemwa hadharani wakati wote, na tunatambua jambo hili lina hatari, linahusu maisha ya mtu, sasa siyo kila wakati kusema kuyarahisisha.
“Unaweza ukasema kumbe kwa kusema sana unawaruhusu na watesi wake pengine waweze kumtoa roho. Kwa hiyo kuna mambo mengine ni sensitive (nyeti), siyo mambo ya kuzungumza rahisi sana. Tunafanya kazi kwa njia mbalimbali kama chama cha siasa na tunakuwa waangalifu sana kuhusiana na tuseme nini kwa wakati gani na kwa taratibu gani lakini kwamba chama kinafuatilia suala hili, kinawasiliana na vyombo mbalimbali. Chama kina vyombo vyake vingine vya ndani ambavyo vinafanya jambo hili lichunguzwe kwa makini.
“Tuko hivyo na tunawahakikishia wote kwamba muda muafaka ukifika tutaweza kutoa taarifa za kina tumekwamia wapi na nini kifanyike cha ziada,” alisema Mbowe.
Hii siyo kawaida ya kiongozi huyo ambaye anafahamika kwa kuyasemea mambo mengi kila yanapotokea, hata kama yanaihusu serikali na chama tawala, CCM.
Mbowe, ambaye Watanzania wengi wanaofuatilia siasa wanamjua, asingeweza kukaa kimya hata kwa siku mbili, achilia mbali siku 45 zote, baada ya kutoweka kwa msaidizi wake binafsi, ambaye ndiye ni mshauri wake wa masuala ya siasa.
Ukimya wake huo umeleta tafsiri hasi katika jamii hasa katika kipindi ambacho Chadema, baada ya kushindwa kwa Operesheni Ukuta, imetangaza kuja na Operesheni Kata Funua.
Tunaambiwa Ben Saanane ndiye aliyeandaa andiko la operesheni hiyo kabla ya kupewa ‘likizo’ na Mbowe kwa ‘kazi nzuri’ aliyoifanya.
Tafsiri iliyopo ni kwamba, kutoweka kwa Ben Saanane huenda ni mojawapo ya mikakati ya kutekeleza Operesheni Kata Funua, na kwa maana hiyo tunalazimika kuamini kwamba hivi sasa operesheni hiyo inaendelea bila Watanzania kuelewa.
Ni nani anayejua kilichomo katika mkakati wa Operesheni Kata Funua zaidi ya Ben Saanane mwenyewe na viongozi wa juu wa Chadema?
Hakuna anayejua kama Ben ametekwa, ametoweka tu, kapotea ama ‘kajiteka’ mwenyewe kwa maana ya kujificha, lakini Mbowe alithubutu kutamka kwamba, kama jambo hilo litazungumzwa sana ‘watesaji wanaweza kumdhuru’ huko aliko!
Tuamini kwamba ametekwa, kapotea ama katoweka tu? Kwamba kumbe kiongozi wa chama anafahamu Ben ametekwa?
Pamoja na hayo, hakuna aliyekanusha wala kuthibitisha taarifa zilizoenea mitandaoni kwamba Ben Saanane alilipiwa nauli na gharama za matumizi ili akapumzike Afrika Kusini. Hakuna.
Tunatambua suala hilo liko kwenye uchunguzi wa vyombo vya dola, lakini kwa namna linavyoshughulikiwa na viongozi wa Chadema, ambao wanafahamika vyema kwa kauli tata za mashambulizi dhidi ya serikali, linaleta mashaka makubwa kama siyo mpango mahsusi wa kuhakikisha harakati za chama hicho zinarejea tena.
Wakati watu wanaendelea kuhoji wapi aliko mwanasiasa huyo, ghafla gazeti la kila wiki (Mwanahalisi) linalomilikiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, limeandika kwamba ati Ben anaonekana akizurura mitaani na kwenye vijiwe vya kahawa, pamoja na kuwatembelea jamaa zake.
Tunaambiwa kwamba, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya Chadema aliwahi kulidokeza gazeti hilo kwamba Ben yupo na ipo siku ataibuka.
"Nina wasiwasi kama siyo mkakati binafsi wa kisiasa. Saanane amekuwa akionesha kutaka kukwea madarakani haraka hata nje ya taratibu. Huu waweza kuwa mtego kwa Mbowe." Anadaiwa kukaririwa mjumbe huyo wa CC ya Chadema.
Lakini tunazidi kufahamishwa kwamba, gazeti hilo lilipata ‘andishi la mkono’ lililopenyezwa kwenye mlango wa ofisi Jumapili, Desemba 25, 2016 ikieleza kuwa wanajisumbua bure kwa sababu ‘mtoto huyo yupo’.
"Ninyi jisumbueni tu. Huyu mtoto yupo na akitokea mtashangaa. Hamumfahamu Saanane. Sisi tunajua alipo. Wala hatuoni anayetishia maisha yake. Kuna wanaodai kauawa. Ni waongo. Anapumua. Kuna kitu wanaandaa. Kaa chonjo.” Sehemu ya andishi hilo inanukuliwa na Mwanahalisi.
Habari hiyo kubwa kwenye gazeti hilo imezua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu muafaka, kwa sababu inavyoonekana ni kama njia ya kumsafisha Mwenyekiti Mbowe na sakata hilo ambalo linazidi kuleta utata.
Kwamba sasa Ben anatuhumiwa ‘kujiteka’ mwenyewe kwa sababu anataka kukwea madaraka nje ya taratibu? Na huo mtego kwa Mbowe ni wa aina gani ambao Ben ameutega?
Kuhusu andishi linalosemwa, ni kwa nini itokee tu likapenyezwe kwenye ofisi za Mwanahalisi wakati kuna magazeti mengi hapa Dar es Salaam? Kwa nini lisipenyezwe kwenye ofisi za Raia Mwema ambao ni jirani zao pale Kinondoni? Kwa nini lisipenyezwe kwenye ofisi za Mtanzania, Mwananchi au hata Uhuru?
Kilicho wazi ni kwamba, Chadema wamejitekenya, na sasa wameamua kucheka kabisa. Kama walikuwa wanataka kutumia kutoweka kwa Ben kama sehemu ya mkakati wao wa Operesheni Kata Funua, basi wameanza vibaya na operesheni hiyo haiwezi kufanikiwa, labda kwa huku kuandikwa mara kwa mara tu.
Kama kuna hila yoyote imefanyika na sasa wanaona mambo yamekaa vibaya hivyo kuamua kutunga habari na kuanza kusafishana, ni wazi Watanzania siyo wajinga kiasi hicho, wanaweza kubaini pumba na mchele.
Vinginevyo, ni hatari sana kucheza na maisha ya mtu kwa sababu ya kutimiza utashi wa kisiasa.
Kama Chadema wanajua aliko Ben, basi wamrejeshe ili kujijengea heshima, tofauti na hapo hakuna atakayewaelewa na mchezo wao huu wa ‘kombolela’!

Mwisho.

Comments